Makala

Matiang’i pabaya? Arati kuongoza ujumbe mwingine wa Gusii kwenda Ikulu

Na WYCLIFFE NYABERI September 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

SIKU chache tu baada ya ujumbe kutoka kaunti za Kisii na Nyamira kumtembelea Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, kundi jingine liko njiani kuelekea ikulu kwa mkutano mwingine na rais.

Gavana wa Kisii Simba Arati Alhamisi, Septemba 11, 2025, anatarajiwa kuongoza baadhi ya madiwani (MCAs) wa kaunti za Kisii na Nyamira kukutana na Rais Ruto jijini Nairobi.

Ziara hiyo kulingana na madiwani hao ambao walithibitisha mwaliko wa rais, inalenga kukwamua miradi ya maendeleo kwa watu wa Gusii.

Wakihutubia wanahabari mnamo Jumanne nje ya majengo ya Bunge la Kisii, MCAs hao waliongeza kuwa mbali na kukwamua maendeleo, watatumia fursa hiyo kumwomba rais awasaidie kuharakisha uundwaji wa Hazina ya Ustawishaji wa Maendeleo ya Wadi ili hazina hiyo iwasaidie kuwatumikia vyema raia.

Diwani wa Masige Mashariki Michael Motume (katikati) aongoza wenzake kuwahutubia wanahabari mnamo Septemba 9, 2025 ili kuthibitisha kuwa watamtembelea Rais Ruto ikuluni, tena. Picha|Wycliffe Nyaberi

“Tutamsihi rais kuwa hata kama ugatuzi ulikuja, utendakazi katika ofisi za MCAs haujakamilika na kwa hivyo tutamweleza afuatilie kwa haraka ili kuundwe hazina hiyo itakayohakikisha madiwani wanatekeleza majukumu yao kwa wapiga kura,” Masige MCA wa Masige Mashariki Michael Motume alisema.

Bw Motume aliongeza kuwa pia watamwomba rais awasaidie wawekwe katika mpango wa pensheni mara tu watakapoondoka madarakani.

“Kama unavyofahamu, MCAs hawana haki ya kupata mafao yoyote ya pensheni na hivyo pia tutamwomba aharakishe katika muhula wake wa kwanza ili kuhakikisha kuwa tuna sheria ambayo inawapa madiwani pensheni,” Bw Motume aliongeza.

Wakati gavana Arati anajiandaa kuongoza ujumbe huo, mwenzake wa Nyamira Amos Nyaribo amekataa mwaliko huo.

Akizungumza Jumanne katika eneobunge la Mugirango Kaskazini, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanywa na wabunge wanaoshirikiana na serikali ya Kenya Kwanza, Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Japheth Nyakundi aliwataka MCAs wa Nyamira kumbandua Nyaribo mamlakani, tena kwa kukataa mwaliko wa Rais.

“Mna mamlaka ya kumwondoa mtu huyo ofisini na kumwacha naibu wake achukue wadhifa huo. Gavana Arati amekubali kupeleka MCAs Ikulu lakini wenu amekataa. Mbandueni,” Bw Nyakundi alisema huku akimwita Nyaribo majina mengine ambayo hayawezi kuchapishika.

Gavana Nyaribo ndiye kiongozi wa chama cha United Progressive Alliance (UPA), ambacho kinahusishwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i.

Waziri huyo wa zamani ametangaza nia yake ya kuwania urais mwaka 2027.

Ingawa mkutano wao wa Mugirango Kaskazini uliitwa mkutano wa kukagua baadhi ya miradi katika eneo bunge hilo, wale waliozungumza walimshambulia vikali Dkt Matiang’i na wale wanaoipinga serikali jumuishi na pana kama anavyoiita Ruto.

Akimjibu Bw Nyakundi, Gavana Nyaribo alimtaka Bw Nyakundi na washirika wake kutoka Kisii kumkoma na badala yake kuzingatia masuala ya kaunti yao.

Bw Nyaribo aliwataka wabunge hao vijana kuheshimu uamuzi wake hata kama hawampendi.

Alisema alichaguliwa na wananchi wa Nyamira na hatatetereshwa na siasa zao za pesa nane.

“Nilichaguliwa na watu wa Nyamira. Wacha washughulike na Gavana Arati. Ikiwa hawawezi kukabiliana naye, hawapaswi kunithubutu,” Gavana Nyaribo alimjibu Nyakundi.

Katikati ya mwezi uliopita, wabunge Nyakundi, Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Zaheer Jhanda (Nyaribari Chache) na Alfa Miruka (Bomachoge Chache) waliongoza sehemu ya wakazi kutoka kaunti za kisii na Nyamira hadi ikulu ambapo pia walidai kuwa wanakwenda kutafuta maendeleo mapya na kufufua yaliyokwama.

Mbunge wa Mugirango Magharibi Steve Mogaka, Mwakilishi wa Kisii Dorice Aburi na mwenzake wa Nyamira Jerusha Momanyi pia walihudhuria.

Hata hivyo, wanaopinga ziara hiyo wanadai kuwa mkutano huo hauhusu kufungua miradi iliyokwama bali yote ni kuhusu siasa na njia za kumkata mabawa Dkt Matiang’i ambaye ana uungwaji mkubwa wa kisiasa Gusii.

Kevin Moseti, mkazi wa Mji wa Kisii anaamini kuwa Rais si mwaminifu katika kuwaalika MCAs wa Gusii Ikulu. Bw Moseti anadai kuwa ziara hiyo inahusu kupanga mikakati ya jinsi wanavyoweza kupunguza ushawishi unaokua wa Dkt Matiang’i.

“Hakuna maendeleo ambayo watakwamua. Watu wa Gusii, kama Wakenya wengine wanastahili maendeleo bila ya kuabudu mtu kwa sababu wanalipa ushuru. Kwa nini rais anafanya mialiko ya mara kwa mara kwa watu kutoka eneo hili kumtembelea Ikulu? Kwa nini hakufanya hivyo wakati Dkt Matiang’i hakuwa ametangaza nia yake ya kuwania kiti cha urais ikiwa kweli alikuwa mkweli?” Bw Moseti aliuliza.

Aliwalaumu MCAs hao kwa kukubali mwaliko huo, akionya kwamba jamii itawaadhibu vikali debeni.

“MCAs hao hao ndio wamekuwa wakikutana na Dkt Matiang’i. Wanapaswa kuwa na msimamo mmoja, vinginevyo wana hatari ya kukabiliwa na ghadhabu ya wapiga kura katika kura,” Bw Moseti aliongeza.