Matumaini ya wakulima yafifia mageuzi ya kufufua sekta ya kahawa yakigonga mwamba
HUKU Rais William Ruto akitoa hotuba yake kwa taifa bungeni Alhamisi, Novemba 21, 2024, wakazi eneo la Mlima Kenya hawana furaha, kwa kuwa tegemeo lao kuu la kiuchumi liko katika hali duni.
Walikuwa na matumaini makubwa kufuatia kuingia madarakani kwa serikali ya Kenya Kwanza ambayo ilikuwa imeahidi kuimarisha sekta ya kahawa.
Hata hivyo, matumaini yanaonekana kufifia haraka huku mageuzi katika sekta ya kahawa yaliyoanzishwa punde tu baada ya serikali ya Kenya Kwanza kuchukua mamlaka kukosa kuzaa matunda.
Kufufuliwa kwa sekta ya kahawa ilikuwa ahadi kuu ya kampeni ya Rais Ruto na mgombea mwenza wake wakati huo, Rigathi Gachagua na punde tu baada ya kuchukua mamlaka zaidi ya miaka miwili iliyopita, Rais alimpa naibu wake ambaye sasa ametimuliwa afisini, jukumu la kusimamia mageuzi hayo katika sekta ndogo za chai na maziwa.
Mnamo 2023, Bw Gachagua aliitisha kongamano la siku tatu la wadau kuhusu mageuzi ya kahawa katika Kaunti ya Meru ili kujadili vikwazo vinavyozuia maendeleo ya sekta hiyo ndogo.
Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kujadili mapendekezo ya kuendeleza na kuboresha kilimo cha zao hilo.
Hata hivyo, matukio ya hivi majuzi katika eneo lote, yanaashiria kwamba mageuzi yanayotarajiwa bado hayajafaulu.
Wakulima wanalalamikia malipo duni, kucheleweshwa kwa malipo na makato yasiyoelezeka kutoka kwa malipo yao au wizi wa moja kwa moja wa mapato yao na wasimamizi wa vyama vyao.
Kwa mfano, ripoti ya hivi majuzi ya ukaguzi wa kamishna wa vyama vya ushirika wiki moja iliyopita ilifichua kuwa chama cha wakulima 7,000 cha Baricho, eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri, kina deni la Sh300 milioni.
Wakulima wa Nyeri, Kirinyaga, Meru na Murang’a, maeneo ambayo yana wakulima wadogo wa kahawa, wanachama wa vyama wamegeukia maandamano kuelezea malalamishi yao kutokana na kupungua kwa mapato ya zao hilo.
Benson Karanja, mwanachama wa chama cha Kahawa kutoka Mathira Kaskazini kinacholeta pamoja wakulima kutoka Kiamariga, Kabiruini, Kahiraini na Hiriga na ambacho kiliporomoka takriban miaka miwili iliyopita, anasema wakulima wamesikitishwa na kushindwa kwa serikali kutimiza ahadi ya kufufua chama chao.
“Tulikuwa na matumaini. Walituambia wakati wa kampeni kwamba walikuwa na mpango kutuhusu, lakini kwa hali ilivyo sasa tumekata tamaa na inaonekana hakuna matumaini,” alisema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA