• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
MATHEKA: Serikali ionyeshe nia njema kuzuia migomo

MATHEKA: Serikali ionyeshe nia njema kuzuia migomo

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI inafaa kutumia muda wa wiki mbili ambazo madaktari wamesimamisha mgomo waliopanga kuanza Jumatatu wiki hii kusuluhisha tofauti zilizoko kati yake na wahudumu wa afya ikiwa kwa kweli inajali afya ya raia wake.

Kwa kusimamisha mgomo wao baada ya ilani ya siku 21 kumalizika, madaktari wameonyesha kuwa nia yao sio kutesa wagonjwa mbali kinachowasukuma kugoma ni ukosefu wa nia njema kutoka upande wa serikali katika kuimarisha mazingira yao ya kazi.

Kugoma kwa wahudumu wa afya wote nchini wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na janga la corona kunaweza kusababisha vifo vya Wakenya wengi.

Hata kama madaktari wameonyesha uzalendo kwa kupatia serikali muda zaidi wa kutatua mzozo uliopo, hali bado ni mbaya katika hospitali za umma kote nchini ikizingatiwa kwamba wauguzi na maafisa wa utabibu nao wameanza mgomo wakilalamika kuwa serikali imewapuuza.

Kwa kawaida, ni wauguzi wanaowasaidia madaktari katika huduma zao na mgomo wao utaathiri asilimia 90 ya huduma katika hospitali za umma. Kuna wanaowalaumu wahudumu wa afya kwa kutokuwa na utu kwa kugoma wakati maambukizi ya virusi vya corona yanapoendelea kuongezeka nchini.

Hata hivyo, inafaa kubainika kuwa sio mara ya kwanza wauguzi, maafisa wa utabibu na madaktari kugoma nchini baada ya serikali kukosa kutekeleza wanayokubaliana nao kuhusu mishahara na mazingira ya kazi.

Inafaa kukumbukwa kuwa, wahudumu hao huwa hawaamki tu na kugoma, bali huwa wametumia njia zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kutoa ilani ya mgomo ya muda usiopungua siku kumi na nne.

Katika muda huo, serikali huwa na nafasi ya kuepusha mgomo sio kwa kukubali matakwa yote ya wahudumu hao bali kwa kuonyesha nia njema kwa kutimiza waliyokubaliana kwenye mikataba ya pamoja kuhusu mishahara na mazingira ya kazi.

Kama ingekuwa inafanya hivyo, ingekuwa vigumu huduma za afya nchini kuvurugwa kila mara na migomo ya wahudumu wa afya.

Ni kinaya migomo hii kutokea katika nchi ambayo serikali inajigamba kuwa inafanikisha huduma za afya kwa wote. Mpango wa huduma ya afya kwa wote, hauwezi kufaulu maslahi ya wahudumu wa afya yakipuuzwa tunavyoshuhudia humu nchini hasa wakati wa janga.

Dalili zote zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mpango huo ni kwa maneno tu.

Tusidanganyane, hakuna mpango wa afya unaoweza kufaulu wahudumu wa afya wakipuuzwa jinsi tunavyoshuhudia wakifanyiwa nchini. Wauguzi, matabibu na madaktari pia ni binadamu kama watumishi wengine wa umma ambao maslahi yao huwa yanapatiwa kipaumbele.

Baadhi yao wameangamizwa na corona wakiwa kazini. Licha ya serikali kudai imewapa vifaa vya kujikinga, wamedai kuwa vifaa hivyo ni duni huku ikifichuliwa kuwa mabilioni ya pesa za kuimarisha usalama wao kazini ziliporwa na watu wenye ushawishi wakishirikiana na maafisa wa wizara na mashirika yaliyo chini ya wizara hiyo.

Ukweli wa mambo ni kuwa kama serikali ingekuwa inatimiza na kutekeleza makubaliano yake na wahudumu wa afya, migomo hazingekuwemo.

You can share this post!

TAHARIRI: CAK yapaswa ikabili matusi mitandaoni

WANGARI: Umakinifu wahitajika katika sheria zijazo za...