MATHEKA: DPP hana nia ya kweli ya kupiga vita ufisadi nchini
NA BENSON MATHEKA
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji alipotangaza kuwa afisi yake itazindua njia mbadala za kutatua kesi za ufisadi, wengi walifikiri kuwa alitaka kupunguza muda ambao kesi huwa zinachukua kortini.
Hatua hii ingepunguza mrundiko wa kesi katika mahakama ambazo zimekuwa zikilimbikiziwa lawama kwa kuchelewesha haki.
Bw Haji alisema kwamba nia yake ilikuwa ni kuhakikisha pesa za umma zilizoporwa zimerejeshwa na washukiwa kupata adhabu nafuu.
Kulingana naye, haya yanaweza kuafikiwa kupitia mazungumzo kati ya washukiwa na afisi yake.
Hata hivyo, kulingana na masharti ambayo aliwekea washukiwa wanaotaka kufuata njia ya mazungumzo, itakuwa vigumu kuafikia malengo yake.
Kwanza, itakuwa vigumu kwa washukiwa kukubali walitenda makosa anavyodhani, ikizingatiwa wengi wao ni watu wenye ushawishi nchini na wamejawa na kiburi.
Pili, ni mali ya washukiwa wa ufisadi imekuwa ikitwaliwa na serikali au akaunti za benki kuzimwa hivi kwamba hawawezi kutumia pesa wanazodaiwa kupora.
Tatu, washukiwa wote wamekataa mashtaka na wako nje kwa dhamana kesi zikiendelea kortini na nne, katiba ya Kenya inasema kila mshukiwa huchukiliwa kuwa hana hatia hadi mahakama iamue kwamba alitenda makosa yanayomkabili kortini.
Sisemi kuwa mbinu ya waendesha mashtaka kukubaliana na washukiwa kwa lengo la kupunguziwa adhabu haifai. Kwa hakika, imeruhusiwa kisheria na imekuwa ikitumiwa.
Ni masharti ya Bw Haji ambayo yatafanya washukiwa kukosa kuikumbatia hasa kwa kuwataka wakiri makosa, wakubali kurudisha mara tatu kiwango cha pesa watakazokiri waliiba na wawe tayari kutumikia kifungo cha muda usiopungua miezi sita jela.
Hii inamaanisha kuwa washukiwa ambao wengi wanashikilia nyadhifa za umma wakiwemo mawaziri na magavana hawataweza kurudi ofisini au kuteuliwa au kugombea wadhifa wowote wa umma.
Ikizingatiwa kuwa mara nyingi kesi hutupiliwa mbali kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi kutokana na mapengo katika uchunguzi au udhaifu wa waendesha mashtaka, kuna uwezekano mawakili wa washtakiwa watawashauri wasikubali mbinu hii na kuendelea na kesi hadi mwisho mahakama itoe uamuzi.
Kile ambacho Bw Haji hakueleza Wakenya ni kuwa hata baada ya upande wa mashtaka kukubaliana na mshukiwa akiri kesi, ni mahakama iliyo na uwezo wa kuamua hukumu kumaanisha inaweza kutoa adhabu tofauti na ambayo waendesha mashtaka watapendekeza.
Katika nchi jirani ya Tanzania, mbinu hii ilitumiwa bila masharti magumu na ikafaulu. Kupitia agizo la Rais John Magufuli, washukiwa walitakiwa kurejesha mali ya umma pekee ili waachiliwe huru.
Katika muda wa wiki tatu, watu 500 walikuwa wamejisajili katika mpango huu na kurudisha mabilioni ya pesa za umma.
Serikali ya Tanzania ililenga washukiwa waliokuwa seli kwanza ambao walikuwa wakiweka mkataba na serikali kuhusu jinsi ya kurudisha pesa walizoiba na kesi kuondolewa kortini.
Ni mpango mzuri ambao Kenya inapaswa kuiga ikiwa inataka uzae matunda.