Makala

MATHEKA: Uhuru atulize joto Jubilee lisielekeze nchi pabaya

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

NI wazi kuwa joto la kisiasa limeanza kupanda nchini hasa katika chama tawala cha Jubilee ambapo kuna mirengo miwili inayozozana.

Mgogoro katika chama hicho imezua mgawanyiko na Jumapili iliyopita ukisababisha mauti ya watu wawili Kaunti ya Murang’a.

Bila shaka hizi ni dalili mbaya katika nchi ambayo hukumbwa na ghasia kabla na baada ya uchaguzi.

Sio siri ghasia hizo huchochewa na kufadhiliwa na wanasiasa. Ni wanasiasa wanaotoa matamshi yanayozua uhasama wa kisiasa na kikabila nchini hasa uchaguzi mkuu unapokaribia.

Kuna hali ya vurumai ambayo inashuhudhiwa katika chama tawala cha Jubilee. Naam, chama tawala ambacho kinafaa kuwa mstari wa mbele kuunganisha Wakenya ndicho kinachowagawanya zaidi.

Hali ilivyo, kuna hatari ya mzozo katika chama hicho kusababisha umwagikaji wa damu nchini hata kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hii ni kwa sababu ya mazingira ya kisiasa nchini ambapo kuna mipango ya kubadilisha katiba huku baadhi ya wanasiasa wakiwa tayari wameanza kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Kiongozi wa nchi ambaye pia ni kiongozi wa chama tawala, Rais Uhuru Kenyatta hana budi kuchukua hatua, na kwa haraka sana, kutuliza joto la kisiasa kwa sababu ni serikali yake itakayobeba lawama zote Kenya ikitumbukia katika ghasia.

Ni kweli ameonya wanasiasa dhidi ya kushiriki kampeni za mapema lakini baadhi yao, akiwemo naibu wake wamemkaidi. Ni kweli ameonyesha uvumilivu unaofaa kwa kiongozi huku wanaoshiriki kampeni za mapema wakimkaidi.

Hata hivyo, sidhani kwamba anafaa kuendelea kuvumilia wakati wanasiasa wanaweka nchi katika hatari ya kukumbwa na umwagikaji wa damu. Nchi hii ina sheria za kutosha ambazo rais anafaa kutumia kulinda usalama wa nchi bila kukiuka haki za raia.

Akiwa kiongozi wa chama cha Jubilee ndicho kitovu cha hali inayoshuhudiwa nchini kwa sasa, Rais Kenyatta hataweza kuepuka lawama nchi ikivurugika kwa sababu ya siasa mbaya. Hakuna kinachomzuia kuvunja uhusiano wake na washirika wake wachache wa kisiasa ili kulinda maslahi ya Wakenya zaidi ya 48 milioni. Jubilee ni nyumba yake na anafaa kuipanga vyema kwanza hata kama maamuzi yake hayatafurahisha baadhi ya washirika wake.

Kuna kila dalili kwamba wanachama wa Jubilee wanaomkaidi wanamdharau kwa sababu ya uvumilivu wake lakini wakati umefika wa kuwaambia wazi kuwa imetosha.

Jambo jingine linalomweka Rais Kenyatta katika hali ngumu ni pendekezo la kubadilisha katiba kupitia mchakato wa Maridhiano (BBI) ambao wanaomkaidi katika chama cha Jubilee wanapinga. Akiwa muasisi wa mpango huo, na ikiwa nia yake ya dhati ni kuunganisha nchi, anafaa kuchunguza iwapo matokeo yake yataacha Kenya ikiwa bora zaidi au yatapalilia mgawanyiko zaidi.

Itakuwa aibu kuendelea na mchakato huo ikiwa hautafaidi Wakenya. Lakini hata ikiwa ndio tiba kwa matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo yamekuwa yakisumbua Wakenya wa matabaka yote kwa miaka mingi, kuutekeleza katika mazingira ya sasa ya kisiasa, hasa katika chama tawala Jubilee, itakuwa bure tu.