MAPITIO YA TUNGO: Novela 'Upande Mwingine' inausuta usasa uliojaa maovu
Mwandishi: Ken Walibora
Mchapishaji: Oxford University Press
Mhakiki: Wanderi Kamau
Kitabu: Novela
Jina la Utungo: Upande Mwingine
Kurasa: 62
MABADILIKO ya kimaumbile ni mambo ambayo jamii na mwanadamu hawezi kuyaepuka hata kidogo.
Kimsingi, mabadiliko hayo ndiyo yamekuwa mhimili wa usasa ambao mwanadamu ameshuhudia kwa muda mrefu; uzamani ukififia tangu siku zinavyosonga.
Huu ndio usawiri anaochora Profesa Ken Walibora katika novela yake ‘Upande Mwingine’.
Ni hadithi inayomrejelea Mzee Kimako kutoka kijiji cha Rangile. Hadithi inapoanza, anarejea kijijini kwake baada ya kukaa uhamishoni kwa miaka hamsini.
Anarejea baada ya vita kuzuka, vita ambavyo vilihatarisha maisha yake. Anapoteza babaye na ndugu zake wanne; kiini cha yeye kutorokea janibu za mbali ili kunusuru maisha yake.
Hata hivyo, anashangazwa na kiwango kikubwa cha usasa ambacho kimekiandama kijiji chake, kiasi cha kutotambulika kwa urahisi. Kuna majengo makubwa, magari mengi, barabara za kisasa kati ya maendeleo mengine yanayodhihirisha usasa.
Kinaya cha usasa huu hata hivyo ni mkinzano mkubwa wa mwenendo wa kimaisha ambao ulikuwepo awali na sasa. Anatupa ulinganisho wa sasa na zamani (akiwa kijana) ambapo kulikuwa na kiwango kikubwa cha watu kujaliana. Utu na undugu ulikuwepo. Usasa unachorwa kuhimiliwa na maovu.
Watu walishirikiana kwa lolote, licha ya kutokuwa na utajiri mkubwa.
Waliishi katika nyumba za msonge, ila walijaliana kwa kila hali; hasa kwa maslahi muhimu kama chakula.
Mazingira yalikuwa safi. Mito ilikuwa yenye maji safi, ambayo yalitegemewa sana na watu wote; wazee kwa vijana.
Katika hadithi hii yenye matumizi makubwa ya lugha ya ishara, mwandishi anatumia jazanda kubwa, kuonyesha vile ujio wa usasa ulivyoadimisha dhana ya utu katika nyoyo na nafsi za wanadamu.
Mfano mkuu unadhihirika mwanzoni mwa hadithi, wakati vijana (ambao ni utingo) wanamzungumzia kwa lugha isiyo taadhima.
Ni katika mazungumzo hayo ambapo kiwango cha ufuska katika jamii ya kisasa ya Warangi inadhihirika. Anafahamu kwamba kuna wasichana wadogo waliokuwa wakiwaandama wazee matajiri ili kushiriki ngono nao!
Mbali na hayo, mwandishi anatupa taswira ya mtaasisiko wa ubinafsi katika maisha yakisasa ya Warangi, ikilinganishwa na zamani ambapo ujima ndio ulikuwa msingi wake mkuu.
Aidha, anarejelea hali ya ukame anayokuta katika kijiji hicho kama hali sawa na uadimifu wa maadili katika jamii za kisasa.
Jamii imetaasisisha na kuabudu uovu kuliko maadili. Ujumbe mkuu ni kuwa maadili ndiyo mhimili mkuu wa jamii bora.