MARAGUA: Eneo ambako polisi hushirikiana na genge kuuza bangi
Na MWANGI MUIRURI
MWEZI Mei kulizuka kisa cha kushtusha kiusalama katika mji wa Maragua ambao uko katika Kaunti ya Murang’a ambapo genge la wauza bangi likijafahamisha kama “Wazaliwa” lilimwandama mlanguzi mwingine aliyesemekana kuwa “mgeni kutoka kaunti ndogo ya Kangema.”
Ni hali ambayo aliyekuwa mbunge wa Maragua Peter Kamande alilazimika kufika eneo hilo na kushutumu vikali kisa hicho akiwataka wenyeji wawajibikie suala la kuwazima walanguzi wa mihadarati katika mji huo.
Genge hilo likiwa limejihami kwa mapanga na mijeledi liliingia katika mitaa ya mji huu likimsaka mlanguzi huyo aliyetambuliwa kama Macharia Mwangi.
Lilimpata katika mtaa wa Rurii na ambapo nusura limwangamize kwa kumkatakata.
Maafisa wa polisi ndio walifika kumnusuru na ambapo walimkamata Bw Mwangi na ambapo hadi sasa anawajibikia kesi yake kuhusu kunaswa akiwa na bhangi.
Ajabu ni kwamba, maafisa hao hawakuwanasa wavamizi hao ambao walikuwa wamejihami na ambao walizua taharuki na kuharibu amani ya umma.
Maafisa hao kutoka kituo cha Maragua walionekana kuegemea mrengo huo wa wauzaji bangi ambao ni wazawa wa eneo hilo na ambapo wengi wao ni wa kutoka familia inayojulikana kama ya Njoya.
Ni familia ambayo makazi yake rasmi ni kijiji cha Maisha Ma Thi na ambapo pia hufahamika na upikaji chang’aa.
“Leo hii, walanguzi hao ambao wanajifahamisha kama wazaliwa ndio wanauza bhangi yao katika mitaa ya Maragua na ambapo kwa kila mlanguzi, polisi hudai Sh500 kwa wiki. Kuna wauzaji bangi kama 20, hii ikiwa na maana pato la polisi kwa wiki ni Sh10, 000,” asema mdokezi wetu katika mji huu.
Wenyeji wanasema kuwa licha ya kutoa habari kwa maafisa wa kiusalama eneo hilo, “habari zetu hupuuzwa na mara zingine kufikishwa kwa walanguzi hao hali ambayo huweka maisha ya walio na pingamizi hatarini.”
Kuna kamanda wa Polisi ambaye amehamishiwa eneo la Bomett akifahamika kama Bi Naomi Ichami ambaye husifiwa sana kuwa enzi yake alikuwa amezima “upuzi huu wa magenge ya ulanguzi mtaani.”
“Bi Ichami alihusika moja kwa moja na uchungyuzi ambao uliishia bhang ya thamani ya Sh3 milioni kunaswa katika nyumba moja ya mlanguzi sugu na ambapo wafanyakazi wake watatu walitiwa mbaroni wakiwa katika harakati za kuipakia tayari kwa soko.
“Wote walifungwa vifungo gerezani kwa kuwa Bi Ichami alifuatilia kesi zao hadi zikazua vifungo,” asema aliyekuwa mshirikishi wa mpango wa Nyumba Kumi eneo hilo, Simon Kamau.
Bw Kamau anasema kuwa kituo cha polisi cha Maragua huwa na visa vya kustaajabisha.
Maafisa wachunguzwe
“Kwa wakati mmoja, Bi Ichami aliagiza maafisa wawili wa polisi katika kituo hicho wachunguzwe kwa madai kuwa walikuwa washirika wa walanguzi wa mihadarati katika Mji huu.
“Maafisa hao wawili walikuwa wameripotiwa kuonekana katika mkutano wa siri na walangzui watatu wa bhangi na kuwaelekeza wawe wakiendelea mbele na biashara yao pasipo hofu ya kukamatwa bora tu wawe wakipokeza maafisa hao hongo ya jumla ya Sh1, 500 kwa siku.”
Wenyeji wanateta kuwa kamanda wa polisi wa sasa katika kaunti hiyo, Josephat Kinyua amehudumu kwa muda mrefu akiwa kamanda wa askari wa utawala (AP) na hivyo basi kudhaniwa kama asiyefaa eneo hilo.
‘Mtu akikaa sana katika eneo moja la kikazi, kuna ule uzoeefu anapata katika jamii…wakora kwa wema wanaweza kuwa wamemsoma Bw Kinyua kiasi kwamba wanajua mbinu zake za kikazi. Hapa kunahitaji mgeni katika safu ya kiusalama,” asema Bw Kamau.
Hata hivyo, Bw Kinyua anasema kuwa “shida ni wakati unapata habari na ukiipokeza maafisa wanaowajibikia eneo fulani, wanaipuuza.”
Anasema kuwa amekuwa akipata habari hizo za bhangi katika mitaa ya Maragua “na huwa nawaagiza maafisa eneo hilo waishughulikie. Ni jukumu la wananchi kuzidi kutupasha habari kuhusu utenda kazi wa maafisa hawa ndio wale wazembe wanaadhibiwa.”