Makala

Matineja waepuke matumizi ya dijitali usiku

Na  BENSON MATHEKA July 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMA wewe ni mzazi wa tineja, tayari unafahamu kuwa mwanao wa kiume au wa kike hutumia saa nyingi kila siku akiwa amezingirwa na vifaa vya kiteknolojia.

Unachoweza kuwa hukifahamu ni kwamba michezo ya video inayochezwa kwa muda mrefu na mazungumzo ya mara kwa mara mtandaoni vinaweza kuathiri uwezo wake kupata usingizi mzuri usiku.

Kwa mujibu wa watafiti kutoka Kitengo cha Afya ya Vijana na Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), vijana wanaotumia saa mbili au zaidi kwa siku kwa kompyuta au kucheza michezo ya video kwa madhumuni yasiyo ya masomo wana uwezekano mdogo wa kupata usingizi wa kutosha ikilinganishwa na wenzao wasiopendelea teknolojia sana.

Aidha, wanafunzi wa shule ya upili wanaofanya mazoezi ya mwili kila siku wana nafasi kubwa ya kupata usingizi mzuri wa usiku kuliko wale wasiofanya mazoezi mara kwa mara.

Matokeo haya yalichapishwa katika jarida la American Journal of Preventive Medicine, baada ya uchunguzi wa kitaifa uliowahusisha zaidi ya vijana 15,000.Wataalamu wanashauri kuwa mwanafunzi wa shule ya upili anahitaji kati ya saa 8 hadi 9 na nusu za usingizi kila usiku. Hata hivyo, vijana wengi hulala saa 5 hadi 6 au hata chini ya hapo.

Katika kipindi cha utineja, melatonini—homoni inayozalishwa katika ubongo—huzalishwa kwa kuchelewa zaidi usiku ikilinganishwa na wakati wa utoto. Hali hii huathiri mzunguko wa jinsi mwili unavyojiendesha na kuchelewesha muda wa kijana kuhisi usingizi.Usingizi hutoa manufaa muhimu kwa watu wa rika zote.

Kwa matineja, ukosefu wa usingizi unaweza kusababisha matatizo ya kusoma shuleni, kudhoofika kwa kinga ya mwili, hasira zisizoeleweka, na hata msongo wa mawazo.

Huwezi kumlazimisha kijana wako ahisi usingizi kabla hajawa tayari, lakini unaweza kuongeza nafasi yake kupata usingizi mzuri kuweka mipaka ya matumizi ya vifaa vya dijitali.

“ Ingawa matineja na teknolojia ni kama ndugu, ni muhimu kuweka mipaka ya busara inayofaa familia yako. Zungumza na mwanao kuhusu mipaka hiyo na eleza kwa nini ni muhimu kwa afya na ustawi wake. Hakuna haja ya kuacha teknolojia kabisa—tafuta uwiano bora kati ya muda wa kuitumia na shughuli nyingine,” asema, Dkt Debbie Glasser, mtaalam na mtafiti wa malezi dijitali.

Vijana wengi, asema, wana kifaa kimoja au zaidi cha kielektroniki katika chumba chao cha kulala. Wengine wana hadi vinne au zaidi. Vifaa hivi vinaweza kuvuruga usingizi. Hamisha baadhi ya vifaa hivyo hadi chumba kingine ili chumba cha kulala kibaki kuwa mahali pa usingizi, si matumizi ya teknolojia.