• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
MATHEKA: Vijana ni hazina ya taifa, serikali iwasaidie sasa

MATHEKA: Vijana ni hazina ya taifa, serikali iwasaidie sasa

Na BENSON MATHEKA

NCHI inayolenga kufikia kiwango cha juu cha ustawi wa kiuchumi, haiwezi kupuuza mchango wa vijana. Nchi inayowapuuza vijana wake, huwa inajiweka katika hatari kubwa ya kukwama kimaendeleo, kuvurugika kwa usalama na maadili.

Katika ulimwengu wa sasa na siku za zijazo, nchi itakayokosa kuwekeza katika miradi ya kuinua maisha ya vijana haitakuwa na nafasi ya kushindana na nyingine katika sekta mbalimbali.

Kwa wakati huu, Kenya ina nafasi nzuri ya kujiandaa kuafikia ufanisi mkubwa wa kiuchumi ikiwa itawekeza kikamilifu katika vijana ambao kulingana na sensa ya mwaka jana, ni asilimia 75 ya raia wa nchi hii.

Vijana hawa ndio nguzo ya maendeleo ya nchi na serikali ikikosa kuweka mikakati ya kuboresha maisha hao itakuwa imeweka msingi mbaya.

Hatua ya kwanza ni kuhakikisha vijana wamepata masomo yanayoafikiana na mabadiliko ya ulimwengu. Serikali inafanya hivi kupitia mfumo mpya wa masomo wa Competency Based Curriculum (CBC). Hata hivyo, itahitaji kuwekeza zaidi katika teknolojia ili kufanikisha mtaala huu.

Bila teknolojia, ubora wa elimu ambayo inapaswa kuwaandaa vijana kwa ujenzi wa taifa lao utakuwa wa kutiliwa shaka.

Serikali pia italazimika kuhakikisha gharama ya elimu ni nafuu ili kuwezesha vijana wote kunufaika. Kuelimisha watoto bila kuhakikisha watapata kazi ni kuongeza matatizo katika nchi.

Vijana wakikosa nafasi za kazi wanaweza kutumia elimu yao kutekeleza uhalifu na hii ni hatari kwa usalama wa nchi. Itakumbukwa kuwa wakati mmoja, vijana waliosomea uhandisi walichimba mtaro chini ya ardhi kuingia ndani ya benki moja mjini Thika na kuiba mali.

Hivi majuzi, vijana wawili walikamatwa wakidukua tovuti ya Shirika la Uchukuzi na Usalama (NTSA) na kusajili magari kinyume cha sheria.

Visa hivi vinaonyesha vile vijana wakikosa kazi wanaweza kutumia maarifa yao kutekeleza uhalifu na kugeuka janga kwa nchi.

Vijana wanapokosa matumaini maishani wanaweza kuwa adui wa taifa lao. Kuna wanaoshawishiwa kujiunga na makundi ya magaidi, magenge ya wahalifu na matumizi ya dawa za kulevya.

Ili kuepuka janga hili, serikali inapaswa kuweka sera madhubuti ya vijana. Sera hii inafaa kutekelezwa kikamilifu kuanzia mashinani hadi ngazi ya kitaifa ili vijana wajihisi kuwa sehemu ya serikali yao. Kwa kufanya hivyo, watahisi serikali inawathamini.

Makosa ambayo serikali hufanya ni kusahau kuwa hazina kubwa ya nchi yoyote sio utajiri wake mbali ni katika vijana wake.

Hivyo basi, kuwapuuza ni sawa na kutupa hazina hiyo. Ili kuhakikisha kwamba vijana watachangia kikamilifu katika uchumi, serikali inapaswa kuweka mazingira mazuri ili wapate kujijenga kupitia taaluma zao wanazosomea vyuo vikuu.

Mazingira kama hayo sio kuwapa mikopo pekee kupitia hazina kama ya vijana, ni kutowatoza kodi za juu, kuhakikisha kuna nguvu za stima kila mahali na kuwasaidia kupata masoko ya bidhaa zao. Mazingira yanayofaa ni kuhakikisha vijana hawaitishwi hongo kupata kazi au huduma serikalini.

Kuweka mazingira ya kuwasaidia vijana kujikuza ni kuweka msingi wa ustawi wa nchi.

You can share this post!

TAHARIRI: Tujiandae kukabili majanga ya mvua

WARUI: Matatizo yanayozonga vyuo vikuu nchini yatatuliwe

adminleo