Margaret Kenyatta: Meya wa kwanza wa kike Kenya
Margaret Wambui Kenyatta, msichana wa kwanza kujiunga na shule ya Alliance High School iliyokuwa ya wavulana, alikuwa na umri wa mwaka mmoja tu alipomuona baba yake, Jomo Kenyatta, akisafiri kuelekea London mwaka wa 1929.
Hakumwona tena hadi Septemba 1930 alipoamua kurejea kwa muda mfupi, kabla ya kuondoka tena mwaka wa 1931 – wakati huo Wambui alikuwa na miaka mitatu tu. Safari hii, hakumwona baba yake tena hadi mwaka wa 1946, akiwa na umri wa miaka 18.
Wambui aliishi na baba yake kwa miaka saba pekee kabla ya Kenyatta kufungwa jela kwa madai ya kuongoza harakati za Mau Mau. Akiwa binti wa mtu mashuhuri, haijulikani wazi jinsi hali hiyo ilivyoathiri maisha yake ya baadaye.
Alizaliwa mwaka 1923 na mke wa kwanza wa Kenyatta, Grace Wahu. Wambui na kaka yake Peter Muigai walikuwa watoto maarufu wa Kenyatta, hasa kwa kuwa walikuwa watu wazima wakati wa utawala wa baba yao.
Peter Muigai aliingia katika siasa na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Juja mwaka 1974, huku Wambui akiwa diwani jijini Nairobi.Kenyatta aliporejea Dagoretti Agosti 1946, ambapo Wambui aliishi na mama yake, Wambui alikuwa karibu kufanya mtihani katika shule ya Church of Scotland Mission (iliyojulikana pia kama Mambere School na sasa Musa Gitau Primary) kabla ya kujiunga na Alliance High.
‘Sikukumbuka vizuri sura ya baba yangu, lakini alikuwa anatuma picha kutoka ughaibuni, hivyo nilimtambua alipoingia,’ alikumbuka Wambui katika dibaji ya kitabu chake.Wambui alipita mtihani na akajiunga na Alliance, akiwa msichana wa kwanza katika shule hiyo ya wavulana pekee.
Kenyatta na Mbiyu Koinange walipoanzisha shule huru za Karing’a pamoja na chuo cha walimu Githunguri, baba yake alimhusisha Wambui kama mwalimu.Lakini shule hizo zilipoonekana kuwa vituo vya uasi wa Waafrika, Kenyatta na viongozi wenzake walikamatwa na kuwekwa kizuizini.
Wambui alihamia Nairobi. Baba yake, aliyefungwa miaka saba kwa kazi ngumu, aliruhusiwa kutuma barua moja tu kwa mwezi – barua ambazo nyingi zilikuwa kwa Wambui.
Alibeba jukumu la kuwa kiungo kati ya Kenyatta na dunia ya nje, ikiwemo jamii ya kimataifa.“Tulituma hadithi nyingi kwa jarida la Drum… kisha tukapanga utetezi kwa viongozi waliokuwa wakifikishwa mahakamani Kapenguria kwa msaada wa wakili D.N. Pritt,” alisema baadaye.
Wambui alipenya katika jamii mbalimbali kwa usaidizi wa wakili Pritt na kundi la wanasheria wa Kieshia – A.R. Kapila, Fitz de Souza na Jaswant Singh.Alifanikiwa kupata kazi ya ofisini kwa Ambu Patel, aliyekuwa akichapisha vitabu, na baadaye aliandika Release Jomo Kenyatta. Patel ndiye aliyeanzisha kampeni ya kumkomboa Kenyatta.
Kenyatta alipowekwa chini ya ulinzi Maralal, Wambui alitangulia kumtembelea kabla ya mke wa nne wa Kenyatta, Mama Ngina.Wambui alipanga ziara za kumuona Kenyatta na akawa mstari wa mbele katika maandalizi ya mkutano mashuhuri wa wanahabari wa kimataifa mwaka 1961.
Wakati huo, alikuwa tayari mshiriki wa harakati za Moral Rearmament Movement, zilizopigania uhuru wa Kenya kwa njia isiyo ya vurugu, kwa kutumia falsafa ya Mahatma Gandhi.Mwaka 1961, pia alikuwa mkurugenzi wa Pan African Press, wachapishaji wa magazeti ya kisiasa – maarufu likiwa Sauti ya Mwafrika.
Baada ya uhuru, alichaguliwa kuwa diwani wa Wadi ya Dagoretti Nairobi. Baada ya kuwa Naibu Meya kwa mwaka mmoja, alipanda ngazi kuwa Meya mwaka wa 1970 baada ya Isaac Lugonzo kuondolewa madarakani.Alidumu kama Meya hadi 1977, akawa mmoja wa mameya waliotumikia muda mrefu zaidi jijini.
Taarifa yake ya ghafla ya kutogombea tena iliwashangaza wengi, hasa baada ya kundi lililoongozwa na mfanyabiashara wa Nairobi Andrew Kimani Ngumba kusema hangeteuliwa tena kwa awamu ya nne.
Ngumba, aliyekuwa Naibu Meya, alikataa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro, na hilo likazua mgawanyiko mkubwa kati ya wafuasi wa Ngumba na Wambui, ikalazimisha uchaguzi kuahirishwa huku kukiwa na vitisho vya Ngumba.Pengine kwa kuona hangeshinda,Wambui aliamua kujiondoa.
Waandishi Philip Ochieng’ na Joseph Karimi walidai katika kitabu chao The Kenyatta Succession kuwa aliahidiwa wadhifa wa ubalozi Saudi Arabia, lakini mgogoro wa Entebbe – ambapo vikosi vya Israel walivamia Uganda na kuwaokoa mateka waliokuwa mikononi mwa magaidi wa Palestina – ulivuruga mipango hiyo.
Badala yake, Wambui aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza Mkenya kushikilia wadhifa mkubwa wa kidiplomasia.
Pia aliongoza National Council for Women of Kenya.’Siungi mkono ukombozi wa wanawake kwa maneno tu,’ alisema wakati mmoja. ‘Wanawake wetu lazima wajitume. Siku za wanawake kupika jikoni na kutembea nyuma ya wanaume zimepitwa na wakati.’
Jukumu lake la mwisho serikalini lilikuwa kama kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya wakati wa utawala wa Moi.