Makala

Maono yanavyosaidia kukabiliana na changamoto katika biashara

March 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA BENSON MATHEKA

Ikiwa hauna maono, usiharibu pesa zako kuanzisha biashara kwa kuwa hautafaulu hata kama umeisomea.

Na ukiwa na maono, ni lazima uipende biashara unayonuia kuanzisha ili uweze kuifanya vyema ifaulu.

“Baada ya kujifunza kazi  ni lazima mtu awe na maono ya kukuza kazi yake, pasipo na maono, utaangamia,” asema Dkt Newton Kariithi mtaalamu wa masuala ya biashara na ajira anayehudumu jijini Nairobi.

Anasema muhimu kabisa kwa kazi na biashara ni kufahamu inavyofanywa, kuelewa changamoto zake na jinsi ya kuzitatua.

Mfanyabiashara Joshua Gitonga akionyesha mafuta anayosindika Meru. PICHA|SAMMY WAWERU

“Umuhimu wa kujifunza kazi ni kwamba hata changamoto zikija, unaweza kukabiliana nazo. Changamoto ni kawaida katika kazi yoyote ile. Ukiielewa kazi yako utaweza kukabiliana nazo zikiibuka,” aeleza.

Lakini ukikosa maono, anaongeza, hautaweza kujua jinsi ya kukabiliana na changamoto hata zile ndogo na hii inaweza kuporomosha biashara na kukufanya ushindwe na kazi yako.

Wanachokosea watu wengi ni kuanza biashara au kuajiriwa wakidhani kila kitu kitakuwa mteremko kwao.

“Watu wengi hukosea kwa kutotarajia changamoto katika kazi au biashara wanazofanya. Kuna mabonde na milima katika biashara na kazi, hali si tambarare kila wakati. Kuna nyakati za dhoruba kali inayoyumbisha mtu, kazi na hata biashara yake,” asema Bw Kariithi.

Joshua Gitonga na mfanyabiashara mwenza kwenye duka lake la mafuta eneo la Meru. PICHA|SAMMY WAWERU

“Ikiwa umesomea kazi unayofanya au unaelewa biashara na una maono, hautavunjwa moyo na watu kwa sababu utakuwa ukijua unachofanya. Lakini ikiwa hauelewi kazi unayofanya au hauna maarifa ya biashara yako, ni rahisi kuvunjika moyo na kushawishiwa na watu ambao baadhi huenda hawana  nia njema,” asema.

Mtu aliye na maono na anayefahamu kwamba dhoruba zinaweza kutokea, anajua wakati wa kubadilisha mkondo wa biashara, wakati wa kuongeza bidhaa na wafanyakazi na wakati wa kuzipunguza.

Dkt Kariithi anasema ni muhimu mtu kuongeza maarifa ya kazi mara kwa mara ili kwenda na wakati.

Mfanyabaishara Joshua Gitonga akionyesha mafuta anayosindika. Wafanyabiashara wanashauriwa kuwa na maono. PICHA|SAMMY WAWERU

“Dunia inabadilika kila wakati na mambo mapya kuibuka. Kizazi cha sasa si sawa na cha jana na cha kesho hakitakuwa sawa na cha sasa. Wateja wa jana sio wale wa leo na wa kesho hawatakuwa wa leo. Hivyo basi mafunzo ya mara kwa mara yatakuongezea maarifa ya kuimarisha biashara yako kwenda na wakati,” ashauri mtalaamu huyo

Miongoni mwa mafunzo ambayo watu wanahitaji kukumbatia, aeleza Bw Kariithi, ni ya teknolojia ya habari na mawasiliano na ubunifu wa biashara.

“Ufanisi wowote katika kazi, biashara na hata maisha ya kila siku ya mtu hutegemea teknolojia ya habari na mawasiliano na ubunifu wake. Teknolojia hii inabadilika kwa haraka na ni lazima mtu abadilike nayo iwapo ni mtu aliye na maono anaweza kung’amua hili,” asema na kuongeza kuwa teknolojia ya sasa sio itakayotumiwa kesho.

“Kila shirika la kibiashara linatoa huduma kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo inabadilika kila uchao. Ni wale wanaoenda na wakati ambao watafaulu kibiashara,” ashauri.