Makala

MAPOZI: Gerald Langiri

May 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KENYA imetambulika katika ngazi za juu za uigizaji hasa kupitia mwigizaji Lupita Nyong’o aliyeiweka nchi hii kwenye ramani ya uigizaji alipojishindia tuzo ya Oscars.

Haiishii hapo tu kwani hapa nyumbani pia vipaji vya uigizaji ni vingi na Gerald Langiri, mwigizaji, produsa na mwelekezi wa filamu na vipindi ni mmoja wao.

Alitambulika kupitia kipindi cha ucheshi cha House of Lungula na hivyo kujiundia jina kama mmojawapo wa waigizaji wanaotambulika sana nchini.

Mbali na filamu hiyo ambapo aliigiza kama Harrison, pia alijiundia jina kupitia Fundimentals ambapo aliigiza kama Joseph.

Pia ameshiriki katika filamu zingine ikiwa ni pamoja na Inherited, Flowers and Bricks, Orphan, 24 hours to live, Accidental kidnapping, Gun theory miongoni mwa zingine.

Aidha, ameshiriki katika vipindi kama vile Santalal, Mali, Stay, Papa Shirandula, Pendo, Pray and Prey, In the forest na Shit Happens kati ya zingine.

Kama mwelekezi amechangia katika vipindi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Selina, Veve, Going Bongo, The Unprotected bali na kuwa mwelekezi wa waigizaji wa kipekee kutoka Kenya katika msimu wa pili wa shindano la BET Top Actor Africa.

Ni ustadi huu ambao umemfanya kutambuliwa katika tuzo mbalimbali. Mwaka wa 2014 alituzwa kama muigizaji bora msaidizi katika vipindi katika tuzo za Kalasha Film and Television Awards kutokana na kushiriki kwake kama Nico kwenye kipindi Stay.

Mwaka wa 2015 aliteuliwa kama mwigizaji bora wa vichekesho katika tuzo za Africa Magic Viewers Choice Awards (AMVCA).

Aidha, aliteuliwa kama muigizaji bora wa mwaka katika tuzo za Nigerian Entertainment Awards (NEA) na kuwa muigizaji wa kipekee kutoka Afrika Mashariki kushirikishwa kwenye orodha hiyo.

Langiri hajang’aa tu kama muigizaji kwani pia ni mwandishi wa masuala ya filamu. Weledi wake ulidhihirika mwaka wa 2014 alipotuzwa kama mwanahabari/ bloga bora wa filamu katika tuzo za African Film Development Awards 2014.

Mjumbe

Mwaka 2018 aliteuliwa kama mjumbe wa kampuni ya mavazi ya Vazzi Clothing line na kuungana na watu wengine maarufu kama vile DJ UV, Camp Mulla, Huddah, DJ kayTrixx, DJ Crème, DJ Hypnotic na Shaffie Weru ambao wamewahi kushirikiana na kampuni hiyo.

Safari yake kama mwigizaji ilianza akiwa angali mdogo ambapo akiwa katika shule ya chekechea, tayari alikuwa ameanza kung’aa katika fani hii huku akishiriki katika michezo ya uigizaji katika mikutano ya wazazi.

Ni kipaji alichokiendeleza hata alipojiunga na shule ya msingi na ya upili, kabla ya kujitosa rasmi katika uigizaji mwaka wa 2011 huku ari yake ya uigizaji ikichochewa na miamba wa uigizaji nchini kama vile Lizz Njagah, Ken Ambani na Raymond Ofula. Hii ilikuwa baada ya kusomea shahada yake katika chuo kikuu na hata kuajiriwa.

Hata hivyo, ufanisi huu usikufanye udhani kwamba hajawahi kukumbana na changamoto.

Kama mwigizaji mwingine yeyote hasa humu nchini, mambo hayajakuwa rahisi huku akikabiliwa na uhaba wa nafasi za uigizaji.

Hata hivyo changamoto hizi hazijazima mwanga wake.

Ni ustadi ambao umemkutanisha na waigizaji wengi maarufu nchini na kimataifa ikiwa ni pamoja na Wakenya waliobobea katika fani hii kama vile Blessing Lungaho, Vera Atsango, Lydia Gitachu, Faith Munini na Innocent Njuguna miongoni mwa wengine, vile vile kigogo kutoka Nigeria, Desmond Elliot.

Bila shaka amejiundia jina kiasi cha kutambulika hata nchini Nigeria, taifa linalotawala fani ya filamu barani. Lakini linalosalia ni kuona iwapo utambuzi huu unatosha kumuinua na kumfikisha katika upeo wa Lupita kwa kuigiza kwenye jukwaa la Hollywood.