MAPITIO YA TUNGO: Utengano; riwaya inayoakisi uhalisia wa maisha tunayoishi
Mwandishi: Said Ahmed Mohamed
Mchapishaji: Longhorn Publishers
Mhakiki: Wanderi Kamau
Kitabu: Riwaya
Jina la Utungo: Utengano
Kurasa: 198
‘UTENGANO’ ni riwaya inayoangazia masuala muhimu ya kijamii kama talaka, nafasi ya wanawake katika jamii, taasubi za kiume, siasa, na msamaha.
Upekee wake mkubwa unatokana na jinsi mwandishi Said A Mohamed anavyotumia lugha kwa urahisi, lakini kwa jazanda kubwa.
Kazija, mhusika mkuu riwayani ni mpenziwe Bwana Maksuudi, mwanasiasa na mfanyabiashara mwenye ushawishi.
Anapanga njama ya kuwakosanisha Bwana Maksuudi na mwanawe, Mussa.
Anafaulu kwenye mpango huo, pale anapowaita wawili hao kwenye nyumba yake.
Maksuudi na Musa wanapigana vikali, hali inayowafanya kutengana.
Hata hivyo, Kazija anafanya hivyo ili kulipiza kisasi kwa niaba ya mwanawe rafikiye, Biti Sururu. Biti Sururu ni mwanawe Bi Farashuu.
Maksuudi alikuwa amemwoa Biti Sururu, ambapo alimdhulumu na kumtaliki. Kutokana na masaibu hayo, Biti Farashuu anageuka kuwa maskini, anajiingiza katika ulevi na kufariki baadaye.
Mwandishi anawatumia wahusika Shoka na James kuonyesha jinsi watu maskini katika jamii wanavyofanya kazi kwa bidii kutafuta riziki. Hata hivyo, badala ya kutumia mapato yao kujiendeleza kimaisha, wanajiingiza katika ulevi na kuzitelekeza familia zao.
Nao Bwana Maksuudi na Bwana Smith wanasawiriwa kuwa watu walaghai katika jamii wanaoipora serikali. Riwaya hii inaangazia kwa undani, nafasi ya mwanamke katika jamii. Mfano huu unadhihirika kwenye maisha anayopitia Bi Tamima, mkewe Bwana Maksuudi.
Ni mwanamke aliyedhulumiwa sana. Amezuiwa kuifahamu dunia na kufanywa mtumwa bila yeye kutoa sauti yoyote.
Mumewe anaenda nje ya ndoa bila kumheshimu hata kidogo.
Maksuudi anamtaliki baada ya kumpiga siku moja baada ya kujifungua, sababu kuu ikiwa hatua yake kumkubalia mkunga kuingia nyumbani mwake. Suala jingine linalojitokeza riwayani ni mtindo wa baadhi ya wanawake kuwaharibia maisha wenzao kimakusudi, bila kujali athari za vitendo vyao. Kwa mfano, Mama Jeni anauza pombe ambapo pia anamiliki danguro.
Ana wanawake ambao wanashiriki biashara ya ngono, wanaowahadaa wanaume na wasichana wadogo kushiriki kwenye ukahaba.
Maimuna, ambaye ndiye mhusika mkuu riwayani, anapevuka sana kutoka hatua moja ya maisha hadi nyingine. Alikuwa msichana aliyefungiwa kwao, lakini anatoroka na kuishia kufanya kazi kazi katika danguro la Mama Jeni.
Baada ya mkondo wa maisha yake kuharibika, anakubali kwamba hahitaji kitu chochote kizuri maishani. Anaelekea katika kijiji pweke cha Futoni, kilicho karibu na ziwa. Licha maisha yake mabaya, anakutana na mwanamume aitwaye Kabi, ambaye anamwoa licha ya matatizo yaliyokuwepo awali. Ndoa yao inajenga daraja la msamaha kati ya Bi Farashuu, Mussa na Maksuudi.
Ni riwaya inayoonyesha kuwa licha ya vitendo vyetu kama binadamu, kila mmoja anahitaji msamaha na Mungu ndiye mwenye uwezo wa kumhukumu mwanadamu.