MAPITIO YA TUNGO: Ndoto ya Amerika; Novela ya kitashtiti inayotoa mwanga kuhusu ulezi wa watoto
Mwandishi: Ken Walibora
Mchapishaji: Longhorn Publishers
Mhakiki: Wanderi Kamau
Kitabu: Novela
Jina la Utungo: Ndoto ya Amerika
Kurasa: 48
NDOTO ya kila mtoto ni kufikia upeo wa malengo yake maishani.
Katika udogo wao, wengi huwa na matamanio makubwa ya kuwa watu wakubwa na wenye ushawishi katika jamii.
Msukumo wa kufikia wayatakayo huwafanya kujitolea kwa hali na mali, hasa kwenye masomo yao.
Ndivyo hali anayojipata mvulana Isaya Yano, mhusika mkuu kwenye novela ‘Ndoto ya Amerika’ yake Prof Ken Walibora.
Isaya ni mvulana kutoka kijiji cha Sangura katika wilaya ya Trans-Nzoia.
Ana ndoto kama za mtoto wa kawaida akuliaye katika mazingira ya kijijini. Babake anafariki akiwa na umri mchanga, hali inayomfanya mamaye kumpa malezi ya wazazi wote wawili.
Miongoni mwa marafiki wa karibu sana Isaya ni mvulana mwenziye, Madoa, waliyesoma katika shule moja.
Madoa amepewa msimbo wa ‘Ndiyo Alaa’ kwani alizoea kuwa na kiitikio hicho katika maongezi yake ya kawaida.
Wawili hao wanapoungana, wanahadithiana kadhia nyingi, mojawapo ikiwa ni matamanio ya kufika nchini Amerika.
Madoa si mwerevu shuleni, licha ya kuwa na ndoto kubwa. Hilo linamfanya kutoyapenda masomo.
Adhabu kali wanazopata kutoka kwa mama zao zinawafanya kutoroka nyumbani mwao. Madoa anaiba Sh2,300 kutoka kwa nyumba ya Mzee Zakayo Wekesa. Wanatumia fedha hizo kusafiria jijini Nairobi kwa imani ya kumpata Rock Mwamba, rafiki yao ambaye angewasaidia “kusafiri Amerika.”
Kwao, Amerika ni ndoto tu, ya nchi yenye magari mazuri, majumba makubwa na mambo ya kifahari.
Wanapofika Nairobi, wanaelekea katika mtaa wa Kayole, wanakokutana na rafikiye Madoa, Mamba.
Baada ya kukaa kwa siku kadha, Isa anagudua kwamba Mamba alikuwa jambazi sugu aliyekuwa akipata ajira kupitia uhalifu.
Madoa alikuwa mshirika wake wa karibu kwani alikuwa amepewa lakabu la ‘Ninja.’
Katika harakati za ‘kufanya kazi’ ambapo ni kufanya visa vya uhalifu, akina Madoa wanakumbwa na mkosi, ambapo wanakamatwa na polisi. Walikuwa wamejihami kwa bunduki!
Watatu hao wanafikishwa mahakamani, ambapo Mamba anaripotiwa kupigwa risasi na mlinzi wa gereza anapojaribu kutoroka, huku Madoa akipewa kifungo cha miaka mitatu kwa kushirikiana na jambazi sugu.
Isaya anaponea, kwani anaunganishwa tena na mamake, japo kwa majuto makuu.
Kimsigi, novela hii inatoa mwanga kwa wazazi kuwa na mashauriano ya kina na wanao, ili kufahamu na kuwaongoza kufikia ndoto zao maishani.
Amefanikisha kazi yake kupitia methali, nahau na lugha ya wastani, inayoeleweka kwa urahisi.
Maudhui makuu yanayojitokeza ni umuhimu mashauriano na malezi mema.