Makala

Maswali serikali ikirejesha sheria ya upakiaji viazi iliyopingwa vikali awali

Na CHARLES WANYORO December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WIZARA ya Kilimo itaanza kutekeleza Sheria ya Viazi Ulaya ya 2019 ambayo inaweka kikomo cha upakiaji wa viazi kuwa kilo 50.

Utekelezaji huu ulisitishwa miaka mitatu iliyopita baada ya kuibuka kwa pingamizi.

Meneja wa Baraza la Kitaifa la Ukuzaji Viazi Henry Chemjor amesema uamuzi wa usitishaji huo mnamo 2021 ulitokana na vikao vya kusikiliza malalamishi ya wakulima na changamoto nyingine.

“Tumeanza mazungumzo na Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) na washirika wengine kupiga jeki utekelezaji,” akasema Bw Chemjor.

Tayari AFA imetoa mafunzo kwa zaidi ya wakaguzi 250 wa mimea kusaidia katika msako wa wanaokiuka kanuni kwa kurefusha magunia hivyo kuwapunja wakulima.

Magunia makubwa yaliyopakiwa viazi kinyume cha sheria shambani Narok. Picha|Labaan Shabaan

Katika kanuni hiyo, wakulima, wanabiashara, wasafirishaji na wasindikaji wanahitajiwa kujisajili na serikali za kaunti; la sivyo watozwe faini ya Sh5 milioni ama kifungo cha miaka mitatu jela.

Bw Chemjor alizungumza katika soko la Katheri, Kaunti ya Meru katika warsha ya mafunzo ya wakulima kuhusu kilimo cha viazi.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la Korea Kusini, KOPIA.

Baraza la viazi limekuwa likitoa hamasa kwa wakulima ili kuwawezesha wakumbatie kanuni hii.

Afisa Mkuu wa Kilimo, Kaunti ya Meru, James Mutia alisema utekelezaji wa sheria hii utakumbwa na changamoto iwapo wakulima hawatajifunza mbinu za kisasa za kuhifadhi mazao.

Vibarua wapakia magunia ya viazi kwenye trekta Narok. Picha|Labaan Shabaan

Bila mbinu hizi, wakulima hulazimika kuuza viazi baada ya kuvuna kwa bei ambayo inaamuliwa na madalali.

“Hata tukiwaambia Wakulima wauze viazi kwa magunia ya kilo 50 na hali hawajui kuhifadhi, watalazimika kuuza kwa mnunuzi yeyote ama mavuno yaharibike,” akasema Bw Mutia.

Mkurugenzi wa KOPIA Kenya Ji Gang Kim anasema, takriban asilimia 20 ya viazi ambavyo huvunwa Meru huharibika ama kupotea kila mwaka kwa sababu ya usimamizi mbaya wa mavuno.

Hii ina maana kuwa, angalau tani 815,000 za viazi huharibika baada ya mavuno.

Mshirikishi wa KOPIA eneo la Meru, Julius Gitonga alisema wamekita maghala katika maeneo ya Katheri na Murungurune ambapo wakulima watahifadhi viazi kwa angalau mwezi mmoja baada ya mavuno.

Vibarua wakivuna viazi ulaya Narok. Picha|Labaan Shabaan

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan