• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
MATHEKA: NSAC ingezima mikutano yote, corona italipuka tena

MATHEKA: NSAC ingezima mikutano yote, corona italipuka tena

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya serikali ya kutoa kanuni za kuzuia ghasia katika mikutano ya kisiasa inafaa hasa ikizingatiwa kuwa fujo ni hatari kwa usalama wa taifa.

Fujo hizi hutokea wanasiasa wanapotoa matamshi ya uchochezi na kuna haja ya kuchukua hatua za kuzizuia.

Ni wazi kuwa hatua hiyo ilifuatia ghasia zilizotokea mjini Kenol, Kaunti ya Murang’a ambapo watu wawili walipoteza maisha yao makundi mawili hasimu yalipokabiliana. Wanasiasa pia wamekuwa wakitoa matamshi yanayoweza kuzua uhasama wa kijamii.

Hata hivyo, kwa kutoa mwongozo kuhusu jinsi mikutano ya kisiasa inavyofaa kuandaliwa, serikali imesahau kwamba kuna virusi vya corona vinavyoweza kusambazwa katika mikutano hiyo ambayo kwa kawaida imekuwa ikihudhuriwa na watu wengi.

Hii inaonyesha kuwa imeacha vita dhidi ya virusi hivyo huku idadi ya maambukizi na vifo vikizidi kupanda.

Kinaya ni kwamba Baraza la Kitaifa la Ushauri wa Kiusalama (NSAC) lililotoa kanuni za kuzingatiwa kuandaa mikutano ya kisiasa ni miongoni mwa vitengo vya serikali ambavyo vimekuwa vikimshauri Rais kuhusu hatua za kukabiliana na corona.

Inashangaza basi, licha ya kusema kwamba huu sio wakati wa kuendeleza siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 baraza hilo liliruhusu mikutano ya kisiasa kuendelea wakati ambao kuna hatari ya kuzuka upya kwa wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Kuna wanaohisi kwamba hatua hii inanuiwa kutoa nafasi kwa kampeni za kupigia debe ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Marufuku ya watu kukusanyika ambayo yalitangazwa kama njia moja ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivi hayakuwa yameondolewa wakati ambao NSAC ilitangaza kanuni za kuandaa mikutano ya kisiasa Jumatano wiki hii.

Ingawa wanasiasa wamekuwa wakikaidi kanuni hizo, ingekuwa bora kama baraza hilo lingesisitiza kuwa kwa wakati huu, ni makosa kuandaa mikutano ya kisiasa hadi marufuku ya watu kukusanyika yatakapoondolewa.

Kwa kuruhusu wanasiasa kuandaa mikutano, serikali imeonyesha ukosefu wa msimamo katika kutoa maamuzi na utekelezaji wake.

Hii ndio sababu viongozi wakuu wamekuwa wakikaidi sheria wanazotaka Wakenya wa kawaida kuzitii.

Kuna maana gani NSAC kushauri Rais adumishe kafyu hadi Novemba wakati inaruhusu wanasiasa kuandaa mikutano kote nchini?

Kuna maana gani ya kuruhusu wenye vilabu na hoteli kufunga biashara zao saa nne usiku na kuruhusu wanasiasa kuandaa mikutano inayohudhuriwa na maelfu ya watu kwa wakati mmoja? Kuna haja gani ya kuagiza matatu kubeba nusu ya abiria zinazofaa kubeba?

NSAC ingeagiza polisi kutoruhusu mikutano yote ya kisiasa kwa wakati huu hadi janga la corona likabiliwe kikamilifu. Kwa kufanya hivi, wanasiasa wangekosa majukwaa ya kutumia kutoa matamshi yanayoweza kuchochea chuki za kikabila na wafuasi wao kukosa maeneo ya kupigania.

Utekelezaji wa kanuni hizi unaweza pia kuzuia migogoro wanasiasa wa baadhi ya mirengo ya kisiasa wakihisi zinatumiwa kuwazima. Ingekuwa bora kama NSAC ingezima mikutano yote ya kisiasa katika maeneo yasiyo na uchaguzi mdogo hadi uchaguzi mkuu utakapotangazwa na kuchukulia hatua watakaokiuka bila kujali mrengo wao wa kisiasa au tabaka lao katika jamii. Ni kwa kufanya hivi ambapo hali iliyoshuhudiwa Murang’a inaweza kuepukwa.

You can share this post!

ONYANGO: Kanuni mpya za mikutano zisitumiwe kufinya...

Sonko avuliwa nguo zaidi