• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
MAPITIO YA TUNGO: Novela aali inayosimika msingi madhubuti wa kiusomi kwa watoto

MAPITIO YA TUNGO: Novela aali inayosimika msingi madhubuti wa kiusomi kwa watoto

Jina la Utungo: Mama Panya na Mtoto wake Chepsoo

Mwandishi: Dorothy Jebet

Mchapishaji: Nsema Publishers

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Hadithi ya Watoto

Kurasa: 38

KATIKA kuweka msingi wa kiusomi kwa mtoto, hatua ya kwanza huwa ni kumsaidia kuimarisha uwezo wake wa kusoma.

Bila shaka, mwanafunzi mchanga hawezi kuimarisha uwezo wake pasi na kupiga msasa unaohimiliwa katika vitabu vya ngano za watoto.

Ni kwa kauli hiyo ambapo kitabu ‘Mama Panya na Mtoto wake Chepsoo’ ni mojawapo ya mihimili mikuu ambayo huenda ikachangia sana kukuza uwezo wa kiusomi wa watoto.

Kikiwa kimeandikwa na Bi Dorothy Jebet, ambaye ni mwanahabari aliyehudumu kwa muda mrefu, hadithi hii inarejelea maisha ya Mama Panya na Mtoto Chepsoo; ukiwa ni msuko unaobuni mafunzo chekwachekwa kwa msomaji.

Hadithi inaanza wakati Mama Panya anatoka sokoni na kuvutiwa na Mama Chura, ambaye anamwimbia mtoto wake bembelezi ili alale mbali na kumweleza vile anampenda.

Aidha, Mama Chura anamhakikishia mwanawe kwamba anampenda kwa dhati, na kuwa anaweza kufanya lolote ili kudhihirisha mapenzi yake kwake.

Kwa hili, mwandishi anatilia mkazo umuhimu wa ukaribu unaopasa kuwapo kati ya wazazi na wanao.

Anapotoka sokoni, Mama Panya anamnunulia mwanawe maziwa na ndizi. Ingawa hadithi hii inajikita katika utoaji mafunzo ya maadili mema kwa watoto, pia inashadidia umuhimu wa kujaliana katika jamii.

Hili linajitokeza wakati Mama Panya na Mama Chura wanapomwona Baba Zimwi, wakiwa wanaelekea nyumbani kwao. Wanashindwa la kufanya, kwani walihofu kwamba huenda angewala.

Kwa haraka, wanamwomba usaidizi Mama Kunguru, anayekubali kuwaficha katika kiota chake. Kwa kuwatumia wanyama, mwandishi pia anafanikiwa kutoa mafunzo ya umuhimu wa usafi, kupitia kwa Mama Sungura.

Jamii ya Mama Sungura inasawiriwa kuwa na umoja mkubwa, kwani watoto wake watano wanagawana majukumu ifaavyo. Kwa mfano, wawili wanaonekana wakiosha mikono yao baada ya kwenda msalani, huku mama yao akiwapikia.

Familia hii pia huomba kabla ya kuenda kulala.

Kwa hili, mwandishi anaonyesha umuhimuwa watoto kufunzwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia dini.

Kitabu hiki ni tafsiri ya Kiswahili kutoka kwa Kikeiyo. Upekee wa familia hii ni kuwa inaomba kwa pamoja kwa unyenyekevu mkubwa.

Kwa jumla, ingawa ni hadithi ambayo inawalenga watoto wa madarasa ya chini, ina umuhimu mkubwa katika kutoa mafunzo ya maadili mema kwa kutumia lugha nyepesi na kwa njia rahisi sana.

Maandishi ya kitabu hiki ni makubwa, kiasi cha kumwezesha mtoto ambaye ana ufahamu wa kusoma kuhitaji ama hata kutohitaji usaidizi wa mwalimu wake.

Ni thawabu kuu kwa kila mtoto na jamii nzima.

 

[email protected]

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wajadili ufaafu...

Walivyozimwa kwa minofu

adminleo