• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
MAPITIO YA TUNGO: ‘Sungura Hakimu’ ni kazi inayochochea usomaji kupitia fantasia

MAPITIO YA TUNGO: ‘Sungura Hakimu’ ni kazi inayochochea usomaji kupitia fantasia

 

KITABU hiki kina hadithi mbili ambazo zinawalenga watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 12.

Matumizi ya fantasia katika hadithi zote mbili yanalenga kuuchochea usomaji wa watoto hao.

Aidha, mumo humo kwenye fantasia mnajitokeza maudhui mazito yanayolenga kuwaadilisha watoto.

Mwandishi anawafunza watoto hao kuwa hisia za ugoigoi na ukaidi hazipaswi kudekezwa katika jamii yoyote ambayo inastahi maendeleo.

Hadithi ya kwanza na ambayo imepewa kipau mbele katika mkusanyiko huu inamzunguka sungura.

Mwanzoni, sungura anadhihirishwa kuwa mnyama mvivu ambaye hapendi kufanya kazi.

Majirani wanapong’amua kwamba sungura hapendi kufanya kazi wanamwambaa na hata baadhi yao kuvificha vyakula mifunguni mwa vitanda wakisubiri sungura aondoke kabla ya kuandaa meza.

Jambo hili linamtia sungura mfadhaiko.

Hata hivyo, anagundua kwamba amejaliwa kipawa cha kipekee.

Yeye ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa.

Anatumia maarifa yake kuwaleta wanyama pamoja. Anawatolea kitabu ambacho anadai kuachiwa na nyanya yake kabla ya kuaga dunia.

Hiki ni “Kitabu cha Sheria’’ ambacho sungura anaeleza kuwa kingetoa mwongozo jinsi ya kutumia sheria ili kumhakikishia kila mmoja utawala wa haki.

Anawaeleza wanyama kuwa ili sheria kuzingatiwa, wanyama walihitaji hakimu. Uchaguzi unafanywa na sungura ambaye aliliangua wazo lile anaishia kuwa hakimu wa wanyama mwenye hadhi kuu.

Hadithi ya pili imekumbatia uhalisia na fantasia.

Hassan, kijana mmoja mtundu, hapendi kufanya kazi. Hulka ya mama yake ya kumwamsha kila asubuhi ili wakalime haimpendezi.

Siku moja anatoroka shambani na kwenda kujistarehesha msituni.

Humu anakutana na jitu ambalo linaitwa Shivero ambalo nusura limwangamize lau si kwa pete ya ajabu anayopewa na kasuku mmoja anayekutana naye katika nyumba ya jitu.

Mvuto

Mambo kadha yanazipa simulizi hizi mvuto.

Kwanza, mwandishi amekumbatia mbinu ya fantasia katika usimulizi wake.

Hii ni mbinu ambayo inaelekea kufifia katika masimulizi ya zama hizi ambayo hulenga uhalisia kama njia moja ya kuwaandaa wanafunzi kubuni insha zenye uhalisia.

Hata hivyo, Bwana Mtuku amedhihirisha kuwa ili uhalisia kufikiwa sharti watoto wachochewe kusoma kwanza.

Njia mojawapo ya kuuchochea usomaji ni kuwachorea ulimwengu wao ambao ni tofauti na ulimwengu wa watu wazima.

Pili, mwandishi ametumia lugha nyepesi iliyotomelewa vito vya misemo na methali nyepesi.

Fauka ya hayo, masimulizi yanaambatana na picha za rangi zilizosanifiwa kwa utaalamu mkubwa.

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Athari ya lugha za kigeni kwa Kiswahili

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya...

adminleo