MAPISHI NA UOKAJI: Keki iliyotiwa matunda
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 30
Muda wa kuoka: Dakika 40
Walaji: 4
Vinavyohitajika
- gramu 250 za zabibu kavu
- maziwa ya maji
- gramu 250 za siagi
- chumvi kiasi cha ½ kijiko
- gramu 240 za sukari
- gramu 250 za korosho au karanga (chochote ulicho nacho kati ya hivi viwili)
- gramu 500 za unga wa ngano
- 1 kijiko kidogo cha baking soda (Baking powder)
- mayai 2
Maelekezo
Washa ovena yako katika joto la nyuzi 165 katika kipimo cha sentigredi kisha kipake chombo chako siagi. Chombo hapa ni kile utakachotumia kuokea keki yako.
Chukua bakuli, changanya unga wa ngano, zabibu na baking soda kisha weka kando.
Chukua bakuli jingine weka siagi na sukari ndani kisha pigapiga mpaka vichanganyike vizuri na kuwa laini kabisa kisha vunjia mayai ndani halafu piga paka mchanganyiko wako uwe laini kabisa.
Sasa chukua mchanganyiko wa unga, mimina kwenye mchanganyiko wa mayai na uchanganye taratibu mpaka upate mchanganyiko mzito wa wastani. Iwapo ni mzito sana, ongeza maziwa na kama utakua mwepesi sana, ongeza unga.
Kwa kuongeza ladha, unaweza kuongezea nusu ya kijiko kidogo cha nutmeg, mdalasini wa unga kiasi cha kijiko kidogo cha chai, na kijiko kidogo cha vanilla ya maji.
Kisha mimina mchanganyiko wako wa keki kwenye chombo utakachotumia kuokea na oka kwa muda wa dakika 45 hivi.
Muda wa dakika 40 ukishatimia, ni muhimu uchukue kichokonoo kisha uanze kudunga keki yako katikati halafu utoe kuangalia. Ukiona kichokonoo kimekuwa kikavu basi keki yako imeiva na iwapo kitakuwa na maji maji keki yako bado haijaiva hivyo iache katika ovena kwa muda mchache kabla ya kuangalia tena.
Toa keki yako, iache ipoe tayari kwa kuliwa.
Pakua na ufurahie.