• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
MAPITIO YA TUNGO: Nimeshindwa Tena; Novela inayotathmini thamani kuu ya mja

MAPITIO YA TUNGO: Nimeshindwa Tena; Novela inayotathmini thamani kuu ya mja

Mwandishi: Ken Walibora

Mchapishaji: Phoenix Publishers

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Novela

Jina la Utungo: Nimeshindwa Tena

Kurasa: 64

ANAPOISHI duniani, lengo kuu la mwanadamu ni kuibuka mshindi kwa kila alifanyalo.

Si nia yake kushindwa hata kidogo.

Lakini kuna ufiche kubwa katika maisha ya mwanadamu kuliko kuishi kushinda tu, kama anavyodhihirisha Prof Ken Walibora katika novela ‘Nimeshindwa Tena.’

Novela hii inajikita katika maisha ya kijana Mshindi Mmoja, anayelelewa katika mazingira ya kumtaka kuwa mshindi daima kwa kila alifanyalo.

Mshindi Mmoja ni mzaliwa wa familia ya kawaida jijini Dar es Salaam nchini Tanzania. Ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Shaaban Robert. Ana rafiki wawili; Kayole na Lunyamila, ambao wanashindana katika shughuli mbalimbali wanazofanya kama wavulana.

Katika maisha yake, anakumbatia kauli ya kuibuka mshindi kwa kila jambo. Hata hivyo, inamtatiza pakubwa kila wakati anaposhindwa na wenzake, kwani anatia bidii sana akiamini kuwa siku moja atavuna tija ya juhudi zake.

Mshindi Mmoja anatia bidii masomoni na michezoni, ila wakati mwingine mambo yalimwendea mrama. Kwa mfano, gazeti la ‘Majigambo’ linatangaza shindano kubwa la kuandika insha, ambapo wale wangeibuka washindi wangepata nafasi ya kutembezwa miji mikuu ya nchi za Afrika Mashariki.

Kwa kujiamini na kutia bidii za mchwa, Mshindi Mmoja anajinyima na kuweka juhudi kubwa kuandika insha bora ili kuhakikisha ameibuka mshindi.

Baadhi ya hatua anazochukua ni kuwaarifu wazazi wake, ambao wanafanya juhudi kumnunulia vifaa muhimu kama Kamusi na madaftari kadhaa. Anajitenga na wenzake, yaani Kayole na Lunyamila, ili kujipa muda wa kutosha kuipiga msasa insha anayoiandika

Baada ya muda wa kuandika insha hizo kuisha, anaipeleka kwa mwalimu wake wa Kiswahili.

Insha hizo zinakusanywa na kutumwa makao makuu ya gazeti la ‘Majigambo.’

Matokeo hayo yangetolewa baada ya muda maalumu kuisha.

Mshindi Mmoja aliamini kuwa ndiye angeibuka mwanafunzi bora. Shauku ilimvaa.

Baada ya matokeo kutangazwa, maskini Mshindi Mmoja hakuwa miongoni mwa washindi. Wenzake, Kayole na Lunyamila walimpiku. Nusura azimie.

Mkasa unatokea pale Kayole anazama majini katika Ufuo wa Bezi wanaposherehekea matokeo yale. Hata hivyo, Mshindi Mmoja anafanikiwa kumwokoa.

Kitendo hicho kinampa sifa kubwa, kiasi kwamba anakumbukwa na kusifiwa pakubwa kotekote!

Funzo kuu ni kuwa, kuna vitendo vya kibinadamu vinavyozidi kuwa bora tu katika mashindano. Utu una thamani na umuhimu mkubwa. Ni hadithi yenye mafunzo inayoeleweka kwa urahisi.

 

[email protected]

You can share this post!

Polisi Mungiki wanavyotesa wananchi

Serikali ya kaunti yafuta bili za waliovamiwa na genge...

adminleo