MAPISHI: Makaroni na nyama
Na MARGARET MAINA
MUDA wa kuandaa: Dakika 25
Muda wa kupika: dakika 15
Walaji: 2
Vinanyohitajika
- Makaroni nusu pakiti (pima kulingana na mahitaji yako)
- Nyanya 4
- Nyanya ya kopo (tomato paste) vijiko 3
- Vitunguu maji 2
- Kitunguu saumu 1
- Pilipili mboga 1
- Soy sauce kwa kijiko kidogo
- Chumvi kijiko 1 kidogo
- Giligilani kijiko 1 kikubwa
- Gharam masala ¼ kijiko kidogo
- Binzari kijiko 1 kidogo
- Tangawizi ½ kijiko kidogo
- Nazi 1 iliyokomaa
- Njegere glasi 1
- Biringani 1, kate vipande virefu na vyembamba
- Italian seasoning kijiko 1 kidogo
- Pilipili ndefu 2; kata vipande vidogovidogo
- Cayenne pepper yaani udaha kijiko 1 kidogo
Maelekezo
- Andaa viungo – menya nyanya, vitunguu maji viwili, pilipili mboga na kitunguu saumu. Kata vipande vidogo. Kamua tui la nazi.
- Andaa njegere, zichemshe ila zisiive sana. Epua.
- Kwenye sufuria, weka maji na chumvi, acha yachemke.
- Weka makaroni, pika kwa dakika 10 kisha epua. (fuata muda elekezi kwenye paketi ya makaroni)
- Chuja maji, hifadhi.
- Ni vizuri ukipika makaroni dakika moja au mbili chini ya muda elekezi kwenye paketi, hii itafanya makaroni yaive vizuri yakichanganywa na sauce na wakati wa kumalizia kupika.
- Weka mafuta ya kupikia kwenye sufuria, bandika jikoni.
- Acha mafuta yapate moto vizuri kisha weka kitunguu maji. Hakikisha moto ni mkali ili mboga ziive vizuri bila kuchuja maji.
- Pika kwa dakika mbili huku unakoroga.
- Weka kitunguu saumu, bizari, tangawizi, pilipili ndefu, giligilani ya unga, italian season na gharam masala.
- Koroga vizuri kisha weka nyanya. Koroga taratibu kisha acha ziive hadi zitengane na mafuta. Weka nyanya ya kopo (tomato paste) na biringani na ukoroge pamoja.
- Weka njegere, koroga pamoja. Weka soy sauce pamoja na chumvi kiasi.
- Weka makaroni kwenye sufuria. Changanya na sauce ya nyanya na njegere. Weka pilipili mboga, koroga na acha ziive kiasi, ili harufu iwe tamu na nzuri. Weka tui la nazi.
- Geuza mara kwa mara kisha acha chakula kichemke kidogo. Nyunyizia cayenne pepper na pilipili manga ichanganye na chakula kisha epua.
Chakula kikishakuwa tayari, pakua na ufurahie.