Makala

MAONI: Wanaopuuza uwezo wa Gachagua kuwa rais hawajasoma historia

Na DOUGLAS MUTUA May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

JE, Bw Rigathi Gachagua, aliyekuwa naibu rais, anaweza kuchaguliwa rais wa Kenya?

Swali hili liliulizwa katika kikao cha wazee waliotokea Mlima Kenya, ambacho nilihudhuria mwishoni mwa wiki jana kwenye jimbo la Virginia, Amerika. Lilizuua kicheko kikuu na cha muda mrefu sana.

Jawabu ya haraka iliyotolewa ni kwamba Bw Gachagua hajaiva kiasi cha, si kumshinda Rais William Ruto pekee, bali pia kuongoza nchi nzima ya Kenya. Hana tajiriba wala ukomavu unaostahili, ilidaiwa.

Wengi waliojadili suala hilo walidai eti ufuasi ambao Bw Gachagua anaonekana kuwa nao umetokana na kuhurumiwa na watu wanaohisi kwamba alidhulumiwa kwa kutimuliwa mamlakani mwishoni mwa mwaka jana.

Wazee hao walisema kuwa bwana huyo ni wingu linalopita tu, eti Mlimani ataibuka mtu mwingine atakayeungwa mkono kikweli, Bw Gachagua asahaulike, hasa kutokana na ulimi wake mkali.

Wakati wote mazungumzo hayo yalipokuwa yakiendelea, binafsi nilikaa kimya na kutabasamu tu kwa kuajabia ukosefu wa taarifa ambao umewagubika watu wengi wa tabaka la kati, ambao wanadhani wanaweza kuamulia nchi kila kitu.

Nilipoombwa kutoa maoni yangu, niliwavunja mioyo kwa kuwaambia kuwa mtazamo wao huo haukuwa sahihi, na kwamba hakuna aliye na hakika ya Kenya itakuwaje kisiasa siku zijazo.

Nililazimika kusema hayo kwani historia inanionyesha kuwa wakati fulani hufika, nchi ikachoshwa na watawala wake, ikaamua kuwaadhibu kwa kuwabandua, ikawapa wasiotarajiwa fursa ya kuiongoza.

Na nchi inapoamua kufanya hivyo, haijalishi kwamba viongozi wanaopewa fursa ya kuongoza wana hulka mbaya au bora kuliko wanaobanduliwa.

Lengo kuu huwa mtesi wa sasa aondoke, aje mwingine tujaribishe bahati. Ni kwa mintaarafu hiyo ambapo majeshi hushangiliwa kwa jazba na raia yanapopindua serikali nduli za kiraia.

Imani ya kila mja wakati huo huwa kwamba serikali nyingineyo ni bora kuliko hii! Hiyo ni nafasi mbaya sana kwa mtawala yeyote kujipata, hasa ikiwa alichaguliwa kwa wingi wa kura.

Jambo la hakika unalopaswa kujua ni kwamba kuna mambo ambayo hayawezi kufanyika nchini Kenya, kama vile mapinduzi ya kijeshi. Kutokana na maslahi yake, Amerika haiwezi kumruhusu yeyote kutwaa mamlaka kwa jinsi hiyo.

Kwa ajili ya kujali mwonekano wa mambo, sharti kila mtu achaguliwe katika uchaguzi wa huru na haki au vinginevyo. Hiyo ni nira ambayo Amerika imeyavisha mataifa manne muhimu ambayo kwayo inatawala Afrika: Kenya, Afrika Kusini, Ghana na Misri.

Ikiwa una shaka kuhusu uwezekano wa Bw Gachagua kuwa rais, nakuomba utafakari tena. Na ikiwa una uwezo wa kumfikishia rais William Ruto taarifa hii, usisite kufanya hivyo.

Nchi ikihangaika sana, ihisi matatizo yake yamefikia kilele, inatafuta yeyote kuiondolea dhiki hiyo, Mtu huyo akibahatika kuwa Bw Gachagua, hasa kutokana na ujasiri wake na kutojali anapotamka mambo ya kuogofya, basi inampa kazi hiyo.

Mnamo mwaka 2002, ilipobainika wazi kwamba Daniel Moi alinuia kusalia mamlakani kupitia mradi ulioitwa Uhuru Kenyatta, viongozi wengi wa upinzani na baadhi kutoka serikalini walikumbuka matatizo ya kiuchumi aliyoleta Moi wakaamua ‘imetosha’!

Bila kushurutishwa, waliamua kuwa mtaalamu wa uchumi aliyewapiku wote wakati huo alikuwa Mwai Kibaki, wakamuunga mkono kwa fujo na akawa rais.

Dkt William Ruto mwenyewe alifaidika kutokana na uchovu wa viongozi na wananchi waliohisi kwamba Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta alinuia kumrithisha Bw Raila Odinga urais visivyo.

Wakati hufika nchi nzima ikaulizana: Nani miongoni mwetu anayeweza kumkabuili na kumshinda mtesi wetu? Ni kisa cha panya walioliwa na paka kupitiliza, wakaulizana ni nani anayeweza kumvisha paka kengele ili wamsikie akiwanyemelea.

Wakisuasua, au akatokea mmoja wao jasiri wa kuaminika, hata akiwa na madhaifu ya aina gani, hayo hupuuziliwa mbali akapewa jukumu la kiondolea nchi janga. Rangi ya paka si hoja, bora anase windo eti.

Rais Ruto ana jukumu la kuhakikisha utawala wake hauchukiwi na wananchi kiasi hicho. Hilo litawezekana tu kwa kutimiza ahadi zake, badala ya kutoa ahadi mpya, na kuhakikisha kuwa idara yake ya mawasiliano inatangaza hatua anazopiga.

Kwa sasa, ithibati ya pekee kwamba Dkt Ruto anatimiza ahadi zake miradi wa ujenzi wa nyumba za gharama ya chini.

Kumbuka chuki na vuta-nikuvute iliyoletwa na mradi huo, hasa kutokana na makato ya shuruti ya mishahara ya watu!

Wengi wamekasirishwa na uuzwaji wa nyumba zenyewe kwa watu wasiochangia chochote, na ambao hauwafaidi kwa vyovyote wanaokatwa mishahara.

Kati ya sasa na Uchaguzi Mkuu ujao, Dkt Ruto pekee ndiye anayeweza kumkosesha Bw Gachagua tiketi ya urais ya muungano wa upinzani kwa kuwapunguzia wananchi mateso wanayopitia.

Na atakuwa amejifaa sana akiepuka majibizano ya wazi na upinzani yanayosababisha achukiwe zaidi. Umma unaotafunwa na ugumu wa maisha unawachukia, hadi ya kuwachukia, viongozi wanaoonyesha dalili za jeuri na kiburi.

[email protected]