• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Masaibu bondeni Kerio yahusishwa na nguvu za giza

Masaibu bondeni Kerio yahusishwa na nguvu za giza

NA OSCAR KAKAI

TANGU serikali ilipotangaza operesheni ya Maliza Uhalifu katika eneo la Kerio Valley, kumeshuhudiwa matukio mengi yasiyoeleweka na ajali za kutatanisha zinazohusisha maafisa wa usalama nchini.

Kifo cha ghafla cha Mkuu wa Majeshi nchini (CDF), Francis Ogolla na wanajeshi wengine tisa kufuatia ajali ya ndege eneo la Sindar, wadi ya Endo, kaunti ya Elgeyo Marakwet mnamo Alhamisi wakiwa kwenye misheni ya kusaka amani, kimezua minong’ono miongoni mwa wakazi.

Japo baadhi walilalamikia kile walidai ni hali mbovu za ndege za kijeshi, wapo wakazi wanaodai kuna nguvu za giza.

Jenerali Ogolla alifariki chini ya dakika mbili kutoka shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel, katika kaunti ya Pokot Magharibi.

Ni mahali hapo ambapo inadaiwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki aliponea kifo chupuchupu baada ya nyoka kutaka kumuuma mnamo Desemba 2023.

Kulingana na wakazi ambao walikuwepo, nyoka huyo alichomokea kwenye nyasi ndefu ambazo zilikuwa zimemea kwenye uwanja wa shule hiyo na alimlenga waziri.

Kwa bahati nzuri, aliuawa na afisa wa usalama kwenye kaunti hiyo.

Kabla ya hilo, ndege ilianguka katika uwanja wa shule ya msingi ya Chemolingot, kaunti ndogo ya Tiaty Magharibi, Kaunti ya Baringo, ikiwa imewabeba maafisa wakuu wa usalama akiwemo Waziri wa Ulinzi Aden Duale ambaye alikuwa kwenye ziara ya eneo hilo Julai 2023.

Kwa bahati nzuri, watu wote waliokuwa kwenye ndege hiyo wakiwemo maafisa wakuu wa jeshi kama brigedia wa operesheni kwenye jeshi Ahmed Saman na Meja Jenerali Jeff Nyagah na wengine, walitoka bila majeraha yoyote.

Ndege yao ilikuwa imegonga mti ilipojaribu kupaa.

Safari hiyo ilisitishwa ghafla.

Isitoshe, maafisa wengi wa usalama wameuawa eneo hilo wakiwa kwenye operesheni za kudumisha usalama.

Aidha, mifugo nyingi imeuawa huku maafisa wa usalama katika maeneo ya Lokor, Napip, Kaakong, KWS, Lotapat, Kalemorock na Kadeng’oi wakikabiliwa na masaibu tele.

Hii imeleta minong’ono ya chini kwa chini kutoka kwa wakazi wa jamii za eneo hilo kwamba hivyo ni vimbwanga.
Wakazi wa eneo hilo sasa wanahofu kuwa shida iliyoko ni suala ambalo linafaa kuangaliwa na wazee.

Wengi wanasema kuwa licha ya jeshi kukita kambi eneo hilo la Bonde la Kerio, operesheni hiyo haijazaa matunda na imekuwa gharama kubwa na hasara kuu kwa serikali na mashirika ya kijamii.

Wanasema kuwa maafisa wakuu wa usalama wanakumbwa na masaibu mengi wakiwa kwenye shughuli za kuimarisha usalama.

“Tulishangaa kuona nyoka ikichomokea kwa nyasi na kumkaribia mkubwa. Tunashangazwa na matukio yasiyoeleweka kuhusu maafisa wakuu. Lazima kuna kitu kibaya ama mikosi katika eneo hilo,” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa.

Mzee mwingine kutoka eneo la Tiaty ambaye naye pia aliomba tubane jina lake, anasema kuwa baadhi ya watu kutoka jamii za Pokot, Marakwet na Turkana hawajafurahishwa na kuuawa kwa mifugo yao wakidai wanajeshi ambao wanaendeleza operesheni ya kiusalama eneo hilo nao wanafaa kujisafisha.

“Mifugo ndio benki yetu kama wafugaji,” anasema.

Anaeleza kuwa zamani watu fulani wenye ushawishi na nguvu za giza walikuwa wanafanya ndege ikwame angani.

Anadai kuwa baadhi ya wazee wanaweza hata kuzuia oparesheni ya kiusalama isifanikiwe.

“Wengine wangetuma nyoka kuwauma na kuwaua maafisa wa usalama ikiwa watatatiza amani. Ndege itazunguka aje angani na ianguke? Lazima kuna kitu kibaya,” anasema.

Anasema kuwa kuuwa kwa mifugo huenda kuwaathiri maafisa wa usalama wanaohudumu katika eneo hilo.

Anasema kuwa kuuawa kwa mifugo wao kumewaweka kwenye umaskini na kunachangia baa la njaa na uchumi wa eneo hilo kudorora.

“Mifugo ni tegemeo la maisha yetu hivyo wasitumie mabomu kuua mifugo yenyewe. Ng’ombe hawana hatia hivyo wawalenge majangili,” anasema.

Anadai kuwa watu wengine kwenye vijiji ni wachawi na hufanya mambo mabaya.

“Wazee wengine ni wabaya na wanaweza kuwapa majangili mitishamba kuchanganya, kuua ama kuiba mifugo. Hakuna kitu kitafanyika kwenye operesheni ikiwa serikali haitawaondoa,” anasema.

Hata hivyo, mwenyekiti wa jamii ya Pokot John Muok anapuzulia mbali mawazo hayo duni akisema kuwa ajali ni kitu cha kawaida ambacho hutokea kwa bahati mbaya na watu wanafaa kukoma kusambaza uvumi usiokuwa na ukweli na mashiko.

“Kuna ushirikina na uchawi ndio lakini kwa mtazamo wangu, hufanya kazi kati ya jamii za eneo hilo pekee na nguvu hizo haziwezi kuathiri mtu wa nje ambaye sio wa jamii husika,” anasema Bw Muok.

Anasema kuwa maafisa wakuu wa usalama nchini wana uhusiano mwema na jamii ya Pokot.

“Hatuna shida na serikali. Wanafanya kazi yao vyema,” anasema.

Alipuzilia mbali propaganda za kuwepo kwa uchawi akisema kuwa nyakati za sasa, watu wengi wanafuata imani za kidini na wameokoka na hawaungi mkoni mila na tamaduni potovu kama hizo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Uchaguzi wa mashinani unavyotishia UDA, ODM

Iran yafananisha shambulio la Israel na...

T L