Matumaini kwa biashara ndogo mashirika ya kifedha yakitoa mamilioni
KUNA matumaini kwa wanaoendesha biashara ndogo nchini huku mashirika ya kifedha yakianzisha bidhaa zinazowalenga.
Bidhaa hizo zinanuiwa biashara kuongeza mtaji kwa upanuzi na kuendelea kupata faida huku zikiongeza nafasi za ajira.
Kupitia mpango kama huu, benki ya ABSA Kenya, imetenga Sh100 bilioni katika miaka mitatu ijayo kwa ufadhili wa Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs) ili kusaidia kukuza biashara hizi nchini.
Kulingana na Mkuu wa Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs) wa Benki ya ABSA Kenya Erastus Muthura, ufadhili huo unalenga sekta za elimu, kilimo, afya, viwanda na biashara.Bw Muthura alisema, shirika lake litatoa mafunzo na kuwajengea uwezo wafanyabiashara 50,000 ili waweze kupanua biashara zao.
‘Watakuwa na uwezo wa kurekebisha biashara zao na kuwa na mifumo ya kuwasaidia kukabiliana na mabadiliko ya mahitaji katika soko na mazingira ya kiuchumi,’ alisema.
Alisisitiza umuhimu wa biashara ndogo kwa uchumi wa nchi, akisema mchango wao katika kubuni ajira hauwezi kupuuzwa.
‘Tunachohitaji kufanya ni kuwafunza wafanyabiashara na wanawake kuelewa mahitaji na mienendo ya soko na kuweza kukidhi mahitaji haya yanayoibuka,” alisema Bw Muthura na kuongeza kuwa mienendo ya masoko inabadilika kila siku kadri mahitaji ya mteja yanavyobadilika.
Afisa huyo alisema kuna umuhimu wa kuwa na sera za bima nchini ambazo zinaweza kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, upatikanaji wa fedha kwa biashara miongoni mwa masuala mengine na benki yake inakusudia kufanya hivyo kwa kuwaleta wadau wote kwenye mazungumzo ya kuboresha mazingira.
Kutokana na changamoto zinazojitokeza kuwakumba wafanyabiashara, alisema, wateja wao wanaopata matatizo katika kulipa mikopo yao wanaweza kwenda katika benki ili kujadili suala hilo na kuongeza kuwa kila biashara ina changamoto za kipekee.
ABSA, iliundwa mwaka wa 1991 na imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Johannesburg (JSE) nchini Afrika Kusini na ni mojawapo ya mashirika makubwa zaidi ya huduma za kifedha barani Afrika na inapatikana katika nchi 12 barani kote.