MAPISHI NA UOKAJI: Jinsi ya kuoka keki iliyotiwa juisi ya limau
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 15
Muda wa kupika: Dakika 55
Walaji: 6
Vinavyohitajika
- siagi nusu kikombe
- sukari kiasi cha kikombe kimoja
- mayai matatu
- vijiko viwili vya ngozi ya limau
- kijiko kimoja cha juisi ya limau
- vanilla kiasi cha vijiko viwili
- nusu kilo ya unga wa ngano
- baking powder robo kijiko
- baking soda robo kijiko
- chumvi kiasi cha robo kijiko
- kikombe nusu cha sour cream
- icing sugar nusu kikombe
Maelekezo
Washa ovena nyuzijoto 165 ipate moto wakati unachanganya keki.
Paka siagi chombo cha kuokea keki, weka pembeni. Kwangua maganda ya limau na kamua juisi yake.
Kwenye bakuli la wastani, chekecha unga wa ngano, baking soda, chumvi na baking powder kisha hifadhi kando.
Kwenye bakuli kubwa, changanya sukari na siagi mpaka ilainike vizuri.
Ongeza mayai; moja baada ya jingine huku unachanganya. Koroga vizuri kisha weka maganda ya limau, maji ya limau pamoja na vanilla. Changanya vizuri.
Ongeza mchanganyiko wa unga wa ngano kidogo kidogo huku ukichanganya na sour cream. Koroga hadi uchanganyike vizuri.
Mimina mchanganyiko wako kwenye chombo cha kuokea ulichopaka mafuta awali.
Oka keki kwa dakika 55 au mpaka iive vizuri. Ikiiva, acha ipoe kwa robo saa kabla ya kuiweka kwenye sahani.
Wakati keki inapoa, changanya icing sugar na juisi ya limau mpaka ichanganyike vizuri.
Nyunyizia mchanganyiko wa icing sugar juu ya keki.
Acha ipoe kabisa. Katakata na ufurahie.