Makala

MAPOZI: Eric Musyoka

June 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

YEYE ni mmojawapo wa maprodusa wanaoheshimika nchini kutokana na kazi yake safi, huku akijivunia kufanyia kazi baadhi ya nyimbo maarufu nchini.

Jina lake ni Eric Musyoka, produsa wa nyimbo na mmiliki wa lebo ya Decimal Records, ambayo imekuwa kitambulisho cha baadhi ya nyimbo safi nchini na mbali.

Katika kipindi cha takriban miongo miwili, Musyoka kama anavyofahamika miongoni mwa mashabiki, anajivunia kufanyia kazi baadhi ya wasanii maarufu hapa Kenya na eneo la Afrika Mashariki.

Amerekodia albamu wasanii wa haiba ya juu kama vile Daddy Owen (Son of Man), Juliani (Mtaa Mentality), Monique (Color Black) miongoni mwa wengine.

Upande wa nyimbo, anajivunia kushughulikia kazi za baadhi ya wasanii maarufu miongoni mwao Prezzo, TID, SEMA, Mr Lenny, Bamzigi, Nameless, AY, Wyre, Peter Miles, Nikki na Nonini huku baadhi ya nyimbo zake maarufu zikiwa ni pamoja na Leta Wimbo, Nataka Kudunda, Watasema Sana, Make a Choice, Muwala, Nipe Nikupe, Hii Ngoma na Furahi Day miongoni mwa zingine.

Pia amehusika katika kuchanganya nyimbo za baadhi ya wasanii marufu kama vile Elani (KooKoo, Jana Usiku, Hapo Zamani), Sauti Sol (Sura Yako, Nerea), Octopizzo (Nani, Black Star, Salute Me), Nonini (LATT, Mbele) Nameless (African Beauty) kati ya wengine.

Aidha, ameshirikiana na baadhi ya majina makuu eneo la Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Prof. Jay na Kleptomaniaks kurekodi kibao Njoo, wimbo ulipopata umaarufu sio tu hapa nchini Kenya bali pia Tanzania.

Mwaka wa 2010, alishirikiana na kikundi Just a Band, kwenye kibao Ha-He alichoandika na kurekodi. Wimbo huu uling’aa eneo la Afrika Mashariki na hata kutambuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa na hivyo kuthibitisha uwepo wa bendi hii katika fani ya muziki.

Kama mtunzi wa nyimbo za filamu, kazi yake imesikika kwenye filamu Nairobi Half-Life na VeVe.

Pia ametunga muziki wa matangazo ya kibiashara, vilevile vitambulisho vya baadhi ya mashirika makubwa nchini.

Mwaka wa 2006 alitangazwa mshindi wa tuzo ya produsa bora wa mwaka kwenye tuzo za Kisima Awards.

Mojawapo ya sifa ambazo zimemtenganisha na wengine kwenye fani hii ni uwezo wake wa kukaa mbali na mwangaza mbaya wa vyombo vya habari, na badala yake kuacha kazi yake imwangazie.

Aidha, anafahamika kwa subira yake katika kazi anazofanya, suala linalomfanya kumakinika na kila mradi anaohusika nao.

Alijitosa katika shughuli za kurekodi muziki mwaka wa 1997 katika studio ya Sync Studio chini ya ukufunzi wa Muhammud Omar, Ambrose Mandugu na Ted Josiah.

Wakati huo alikuwa mmojawapo wa wanarepa kwenye kikundi cha Nannoma, kilichojumuisha marafiki zake kutoka shule ya upili.

Kikundi hiki kilitumbuiza pamoja hadi 2001, alipoamua kufuata ndoto yake ya kuwa produsa huku akifanya kazi na Ukoo Flani na Mau Mau.

Wasanii wa kwanza kuwarekodi walikuwa Juliani, Zakah na Kah. Wakati huo alirekodia kikundi Ukoo Flani na Mau Mau, vibao kama vile Dandora LOVE, DC na Sisi, Angalia Saa, Punchline Kibao na vingine vingi.

Baadaye aliajiriwa na lebo ya Homeboyz Entertainment kama produsa mkuu. Ili kujiimarisha kitaaluma, alienda ng’ambo kuzidisha masomo aliporejea alianzisha studio Decimal Media House.

Wakati huu alisajili kikundi cha P-Unit na kukirekodia ngoma kama vile Juu Tuu Sana, Kare, Hapa Kule, You Guy, Mobimba na Weka Weka kati ya vingine.

Yeye ni mfano wa kuigwa miongoni mwa maprodusa wengine nchini, sio tu kutokana na unyenyekevu wake bali pia umakini kila anaposhughulikia kazi zake.

Sasa kibarua kwake ni kuzidisha moto huu, vilevile kudumisha jina hili safi ambalo amejiundia kwa miaka.