MAPISHI: Jinsi ya kupika wali wenye korosho
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 15
Muda wa mapishi: Dakika 40
Walaji: 4
Vinavyohitajika
- kilo 1 ya wali uliopikwa
- mchanganyiko wa mboga majani upendazo
- gramu 250 za korosho
- kitunguu saumu
- tangawizi mbichi; osha na katakata
- mafuta ya kupikia
- vijiko 2 vya Soy Sauce
- chumvi
Maelekezo
Andaa kila kitu na kiwe karibu na kikaangio chako kisha washa moto meko yako ili kikaango kipate moto.
Weka mafuta ya kupikia kisha weka korosho na kaanga ziwe na rangi ya kahawia kabla ya kuziepua na kuziweke pembeni.
Kama utatumia nyama ya ng’ombe, mbuzi au minofu ya kuku, unaweza kukaanga pamoja na korosho hizi ili ziive pamoja.
Katika kiaangio hicho, weka kitunguu, tangawizi, na kitunguu saumu halafu kaanga kiasi.
Sasa ongezea ule mchanganyiko wa mboga ulizozichemsha na kisha ukazichuja. Kaanga kwa muda wa dakika moja.
Ongeza soy sauce pia na ukaange kwa muda wa angalau sekunde 15. Sasa ni zamu ya kuongezea ule wali wako uliopo tayari.
Hapa unaongezea korosho pia kama unatumia nyama ongeza pamoja na nyama endelea kuchanganya ichanganyike vizuri.
Unaweza mwagia juu ya wali wako majani mabichi ya kitunguu na majani ya giligilani ili kuongeza ladha na muonekano wa rangi tofauti.
Pakua na ufurahie.