• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mapenzi matamu, yanabomoa kuta za matabaka   

Mapenzi matamu, yanabomoa kuta za matabaka  

NA BENSON MATHEKA

MOSES, 26, na wazazi wake wametofautiana kwa sababu ya mpenzi wake.

Anasema wazazi wake wanataka atamatishe uhusiano wake wa mapenzi wakisema kuwa msichana anayechumbia sio wa tabaka lao na hawawezi kumkubali kama mke wa mwana wao.

Lakini Moses anashikilia kwamba anampenda mwanadada huyo kwa dhati na hawezi kumwacha kamwe.

“Siwezi kulazimishwa kumuoa msichana ambaye simpendi,” asema.

Kwa wakati huu Moses anapanga kuhama nyumbani kwa wazazi wake katika mtaa wa kifahari wa Lavington ili akaishi na mpenzi wake katika mtaa wa Donholm mashariki mwa jiji la Nairobi.

Moses anafananisha masaibu yake ya Prince Harry wa Uingereza aliyelazimika kuvua wadhifa wake katika familia ya kifalme kwa sababu ya mapenzi.

Alichukua hatua hiyo baada ya familia ya ufalme kumdhalilisha mkewe Meghan aliyechukuliwa kuwa wa tabaka la kina yakhe.

Watalaamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwa kiwango kikubwa tofauti za kitabaka zinaweza kuathiri uhusiano wa mapenzi.

Wanasema ingawa siku za mwanzo wachumba wanaotoka matabaka tofauti wanaweza kutawaliwa na hisia na mvuto wa mapenzi, tofauti zinazoweza kusambaratisha penzi hujitokeza baadaye wasipokuwa waangalifu kuzishinda.

Kulingana na mwanasaikolojia Tamar Lewis sio mali pekee inayoweza kuwa kikwazo katika uhusiano wa aina hii. Lewis asema katika makala yake kwa jina when the richer and the poorer love yaliyochapishwa katika gazeti la The New York Times kwamba tabaka linaweza kuhusisha pia toauti za dini.

“Sawa na tofauti za mali na elimu, imani za kidini huathiri uhusiano wa mapenzi,” asema na kuongeza kuwa watu wanafaa kutafakari kuhusu wanakotoka kabla ya kujiingiza katika uhusiano wa mapenzi.

Hata hivyo, anasema wazazi hawafai kulazimisha watoto wao kuoa wachumba wasiowapenda akisema nyakati hizo zimepitwa na wakati.

Moses asema wazazi wake wanamshinikiza aoe msichana mwingine kutoka familia tajiri kama yao.

“Simpendi na siwezi kumwoa,” asema na kuongeza kwamba ameridhika kuishi mtaa duni karibu na msichana anayempenda.

“Anamaanisha kila kitu maishani mwangu,” asema.

Katika makala yake Lewis asema wazazi wanaowashinikiza watoto wao kuoa wasichana wa tabaka lao wanawanyima fursa ya kufurahia maisha.

Hata hivyo, anasema watu wanaoamua kuoa au kuwa na uhusiano wa mapenzi na watu wasio wa tabaka lao wanaweza kujikosesha raha maishani.

“Watu wanaopenda watu wasio wa tabaka lao hujikosesha raha maishani. Hii ni kwa sababu mipango na fikira za watu walio na mali au kiwango mbalimbali vya elimu ni tofauti” asema.

Bi Helen Njihia mshauri na mwelekezi wa wanandoa katika shirika la Dating Bells asema vijana wengi wa matajiri wanaamua kuoa wasichana wasio wa tabaka lao wakisema vipusa kutoka familia tajiri hawajui kudumisha penzi.

“Nimeona vijana wengi kutoka mitaa ya matajiri wakioa wasichana wasio wa tabaka lao. Wanasema wasichana wa matajiri hawadhamini mapenzi,” asema.

“Siku hizi watu wanatafuta raha maishani. Haina haja ya kuoa msichana atayekufanya ukose usingizi. Heri kuoa msichana asiye wa tabaka lako ambaye atakuheshimu,” asema na kuongeza kuwa hii haimaanishi kuoa msichana aliye na elimu ya chini.

Njihia asema penzi ni zaidi ya elimu na tabaka.

“Ni maisha yako na hakuna asiyependa raha maishani,” aongeza.

Lakini Jimmy Kandie, 26 mkazi mtaa wa South C Nairobi anasema cha muhimu sio tabaka bali ni chaguo la mtu.

Anasema vipusa wa tabaka la juu hawawezi kulinda penzi jambo ambalo limewafanya vijana wengi wa kiwango chao kugeukia warembo wa matabaka ya chini.

Anatoa mfano wa wasichana wanaoamini kwamba kwa sababu wana pesa hawawezi kunyenyekea kwa wanaume.

“Ni vigumu kwa mwanaume kuvumilia mwanamke wa sampuli hiyo,” asema.

Kijana huyo asema kuna watu wanaojuta kutokana na jinsi mapenzi yanavyowatesa. Anasema dhamira ya mtu kupenda ni kupata furaha maishani  na wanapobahatika kuwa na wapenzi ambao wanayageuza maisha yao kuwa yenye furaha wanawakumbatia bila kujali tabaka wanalotoka.
“Ukimpata mpenzi anayewasha moto wa furaha katika maisha yako mshikilie. Usijali tabaka lao mradi muelewane,” asema

Kulingana na Njihia kupenda ni upofu, anasema ni vigumu kuzuia moyo kupenda.

“Na kuuzuia moyo ukipenda ni kujiweka katika majuto. Kipendacho moyo ni dawa” asema.

Mtaalamu huyu asema kuna watu wanaolia kwa sababu waliingia katika uhusiano wa kimapenzi na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati ila waliwaoa watu wa tabaka lao wasionekane kujishusha hadhi.

Bi Susan Kahoro, 30, mkazi wa mtaa wa Kileleshwa asema hatajali kuolewa na mwanaume asiye wa tabaka lake.

Hata hivyo, anasema lazima penzi kama hilo liwe la dhati na wala sio tamaa.

“Ikiwa penzi la aina hii litaongozwa na tamaa halitadumu.

Kwa upande wangu sina shida na kuolewa na mwanaume asiye wa kiwango changu. Bora tuelewane na tuheshimiane” asema.

Kahoro anakiri kwamba uhusiano kama huu unakabiliwa na changamoto nyingi na kusema penzi la kweli linahimili dhoruba za kila aina.

Lakini Tabitha Wanjala, mkazi wa mtaa wa Parklands anaapa kwamba hawezi kushiriki uhusiano na mwanaume siye wa kiwango chake.

“Natamani mwanaume atakayepalilia kile wazazi wangu wamepanda ndani yangu. Kuolewa na kijana asiye wa kiwango changu ni kujishushia hadhi na kuwafedhehesha wazazi wangu,” asema.

George Maketi, 33, aliyezaliwa na kukulia katika mtaa wa Westlands hana tatizo lolote na vipusa wasio wa tabaka lake.

Anasema kwa miaka mingi amechumbiana na msichana kutoka mtaa wa Huruma na sasa wanapanga kuoana.

“Ikiwa uhusiano umejengwa kwa misingi ya penzi la dhati tabaka halifai kuwa kizingiti cha ndoa. Penzi hufanya watu kuvumiliana na kufunzana mambo mengi,” asema.

Wataalamu wanasema tafiti zimeonyesha kwamba ndoa nyingi za watu wanaotoka matabaka mbalimbali hatimaye huvunjika.

Wanataja tofauti za kielimu, kuzaliwa na kukulia katika mazingira tofauti kama zinazofanya uhusiano kutoafaulu.

Hata hivyo, wanasema dawa la penzi ni kutoingiliwa na watu wa nje na wa familia.

 

  • Tags

You can share this post!

Michango ya mitandaoni yageuka karaha kwa Wakenya wakarimu

Washukiwa 12 mbaroni kwa kupatikana na chang’aa

T L