MakalaSiasa

MAPINDUZI 1982: Shoka ‘lilivyozima’ njama ya Ochuka

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOSEPH WANGUI

KWA saa chache Agosti 1, 1982, Kenya ilikuwa chini ya utawala wa kijeshi kufuatia jaribio la mapinduzi ya serikali.

Mwanajeshi wa kikosi cha wanahewa, Hezekiah Ochuka ndiye alijitwika mamlaka ya uongozi wakati aliposimamia jaribio hilo la kupindua serikali ya aliyekuwa rais Daniel arap Moi.

Matukio ya siku hiyo hayajafutika akilini mwa mwanajeshi mstaafu Douglas Karanja Wachira.

Bw Wachira, 61, alikuwa miongoni mwa maafisa wa jeshi la wanahewa walioegemea upande wa serikali ambao walitumwa hadi kambi ya jeshi iliyo Eastleigh, Nairobi kukabiliana na Ochuka na wenzake mwendo wa saa moja asubuhi siku hiyo.

“Tulipofika mtaa wa Mlango Kubwa tulipata watu wakipora maduka na mmoja wao alikuwa amebeba shoka dogo. Nilifanikiwa kumpokonya kisha tukazuia waporaji kuvunja maduka,” akasema.

Kile ambacho hawakufahamu ni kwamba, shoka hilo lingewasaidia baadaye kwani ndilo walitumia kukata ua la nyororo na kuingia kambini wakiongozwa na Meja Jackson Tuwei.

Maafisa wa ulinzi waliokuwa langoni Eastleigh walitufyatulia risasi. Tuliondoka hapo tukaenda kutafuta njia nyingine ya kuingilia. Ingekuwa vigumu kwetu kuingia kambi ya jeshi kama singekuwa na shoka hilo nililompokonya mporaji. Si rahisi kuvunja ua kambini kwa kutumia mikono mitupu au hata bunduki,” akaeleza.

Hadi leo, mwanajeshi huyo aliyekuwa akifanya kazi katika kambi ya Lanet, Nakuru, bado amehifadhi shoka hilo kama mojawapo ya kumbukumbu zake za thamani nyumbani kwake Tetu, Kaunti ya Nyeri.

Kulingana naye, jaribio la mapinduzi lilianza mwendo wa saa tisa usiku.

“Ilipofika saa kumi, Brigedia Msomba alikuja mahali nilipokuwa nikilinda. Niliambiwa niwashe king’ora kisha maafisa wote wakakusanyika uwanjani. Tuliambiwa tuchukue silaha zetu mara moja kutoka kwa chumba cha kuzihifadhi,” akasema.

Waliambiwa walihitajika kwenda katika makao makuu ya jeshi Nairobi, ambako wangepewa maagizo zaidi.

Ochuka alikuwa amerudi katika kambi ya jeshi baada ya kutangaza mapinduzi katika kituo cha redio cha taifa cha VoK, lakini akahepa wakati kikosi kilichomjumuisha Bw Wachira kilipowasili.

Baadhi ya wanajeshi ambao Ochuka aliwaacha kulinda VoK walizidiwa nguvu na kuangamizwa.

Katika kambi ya Eastleigh, baadhi ya waasi walikamatwa. Ochuka alitorokea Tanzania baada ya kikosi chake kuzidiwa nguvu.

“Baada ya ndege iliyomtorosha Ochuka kuondoka, hakuna ndege nyingine ilipaa kwani tulichukua udhibiti wa kambi,” akasema.

Ochuka alirudishwa Kenya baadaye, akashtakiwa na kupatikana na hatia ya uhaini kisha akanyongwa.

Bw Wachira alipandishwa cheo kuwa Koplo lakini akastaafu mwaka wa 1989 na akaamua kuwa pasta.

Baada ya kuhitimu kutoka taasisi ya mafunzo ya kidini, alianzisha Kanisa la Prophet and Apostles Faith mwaka wa 1992.