Makala

Mashahidi zaidi ya 20 walivyomhusisha Lali na kifo cha binti wa Keroche

Na RICHARD MUNGUTI October 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUFUATIA kifo cha kutatanisha cha binti wa Seneta wa Nakuru Tabitha Karanja, mahakama Ijumaa iliamuru ashtakiwe kwa mauaji.

Hakimu mwandamizi Mahakama ya Kibera, Bi Zainab Abdul aliamuru Omari Lali ashtakiwe kwa mauaji ya Tecra Mungai.

Tecra aliyetazamiwa kuwa mrithi wa kiwanda cha kutengeneza mfinyo cha Keroche Breweries (KBL) kilichoko Naivasha alikufa katika mazingira tata katika hoteli moja ya kitalii  eneo la Pwani.

Bi Abdul aliyechunguza kifo hicho alifikia uamuzi kwamba “Omari Lali ashtakiwe kwa mauaji.”

Akitoa uamuzi hakimu alisema “baada ya kutathmini ushahidi niliopokea ni bayana kwamba lawama za mauaji ya Tecra zinamuota mpenziwe Omari Lali.”

Hakimu aliendelea  kusema kwamba ushahidi wote uliowasilishwa umebaini ni yeye (Omari Lali) aliyehusika na kifo cha Tecra.

Familia ya Karanja iliwakilishwa katika uchunguzi huo na wakili mwenye tajriba ya juu James Orengo na wakili Profesa Elisha Ongoya.

Baada ya kupokea taarifa za mashahidi zaidi ya 20 hakimu alisema “Lali alihusika na mauaji ya Tecra.”

Kufuatia uamuzi Bi Abdul aliamuru faili ya kesi hiyo ipelekewe Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga ndipo amfungulie mashtaka ya mauaji Omari Lali.

Awali  Lali alikuwa ameshtakiwa kwa mauaji lakini DPP wa zamani Noordin Haji alisitisha mashtaka na kuamuru uchunguzi ufanywe na idara ya mahakama kubaini kilicho sababisha kifo cha Tecra.

“Nimefikia uamuzi kwamba Lali alihusika na kifo cha Tecra. Hivyo basi hii imepata kwamba Lali alihusika na mauaji ya Tecra,” alisema Bi Abdul Ijumaa katika uamuzi aliosoma kupitia video mtandaoni.

Alimpendekezea DPP Lali ashtakiwe kwa mauaji kinyume cha Sheria Nambari 203 na 204 za Uhalifu.
Hakimu alisema kwamba fuvu la kichwa cha Tecra lilikuwa limepasuka mbali na majeraha mengine aliyokuwa nayo binti huyo wa mmiliki wa kampuni ya pombe ya Keroche Breweries.

Mahakama ilisema Tecra na Lali walikuwa wawili tu alipokufa.

Hakimu alisema ijapokuwa Lali alijitetea kwamba Tecra alianguka na kujeruhiwa ni bayana majeraha aliyopata hayaambatani na mtu aliyeanguka.

Hakimu alisema ubongo wa Tecra ulikuwa na majeraha mabaya.

Pia alisema Lali alijikanganya katika ushahidi wake. Kabla ya kifo chake Tecra watu wa familia yake walikuwa wamemshinikiza avunje urafiki wake na Lali.

Sasa DPP atapata samanzi siku ile Lali atafika kortini kufunguliwa mashtaka ya mauaji yaliyotokea Aprili 2020