MAPISHI: Viazi vya kuponda na nyama ya kuku
MUDA wa kuandaa: Dakika 5
Muda wa kupika: Dakika 20
Walaji: 3
Vinavyohitajika kwa mapishi ya viazi
- Kilo 1 ya viazi
- Lita 1 ya maji
- Maziwa kikombe nusu
- Vijiko 3 vya siagi
- Chumvi
Maelekezo
Menya, osha na kukatakata viazi vipande vikubwa vikubwa.
Weka viazi kwenye sufuria, ongeza maji ya kutosha.
Chemsha mpaka maji yachemke, kisha ongeza chumvi. Chemsha mpaka viazi viive vizuri.
Viazi vikishaiva vizuri, epua kisha chuja maji.
Anza kuponda viazi na uhakikishe hakuna mabonge mabonge.
Ongeza maziwa na siagi mpaka upate uzito na ladha utakayopenda.
Vinavyohitajika kwa kuku
- Minofu ya kuku nusu kilo
- Pilipili mboga 3 (nyekundu, kijani na njano). Wengi wana mazoea ya kuita pilipili mboga eti ni pilipili hoho. Ita jinsi utakavyo wewe.
- Kitunguu maji
- Mafuta ya kupikia
- Kijiko 1 cha chicken seasoning
- Kijiko 1 cha kitunguu saumu na tangawizi
- Chumvi na pilipili manga
Melekezo
Andaa viungo kisha katakata kuku, kitunguu na pilipili mboga vipande virefu virefu.
Kwenye kikaango katika moto wa wastani, chemsha mafuta kisha ongeza nyama ya kuku, chicken seasoning, kitunguu saumu na tangawizi.
Kaanga mpaka nyama ikaribie kuiva kisha ongeza kitunguu maji, pilipili mboga, chumvi na pilipili manga.
Endelea kukaanga kwa dakika chache mpaka nyama ya kuku iive vizuri.
Pakua pamoja na viazi vya kuponda na ufurahie.