MAPISHI: Jinsi ya kuandaa viazi vya kuponda, kuku na sosi
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 10
Muda wa kupika: Dakika 20
Walaji: 3
Vinavyohitajika kwa viazi
- kilo 1 ya viazi
- lita 1 ya maji
- maziwa ½ kikombe
- vijiko 3 vya siagi
- chumvi
Maelekezo
Menya, osha na kukatakata viazi vipande vikubwa vikubwa.
Weka viazi kwenye sufuria na ongeza maji ya kutosha.
Chemsha mpaka maji yachemke, kisha ongeza chumvi. Chemsha mpaka viazi viive vizuri.
Viazi vikishaiva vizuri, epua kisha chuja maji.
Anza kuponda viazi na uhakikishe hakuna mabonge mabonge.
Ongeza maziwa na siagi mpaka upate uzito na ladha utakayopenda.
Vinavyohitajika kwa kuku
- kilo ½ minofu ya kuku
- pilipili mboga 3 (nyekundu, kijani na njano)
- kitunguu maji 1
- mafuta ya kupikia
- kijiko 1 cha chicken seasoning
- kijiko 1 cha kitunguu saumu na tangawizi
- chumvi na pilipili manga
Maelekezo
Andaa viungo kisha katakata kuku, kitunguu na pilipili mboga vipande virefu virefu.
Kwenye kikaangio katika moto wa wastani, chemsha mafuta, kisha ongeza nyama ya kuku, chicken seasoning, kitunguu saumu na tangawizi.
Kaanga mpaka nyama ikaribie kuiva, kisha ongeza kitunguu maji, pilipili hoho, chumvi na pilipili manga.
Endelea kukaanga kwa dakika chache, mpaka kuku iive vizuri.
Pakua na viazi vya kuponda,mboga na ufurahie.