MakalaSiasa

MATIBA: Viongozi wasifu ushujaa wa 'Baba wa demokrasia nchini'

April 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

VIONGOZI mbalimbali nchini wamemiminia sifa tele mwanasiasa mkongwe Kenneth Stanley Njindo Matiba huku wakimtaja kuwa ‘Baba’ wa demokrasia na mfumo wa vyama vingi.

Matiba Jumapili katika hospitali ya Karen, Nairobi huku akiwa na umri wa miaka 85.

Katika rambirambi zake Rais Uhuru Kenyatta alimtaja Matiba kama mzalendo halisi aliyejitolea mhanga kupigania demokrasia.

“Mzee Matiba alikuwa miongoni mwa wana wa Kenya walioweka misingi ya taifa hili. Alitumikia taifa hili kwa uadilifu tangu alipokuwa mwalimu katika shule ya Upili ya Kangaru na hata alipokuwa waziri na mtetezi wa demokrasia,” akasema Rais Kenyatta alipokuwa akihutubia taifa kutoka Ikulu, Jumapili usiku.

“Kwa niaba ya familia yetu, Bi Margaret na mimi tunatuma risala zetu za pole kwa Bi Edith Matiba na familia yake kwa kumpoteza Mzee Kenneth Matiba,” akaongezea.

Naibu wa Rais William Ruto alimtaja Bw Matiba kama mtetezi wa wanyonge na shujaa aliyepigania mageuzi na demokrasia.

“Bidii yake katika kupigania uhuru wa kujieleza, demokrasia ilimfanya kuzuiliwa kikatili. Alipendwa katika eneobunge la Kiharu na eneo zima la Muranga kwa kuwa aliwatumikia kwa kujitolea na uadilifu,” akasema Bw Ruto.

Jaji Mkuu David Maraga alimtaja Bw Matiba kama mwanasiasa shupavu aliyetumikia taifa kwa kujitolea.

 

Kielelezo

“Japo Mzee Matiba ametuacha, maisha yake yataendelea kuwa kielelezo kwa familia yake na Wakenya wote waliomfahamu. Tunashukuru Mungu kwa kutupatia Mzee Matiba kuwa nasi kwa kipindi hicho hadi alipotuacha,” akasema Jaji Mkuu.

Kinara wa Upinzani Raila Odinga alisema Mzee Matiba alikuwa shujaa na nembo ya ukombozi wa nchi hii.

“Kenya imepoteza nembo ya mwisho ya mwisho ya maumivu yaliyotokana na harakati za kupigania ukombozi na demokrasia. Matiba alijitolea mhanga kuhakikisha kuwa Wakenya wanakuwa na maisha bora na demokrasia ya kudumu,” akasema Bw Odinga.

Viongozi wengine waliotuma risala zao za rambirambi ni Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavad, Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria kati ya wengineo wengi.

Matiba alikuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Kangaru, Embu baada ya kukamilisha masomo yake katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda mnamo 1960.

Kati ya 1961 na 1962 Bw Matiba alihudumu kama Naibu Afisa wa elimu ya juu katika wizara ya Elimu.

 

Katibu wa kwanza

Mnamo Mei 18, 1963, Bw Matiba aliyekuwa na umri wa miaka 31 aliitwa katika afisi ya waziri wa Elimu katika serikali ya wakoloni, David Gregg. Bw Matiba aliteuliwa kuwa Katibu wa wizara siku hiyo, kulingana na tawasifu yake, Aiming High.

Bw Matiba alikuwa katibu wa wizarawa kwanza mweusi na jukumu lake kuu lilikuwa kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inaambatana na maadili na matakwa ya Kiafrika.

“Wanafunzi wote waliotaka kwenda kusomea ughaibuni walilazimika kupata saini yangu katika paspoti zao kabla ya kusafiri,” akasema Bw Matiba.

Wadhifa huo ulimwezesha Bw Matiba kukutana na idadi kubwa ya wanafunzi ambao baadaye walikuwa maafisa wenye ushawishi katika serikali ya Mzee Jomo Kenyatta.

Baadaye aliteuliwa kuwa Katibu wa Wizara ya Masuala ya Ndani ambapo aliweza kufanya kazi na Daniel arap Moi aliyekuwa waziri. (Rais Mstaafu) Moi alikuwa rafiki wa karibu wa Bw Matiba.

Alipokuwa waziri wa Ujenzi, Bw Matiba alifanikiwa kukwea safu ya Milima Himalayas iliyoko barani Asia. Aliweza kusimamisha bendera ya Kenya katika kilele cha mlima wa Island Peak ulioko Nepal na alikuwa Mkenya wa kwanza kufanya hivyo.

Aliwahi kutembea kutoka jijini Nairobi hadi Murang’a akichangisha fedha, hatua iliyomfanya kujizolea sifa tele.

 

Mfugaji

Kabla ya kujiunga na siasa Bw Matiba pia alikuwa mkulima na mfugaji wa nguruwe mtajika katika eneo la Limuru.

Biashara ya nguruwe iliporomoka baada ya mmoja wa wafanyakazi wake kuwalisha chakula kingi na kuwafanya kuwa wanono kupindukia hivyo akawauza wote kwa bei ya chini.

Baadaye, Matiba alianzisha shirika la safari za ndege, African International Airways.

Matiba pia aliwekeza katika sekta za elimu, hoteli na alikuwa miongoni mwa mamilionea wachache humu nchini huku akiwa na umri wa miaka 48.

Mnamo 1988, alijiuzulu kutoka serikalini baada ya kutofautiana na serikali ya Rais ya Moi kuhusiana na uchaguzi wa viongozi wa Kanu katika eneo la nyumbani, Murang’a.

Akiwa na Charles Rubia ambaye pia alikuwa amejiuzulu kutoka serikalini, alijiunga na wanaharakati wa kupigania mfumo wa vyama vingi kama vile Jaramogi Oginga Odinga na vuguvugu la vijana lililojulikana kama ‘Young Turks’.

 

Kiharusi korokoroni

Kabla ya maandamano ya Julai 7, 1990 yaliyojulikana kama Saba Saba, Bw Matiba alikamatwa na kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani hadi 1991. Aliachiliwa huru baada ya kuugua maradhi ya kiharusi.

Mfumo wa vyama vingi ulipoanza Matiba alijiunga na chama cha Ford kilichojumuisha viongozi wa upinzani kama vile Jaramogi Oginga Odinga. Makamu wa Rais wa zamani na Waziri wa Afya Mwai Kibaki alijiuzulu kutoka serikalini na kubuni chama chaDemocratic Party (DP) kabla ya uchaguzi mkuu wa 1992.

Mvutano baina ya Matiba na Odinga kuhusiana na mwaniaji wa urais, chama cha Ford kilisambaratika na kuwa Ford-Asili cha Matiba na Ford-Kenya chake Odinga.

Rais Moi aliibuka mshindi kwa kura 1.9 milioni, Matiba kura 1.4 milioni, Bw Kibaki 1.05 milioni na Odinga akapata kura 0.94 milioni.

Matiba alimtoa kijasho Rais Moi, Kibaki na Odinga licha ya afya yake kuzorota.

Mwaka 2017, Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola aliagiza serikali kumlipa Mzee Matiba kitita cha Sh945 milioni kwa kumtesa na kumzuilia kikatili katika gereza la Kamiti.