MAPENZI: Ushauri wa mzee Olengetui kuhusu uhusiano wa kimapenzi na ndoa
Na SAMMY WAWERU
MZEE Joseph Olengetui ni mkwasi wa ushauri na wosia kila unapokutana naye na kufanya mazungumzo.
Ni mcheshi, na kuanzia mada ya uhusiano wa ndoa, uchumba na jinsi ya kutangamana na kuishi na watu, amebobea katika ushauri nasaha ikizingatiwa umri wake. Wanasema kuishi kwingi kuona mengi.
Anakasirishwa na mauaji ya mara kwa mara; chanzo kikiwa ni migogoro katika ndoa na uhusiano, visa ambavyo vimeonekana kukita mizizi katika siku za hivi karibuni.
Mzee Olengetui, 77, akijaribu kulinganisha vijana wa kizazi cha sasa na cha wakati wake, anaona kuna tofauti kubwa kabisa kinidhamu na kimaadili. Bw Olengetui, ni mzaliwa wa kaunti ya Samburu na anasema akiwa kijana, vijana wa rika lake kila jioni wasingekosa kushiriki kikao cha babu, ambaye aliwashauri mambo mengi tu.
“Kabla kupashwa tohara, baba na babu walifanya kikao na vijana na wajukuu, shabaha ikiwa kutushauri. Mazungumzo yalikuwa mapana, kuanzia kuvuka daraja la ujana kuwa mzee, majukumu ya mzee kwenye ndoa na jinsi ya kutambulika mzee wa boma,” afafanua.
Mazungumzo yaliegemea kuheshimu waliowazidi umri, rika lao, na wale wadogo, ikiwa ni pamoja na heshima kwa jinsia ya kike.
Isitoshe, Mzee Olengetui anasema walinolewa makali namna ya kurusha chambo au mistari ya mahaba kwa mwanamke, na jinsi ya kumuongelesha pamoja na kumtunza wanapochumbiana.
“Mume ndiye kiongozi au kichwa katika boma; na anapasa kujua majukumu yake. Mke naye, ni shingo, amheshimu na kumtumikia na kuafikia mahitaji ya ndoa,” ashauri.
Kulingana naye, yote hayo msingi wake ulikuwa kwenye vikao vya mara kwa mara, chini ya babu na wazee waliojawa na ushauri nasaha. Wasichana nao, lilikuwa jukumu la nyanya na mama zao kufanya mazungumzo, lengo likiwa kuwanoa kuwa wake na kina mama bora.
“Jamii ya Samburu inaruhusu mzee kuoa zaidi ya mke mmoja, na licha ya changamoto za ndoa zisizokosa, visa tunavyosikia siku hizi hasa vya mauaji, havikusikika wakati wetu,” Bw Olengetui aeleza akionekana kushangazwa na mauaji ya walio kwenye uhusiano na ndoa jinsi yalivyoenea.
Kwa mtazamo wake, upuuzaji wa mila na itikadi za kijamii ndio chanzo cha masaibu yanayozingira kizazi cha kisasa. Anahisi endapo mila na tamaduni za kila jamii zingetiliwa mkazo na kufufuliwa, kizazi cha kisasa huenda kikapevuka.
Isemwavyo, mwacha ni mtumwa, Mzee Olengetui anaonya isitarajiwe mila na utamaduni wa jamii upuuzwe, halafu kizazi cha kileo kiwe na maadili mema. Kwa kuzipiga teke na kuiga za ughaibuni, bila shaka mshauri huyo anasema vijana wa kileo hawatakuwa na budi ila kupotoka kimtindo, kimaadili na kitabia.
Ni mwishoni mwa mwaka uliopita, 2019, msichana wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 16, Valerian Njeri, anadaiwa kuuliwa kinyama na mvulana mwenye miaka 17, katika kile kinachosemekana msichana kukataa ombi lake la mapenzi.
Aidha, kisa hicho ni mojawapo ya vingi tu ambavyo viligonga vichwa vya vyombo vya habari 2019.
Kulingana na mzee Olengetui, kitendo cha aina hiyo kinaashiria ukosefu wa maadili miongoni mwa vijana wa kisasa.
“Wazazi wawashirikishe watoto wao kwenye ushauri nasaha na zaidi ya yote wawalee kwa msingi dini na kumuogopa Mwenyezi Mungu,” asisitiza.
Kauli yake inaonekana kuwiana na ya mzee Boniface Macharia, 74, akihimizia haja ya wazazi kuelekeza watoto kanisani au misikitini.
“Ni vyema kuhusha watumishi wa Mungu katika malezi ya mtoto,” asema Bw Macharia.
Wazee hao kwa kauli moja wanaafikiana kwamba wazazi wa kisasa wana majukumu mengi na makuu katika ulezi, muhimu zaidi wakisisitiza “utamaduni, mila na itikadi za jamii zitiliwe maanani”.
Hata ingawa kuna zile potovu, kama ukeketaji wa wanawake (FGM) wanasema za aina hiyo ziepukwe na kukumbatia zile faafu. Vita vya kijinsia wanavikashifu, wakisema vya kisasa vimevuka mipaka.
Vitabu vya kidini, hasa Biblia na Kurani, vinakashifu mauaji, na kwa mujibu wa wazee hao haja ipo vijana kukumbushwa kupitia sheria hizo.
Bw Joseph Olengetui anashangazwa na wazazi wa kileo kutekwa nyara mawazo na teknolojia ya kisasa kama vile mitandao, ambayo wanatumia muda mwingi kwayo. Badala yake, muda huo, hasa jioni anasema unapaswa kutumika katika malezi ya watoto. “Watoto hao wakati mmoja watakuwa wazazi. Wanaiga wanachofanya wavyele wao. Changamoto tunazoshuhudia zitaendelea kuibuka na hata kukithiri kwa watoto wa kizazi cha sasa endapo hawatapata malezi bora,” anaonya mzee huyo.
Mzee Olengetui anasema lisiwe jukumu la mzazi mmoja katika malezi, ila washirikiane, yaani mume na mke. Anasema mume alainishe mtoto au watoto wa kiume, naye mke wa kike, na ikiwezekana kuwe na kikao cha pamoja ili kuwaonesha umoja, utangamano na uwiano.