• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Matamanio ya kidosho 2024 kupata ‘mpoa’ asiye na hasira

Matamanio ya kidosho 2024 kupata ‘mpoa’ asiye na hasira

NA MWANGI MUIRURI

DOREEN Natecho 23, anasema kwamba maono yake ya Mwaka Mpya 2024 ni kuokoka na kuanza kumhudumia Mungu kama chombo chake cha Injili.

Kabla ya aokoke, anasema kwamba atawasamehea wote waliomkosea maishani, huku naye akitarajia umsamehe ikiwa ameshawahi kukukosea.

“Mimi nimeonelea kwamba katika haya maisha hakuna cha maana zaidi kuliko kumtegemea Mungu katika hali zote na kuhakikisha unaeneza wema wake kwa wote,” anasema.

Bi Natecho anaongeza kwamba kwa sasa hana mchumba lakini yeye atang’ang’ania kujipa nembo zote za mke mwema mtarajiwa akingoja Mungu ampe wake wa roho.

“Ndio naelewa kwamba ni lazima mimi nichangie kumnasa wangu wa roho…Najua kwamba ni mimi niliye sokoni wala sio Mungu…Lakini najua kwa dhati kwamba juhudi zangu zote pasipo kumhusisha Mungu zitaishia kuwa za bure,” anasema.

Iwapo atampata wake mzuri wa moyo, Bi Natecho anaomba kwamba “asiwe ni wa hasira na fujo…Asiwe wale wa kuwa na ulafi na tamaa”.

Anasema angetaka mpoa wake awe ni wa maono ya mbali katika mazingara ya kutekeleza bidii katika majukumu yote.

“Sitaki wa kutelekeza majukumu yake…hata kwa hayo unayowazia sitaki mzembe ndio nisiwe wa kuingiwa na mahangaiko hata ya kufikiria kwenda malishoni nje,” asema.

Katika utumishi wake kwa Mungu, Bi Natecho anasema kwamba atalenga kueneza matumaini katika hali za magumu maishani, subira, kuridhiana na kusameheana na watu kuheshimu uhai kama uliyotuzwa binadamu na Mungu na ndiye pekee anafaa kuutwaa.

“Siku hizi unapata watu wako mbioni kuuana ni kama binadamu tumekuwa mende ambaye kila akionekana hupondwa. Hata katika hali ambazo la busara lingekuwa kujiepusha na kuondokea hatari ya kutoa uhai, unajiingiza tu kwa mauaji kiholela,” asema.

Bi Natecho anasema Kenya ni ya Mungu na katika hali zote “sisi ni wateule wa kubarikiwa na hatutalaaniwa kwa vyovyote vile”.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, alisema katika hali zote Wakenya wanafaa waelewe kwamba kuna Mungu mbinguni ambaye huwawazia baraka za ufanisi na hata majaribu yakija kama mawimbi ya baharini, Mungu atabakia kutawaza taifa hili katika jukwaa la ufanisi”.

Bi Natecho alisema kwamba mwaka wa 2024 utakuwa wa uzinduzi ambapo yote ya kale yatafanywa mapya.

“Msiwe wa kufa moyo kwa urahisi…Hali itakuwa ya afueni katika safu za kijamii na pia kisiasa na kiuchumi. Watoto watasoma, magonjwa yatashindwa na majanga yatatukoma kwa kuwa Mungu bado yuko katika kiti cha enzi,” akasema.

Aidha, anawataka Wakenya wawe wa kumtumainia Mungu wala sio wanasiasa na la mno “tuwe watu wa kuomba kwa dhati tukimsihi Mungu awe wa neema kwetu na asituonyeshe kisogo chake katika talaka ya baraka kwa kuwa tutaisha”.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mwaka Mpya 2024 ulivyokaribishwa

Viatu vinavyoundwa kwa magamba ya samaki

T L