Makala

MARWA: Chipukizi anayelenga kufikia hadhi ya Lupita Nyong'o

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

PENYE nia pana njia.

Ndivyo wahenga walivyolonga na tangia zama hizo ndivyo hali ilivyo hadi sasa. Ni msemo unaonekana kuwa na mashiko kwa kiwango fulani miongoni mwa jamii. Pia ni msemo unaozidi kuthibitishwa na vijana wengi wanaojitosa kuchangamkia shughuli tofauti kwenye jitihada za kusaka riziki.

Dorcas Kambua Kelly maarufu kama Marwa ni miongoni mwa waigizaji wa kike wanaokuja wanaolenga kufikia hadhi ya kimataifa miaka ijayo. Ni mwigizaji anayeibukia pia mwanafunzi wa mwaka wa Pili katika Taasisi ya Lake Naivasha Institute anakosomea kuhitimu kwa shahada ya diploma katika masuala ya maigizo na uanahabari.

”Ingawa ndio naanza kucheza ngoma ninaamini nina talanta ya kufanya vizuri katika tasnia ya uigizaji,” alisema na kuongeza kuwa anaamini anatosha mboga kutinga upeo wa wana maigizo wa kimataifa miaka ijayo.

Aidha anasema katika ulimwengu wa uigizaji anawazia kufikia upeo wa mwigizaji Mkenya anayetamba katika filamu za kimataifa za Hollywood, Lupita Nyong’o. Anasema huvutiwa na filamu yake iitwayo Black Panther.

”Ingawa nilitamani kuhitimu katika masuala ya maigizo kama taaluma yangu tangia nikiwa mdogo nilianza kujituma katika jukwaa hili mwaka 2015 kipindi hicho nikisoma Shule ya Upili ya Presbyterian Girls High School, Pwani. Mwanzo huo nilikuwa navutiwa na kazi zake msanii wa Bongo Muvi, Elizabeth Michael,” akasema.

MKE SUMU

Binti huyu aliyezaliwa mwaka 2000 anajivunia kushiriki filamu tatu ‘House of Commotion’ na ‘Misukosuko’ zilizobahatika kupeperushwa kupitia KTN Burudani. Pia ameshiriki filamu kwa jina ‘Mke sumu,’ zote zilizozalishwa na Bahati Zenawood Production. Katika mpango mzima anasema ndani ya miaka mitano ijayo anatarajia kuwa amejijenga kisanaa hasa kwa kushiriki filamu nyingi tu na kupata nafasi kupeperushwa kupitia runinga tofauti nchini.

Kwa waigizaji wa humu nchini anasema angependa kufanya kazi na wasanii kama dada anayezidi kujizolea sifa sio haba Yasmeen Said maarufu Maria katika kipindi cha Maria cha Citizen TV. Pia Brenda Wairimu ambaye huigiza katika kipindi cha Selina ambacho huonyeshwa kupitia Maisha Magic TV. Kwa wanamaigizo wa kimataita anasema angependa kufanya kazi na mwigizaji wa Bongo muvi, Wema Sepetu.

HIMIZO

Anatoa wito kwa serikali za Kaunti ziwazie kuanzisha kumbi za kuonyesha filamu ili wenye talanta kupata maeneo ya karibu wanakoweza kuonyesha talanta zao. Pia anasema itakuwa vizuri kwa serikali endapo itafungua vituo vya kutoa mafunzo kwa waigizaji wanaokuja wanaume na wanawake ambao wamefurika katika kila pembe mwa taifa hili.

USHAURI

Kwa waigizaji wanaokuja kwenye gemu anawahimiza wawe wabunifu pia wasiwe wepesi wa kuvunjika moyo. ”Kwa wenzangu wanastahili kuelewa kuwa changamoto ni tele bali wanastahili kuwa wavumilifu. Pia wanastahili kufahamu kuwa sio rahisi kupata nafasi ya ajira maana kila sekta ina pandashuka zake.” Pia anawashauri kuwa makini zaidi ili kuwakwepa maprodusa wale hupenda kuwashusha wanawake hadhi.