MATHEKA: Ofisi ya DPP izingatie utaalamu kukusanya ushahidi
Na BENSON MATHEKA
MJADALA kuhusu iwapo magavana wanaoshtakiwa kwa ufisadi wanapaswa kuzuiwa kukanyaga ofisi zao umekuwa ukiendeelea kwa muda sasa.
Magavana na baadhi ya madiwani na wafuasi wa washukiwa hao wanahisi kwamba kuzuia magavana kufika katika ofisi zao ilhali walichaguliwa na watu ni kuwahujumu.
Wanasema kwamba wakiwa washukiwa, hawana hatia hadi kesi zao zitakaposikilizwa na kuamuliwa.
Ingawa wanasema hawatetei au kulinda wenzao wanaohusika na ufisadi, magavana wanahisi kwamba kuzuiwa kufika ofisini kunaathiri utoaji wa huduma na usimamizi wa serikali za kaunti zao kwa sababu maamuzi muhimu hayawezi kupitishwa na kuidhinishwa.
Kulingana na upande wa mashtaka, magavana hao wanafaa kuepuka ofisi zao kwa sababu ofisi hizo zinachukuliwa kuwa maeneo ya uhalifu na wanaweza kuvuruga ushahidi na kutisha mashahidi.
Waendesha mashtaka, wakiongozi wa Mkurugenzi wao Noordin Haji, wanasema kuwa kila afisa wa umma anayeshtakiwa au kuchunguzwa kwa ufisadi anapaswa kuondoka ofisini hadi kesi ikamilike.
Binafsi siungi mkono ufisadi wala sitetei ufisadi. Ninaamini kuwa wezi wa mali ya umma au watu wanaotumia mamlaka yao vibaya wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Ninaamini mkondo wa kisheria unapaswa kufuatwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria na haki bila ubaguzi wowote katika kesi za zote zikiwemo za ufisadi, matumizi ya pesa za umma na ulanguzi wa pesa.
Ninaamini kwamba kuruhusu magavana kufika katika ofisi zao kunaweza kuathiri kesi. Hata hivyo, ninatofautiana na sababu ambazo upande wa mashtaka umekuwa ukitoa kwamba lengo la kuzuia magavana hao kufika katika ofisi zao ni kulinda ushahidi.
Nasema hivi kwamba sababu kabla ya kufungulia mshukiwa yeyote mashtaka, upande wa mashtaka unapaswa kuwa umekusanya ushahidi unaoamini unaweza kuthibitisha kesi.
Hivyo basi, kwa kudai kwamba washukiwa wanaweza kuvuruga ushahidi ulio katika ofisi zao ni kuonyesha kuwa huwa wanafungulia washukiwa mashtaka kabla ya kupata ushahidi. Kufanya hivi ni kuvuruga kesi zao wenyewe.
Huu ni ukosefu wa utaalamu katika uchunguzi na upande wa mashtaka kwa sababu mtu yeyote anaweza kuvuruga ushahidi huo. Sishawishiki kuwa sababu ya kuzuiwa kwa washukiwa kufika katika ofisi zao ni kulinda ushahidi.
Upande wa mashtaka pia umekuwa ukidai kuwa washukiwa wanaweza kutisha mashahidi ambao ni wafanyakazi katika serikali zao. Ni haki yao kuwa na hofu ya aina hii ikizingatiwa kuwa tumeshuhudia mashahidi katika kesi tofauti zinazohusu watu wenye ushawishi wakitoweka.