Makala

MATHEKA: Haifai Wakenya kuamini wanasiasa kuhusu BBI

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

MCHAKATO wa kubadilisha katiba ambao ulianzishwa miaka miwili iliyopita kufuatia handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga umeingia awamu muhimu ya kukusanya saini kuunga mswada utakaowasilishwa kwenye kura ya maamuzi.

Ingawa awali baadhi ya wanasiasa walikuwa wamepinga mchakato huo, wameanza kuonyesha dalili kwamba wanauunga mkono hata kama masuala ambayo walikosoa hayakutatuliwa kikamilifu. Hii ni kwa sababu waligundua kwamba mageuzi hayo yatakuwa na manufaa kwao binafsi na sio kwa wananchi wa kawaida.

Ikiwa hakutakuwa na kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi kitaifa atakayepinga mswada huo wananchi wataamini kwamba unalenga kuimarisha maisha yao ingawa sio kweli. Shida ya Wakenya, na imesemwa mara nyingi na wachanganuzi huru wa utawala, ni kuamini chochote wanachoambiwa na wanasiasa.

Uchunguzi wa kina wa mageuzi yanayopendekezwa unafichua kuwa ni wanasiasa watakaonufaika kwa mswada huo ukipitishwa kwenye kura ya maamuzi.

Ajabu ni kuwa, ni huu ndio ukweli wa mambo na ni wananchi watakaopitisha mapendekezo hayo wakidhani yatawanufaisha. Hii ni ndoto. Kila wakati wanasiasa wanapoungana kupanga jambo huwa wanalenga kutilia maanani maslahi yao. Ili kuepuka lawama, huwa wanatumia umma kutia muhuri malengo yao na kwa sababu kazi ya raia ni kuabudu viongozi wa kisiasa wa makabila yao, mwishowe hujipata wameanguka kwenye mitego.

Hivi ndivyo ilivyo katika mswada wa kurekebisha katiba wa BBI. Kwa sasa wanasiasa wanazunguka kote nchini wakiwarai raia kuunga mswada huo na kuupitishwa kwenye kura ya maamuzi. Kuna uwezekano kuwa ifikapo mwisho wa mwaka ujao, muda mfupi baada ya kupitisha mswada huo, ambao hali inaonyesha utapita, Wakenya wataanza kulia kwamba wanakadamizwa.

Kilio hicho kitazidi baada ya uchaguzi mkuu ujao watakapobeba mzigo wa kulipa wabunge 600 katika mabunge mawili. Hawaulizi maswali kuhusu zikapotoka pesa za kuwalipa wabunge hao mishahara.

Hawaulizi maswali kuhusu zitakapotoka pesa za kugawia serikali za kaunti asilimia 35 ya mapato ya serikali katika nchi ambayo inategemea madeni kwa kuwa haitimizi viwango vya ukusanyaji ushuru. Wanachangamkia pendekezo la kubuniwa kwa waziri mkuu na manaibu wawili bila kuuliza zitakapotoka pesa kuwalipa mishahara na gharama ya kuendesha afisi zao.

Hii ndiyo sababu wameanza kutoa saini zao kuunga mswada huo bila kuuliza kitachowapata baada ya katiba kurekebishwa. Wakati watakapokuwa wakilia, wanasiasa watakuwa wakigawana nyadhifa walizowatumia kuzibuni nao watakuwa wakilala njaa. Watakaokosa kupata nyadhifa za uongozi, watarudi katika maeneo yao kulia kwamba jamii yao imebaguliwa.

Wangebaini kuwa mapendekezo yanayodaiwa kuwa ya kuwanufaisha hayahitaji katiba kubadilishwa, wangewauliza viongozi kwa nini hawangeweka sera na kuzitekeleza awali.

Matatizo yote ya nchi hii yanatokana na tabia ya Wakenya ya kuamini wanasiasa na ujanja wao. Chochote kinachotoka kwa wanasiasa ni chao. Wanachofanya ni kubuni mikakati ya kutumia umma na ndivyo inavyofanyika wakati huu wa mchakato wa kubadilisha katiba unaodaiwa kuwa wa kuleta maridhiano nchini.