• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Masaibu ya Konstebo Apollo Kioria ndani ya ajira ya polisi

Masaibu ya Konstebo Apollo Kioria ndani ya ajira ya polisi

Na MWANGI MUIRURI

KONSTEBO Apollo Kahungu Kioria, 37, anasononeka si haba na raia wanaofuatilia kile kinaweza kutajwa kama masaibu yake ndani ya ajira ya kikosi cha polisi wanashindwa kuelewa haki hupatikana wapi ikiwa maafisa wa usalama pia wanapitia aina fulani ya mahangaiko.

Masaibu ya Konstebo huyu yamo katika hali kwamba anadai kutoka kwa mwajiri wake jumla ya Sh2.8 milioni ambazo ni haki yake kwa mujibu wa utathmini wa mamlaka husika iliyoamrisha alipwe.

Pesa hizo ni fidia ya majeraha aliyopata akiwa kazini na ambayo mnamo Januari 14, 2015, idara ya ukadiriaji fidia katika mazingira ya kikazi – Directorate of Occupational Health Safety Services – ilisema alipwe jumla ya Sh 1,805, 886.

Agizo hilo lilitolewa chini ya barua rasmi Mrg/112/2015.

Katika kufuatilia fidia hii yake ilipwe, Bw Kioria amejipata katika kila aina ya shida na mwajiri wake ambapo amekuwa akipewa uhamisho bila mpangilio na akichanganyikiwa atii uhamisho gani na atupilie mbali upi, na hivyo hujipata amesimamishwa kazi au mshahara wake kusimamishwa.

Pia, maafisa wa ngazi za juu katika ajira yake ambao wanafaa kuwa katika mstari wa mbele wa kumsaidia aafikie haki zake kama mwajiriwa wamedaiwa kuwa mstari wa mbele kumhangaisha na kumtenga, ishara zote zikiashiria uwezekano kuwa baadhi yao huenda wanamtaka awaahidi kuwa pesa zake zikilipwa, atawatengea kiasi fulani.

Hii ni hali ambayo imempata akiwa anadai mshahara wa miaka miwili kutoka kwa mwajiri wake na mara kwa mara akitumia huduma za mawakili amekuwa akiandika barua nyingi kwa tume ya kuajiri maafisa wa polisi  (NPSC) sawia na makao makuu ya polisi yakiongozwa kwa sasa na Inspekta Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai.

Licha ya hayo, hakuna afueni amepata hivyo basi kumgeuza afande Kioria kuwa mwanaharakati katika mitandao ya kijamii, mambo yakichacha, kwa wakati mmoja Mei 2019 alipochapisha maneno au kauli inayoonyesha kutamaushwa kabisa.

Katika ujumbe huo, mzawa huyu wa Kaunti ya Murang’a na ambaye alihusika pakubwa katika vita vya 2007 vya kudhalilisha kundi haramu la Mungiki aliacha wosia katika ukurasa wake wa Facebook akitaka azikwe katika makaburi ya umma ikiwa angeaga dunia akifuatilia haki zake.

Aliwaagiza marafiki zake wasichange pesa kwa matanga au mazishi yake bali usaidizi wote uwadilishwe kwa familia za mitaani; chokoraa.

Bado mahangaiko yanatokota.

“Kwa miaka miwili nadai mshahara wangu ambao ni Sh21,510 kama mshahara wa msingi, ongeza marupurupu ya Sh8,900 kila mwezi kisha ujumlishe hesabu hiyo na miezi 24,” anasema Kioria.

Masaibu yake yanaonekana kuchochewa na ukaidi katika NPSC na NPS kwa kuwa mnamo Mei 13, 2016, Sarah Muthiga akiandika kwa niaba ya katibu Maalum katika wizara ya Usalama wa ndani Karanja Kibicho alizitaka tume za NPSC na NPS zilipe afisa huyu gharama hiyo ya ujumla kabla ya siku 14 ili kujiepusha na kuandaliwa kesi kortini.

Kuishtaki serikali

Kupitia kampuni ya uwakili ya Kirubi, Mwangi Ben advocates, Konstebo Kioria alikuwa ametisha kupitia ilani 12 ya 2016 kushtaki serikali kwa kukaidi kutimiza matakwa ya haki zake za kimsingi ya kulipwa fidia akiumia katika mazingara ya kikazi.

Aliajiriwa kazi mwaka wa 2006, na akiwa katika Kaunti ya Murang’a kuwajibikia ajira yake, mnamo Septemba 30, 2013, aligongwa na gari na akapata majeraha mabaya katika mkono na mguu upande wa kulia.

Maasaibu yake yalimwandama kwa kuwa alilazwa katika hospitali kuu ya Nyeri na Machi 27, 2014 bibi yake alimwachia mtoto mchanga na akahepa akisingizia kukosekana kwa mtu wa kutunza familia.

Safari yake ya kulazwa akitoka hospitalini ikaanza na hadi leo hii, maisha yake yamegeuka kuwa ya ulemavu, hali ambayo NPSC na NPS hazionekani kutambua ili kumpa aidha kazi nyepesi au kuamua kumstaafisha na alipwe fidia.

Hata hivyo, hawezi akastaafishwa kwa lazima kwa kuwa katiba na sheria za nchi zinakataa mtu kubaguliwa kwa msingi wowote ule.

Mahangaiko yake yamkekuwa mengi kiasi kwamba amekuwa akipokezwa barua za kinidhamu anapolemewa kujitokeza kazini kwa kuwa hana mshahara au fidia na pia kazi yake haijabainishwa rasmi katika hali yake ya kisasa ambayo ni ya ulemavu.

Akiwa mpangaji ambaye hulipa kodi ya Sh6,500 katika mtaa wa Kasarani, anahitaji kugharamia madawa yake ya kimatibabu, gharama za kliniki na piakujigharamia mahitaji yake ya kawaida, maisha yake yamegeuka kuwa sio ya afisa wa polisi bali ni ya mtumwa ndani ya huduma ya kiusalama.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa NPSC , Eliud Kinuthia, kesi ya afisa huyu inazingatiwa.

“Kumbuka nimeingia afisini hivi majuzi na suala la kwanza ambalo nimekumbana nalo ni hili kumhusu afisa huyu. Nimefuatilia hali yake na ninawiana na wengi kuwa kuna haja ya kumshughulikia kwa dharura. Hata hivyo unafaa uelewe kuwa unaweza ukasema anahangaishwa lakini katika vikosi vya kiusalama, lugha ni tofauti kwa kuwa katika hali zote afisa ameamrishwa na huduma kuwa na nidhamu,” anasema.

Kuhusu ni wapi Konstebo huyu anaweza kuwa amekosea katika vigezo vya kinidhamu, aidha iwe ni kupitia kujipata na majeraha kazini au kubakia mlemavu na asiye na uwezo wa kushiriki kazi ngumu ndani ya ajira, Bw Kinuthia anasema “hayo tuachie ndani ya NPSC.”

Anasema kuwa hadi sasa kesi ya afisa huyu inashughulikiwa katika kamati teule ndani ya NPSC na hivi karibuni afueni itapatikana.

Hivi karibuni ambayo hajabainisha iwe wakati wa uhakika, akisema tu “tunajituma kushughulika.”

You can share this post!

AKILIMALI: Kuna njia bora zaidi ya kuzalisha mbegu bora za...

AFCON 2019: Zifa yatangaza kikosi cha Zimbabwe licha ya...

adminleo