MAPISHI: Nyama iliyosagwa
Na MARY WANGARI
KATIKA jiko letu hii leo tutaandaa kitoweo cha nyama iliyosagwa au ukipenda kima.
Viungo:
- 1 kilo nyama iliyosagwa
- ¼ lita mafuta
- 1 kijiko kidogo chumvi ya kuongeza ladha
- 2 vitunguu maji kikubwa
- 2 iliki
- 1 Tangawizi
- 4 nyanya kubwa
- 1 pilipili mboga
- 1 ndimu
- 1 kijiko bizari
- 1 kijiko cha karafuu iliyosagwa
- 2 viazi vikubwa
- 1 kikombe cha maharage ya kijani kibichi
- 2 karoti kubwa
- Mahindi yenye maziwa maziwa (ukipenda)
Utaratibu
Menya vitunguu na uvikate kate vipande vyembamba sana.
Chambua na uikwangue karoti iwe kama uji.
Katakata pilipili mboga katika vipande vyembamba.
Menya nyanya na uzikate katika vipande vya wastani.
Osha na uikwangue tangawizi.
Pondaponda na kutwanga vitunguu saumu.
Bandika sufuria ya kupikia jikoni.
Weka nyama na anza kukoroga ili kuzuia isigandie kwenye sufuria na kuungua.
Weka kitunguu maji huku ukiendelea kukoroga kwa muda wa dakika 10.
Weka kitunguu saumu na tangawizi. Endela kukoroga kwa muda wa dakika tano zaidi.
Weka mafuta kidogo sana ili kufanya viungo viize.
Weka pilipili mboga, karoti na kamulia ndimu. Ongeza chumvi kidogo. Endelea kukoroga.
Weka nyanya, koroga na funika sufuria na mfuniko kwa muda kama dakika 10.
Kisha ongeza viazi, maharage na mimina maji kiasi kwenye rojo. Makinika usiongeze maji kupita kiasi wala usipunguze mno na kuufanya mchuzi uwe mzito na kukauka.
Funika na uruhusu mchuzi wako kutokota hadi viazi vilainike.
Mimina tomato sauce na uchanganye vyema.
Sasa kitoweo chako kiko tayari, epua na ufurahie!
Unaweza kuambatisha na chapati, wali au hata kula kitoweo chako kavukavu kulingana na starehe yako.