Makala

Mauaji: Yafichuka mama alikanya bintiye kuhusu mpenziwe GSU

Na KALUME KAZUNGU May 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA ya mwanamke aliyeuawa pamoja na mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano katika Kaunti ya Lamu imefichua kuwa, alishauriwa kuwazia upya uhusiano wake na afisa wa kitengo cha GSU aliyetekeleza mauaji hayo kabla ya kujitoa uhai.

Imebainika kuwa, afisa huyo aliyewapiga risasi na kuua mama na mtoto wake wa miaka mitano na kisha kujitoa uhai mjini Mokowe, Kaunti ya Lamu mnamo Jumapili hakuwa mume bali mpenzi wa mwanamke huyo.

Imesemekana mwendazake, Sheila Nyamokami Mokaya, 32, alifaa kumtambulisha afisa huyo rasmi nyumbani kwao mnamo Desemba kama mchumba wake wanayepanga kuoana.

Mamake marehemu, Bi Teresia Gethemba Mose, alieleza masikitiko yake kwamba bintiye na mjukuu wake, Lency Amelia, waliuawa na mwanamume ambaye hata hatambuliwi nyumbani.

Kulingana na Bi Mose, bintiye, ambaye pia ni kifungua mimba katika familia ya watoto watano hakuwa ameolewa baada ya ndoa yake ya kwanza kusambaratika.

Sheila Nyamokami Mokaya aliyeuawa na GSU Jumapili, Mei 11, 2025 mjini Mokowe, Lamu. Picha|Familia

Sheila ni mama wa watoto wawili, wa kwanza ambaye ni mvulana akiwa na umri wa miaka 12 huku wa pili akiwa ni msichana ambaye aliuawa pamoja.

Bi Mose alifafanua kuwa, msichana wake alipata mtoto wake wa kwanza alipokuwa akisoma chuo kikuu cha Kisii mwaka wa 2013.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya ualimu, Sheila alirudi nyumbani kwao Chirichiro eneobunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii na kujaribu kuolewa katika eneo la karibu.

“Baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu, binti yangu aliolewa eneo jirani la Keumbu. Baada ya kuzaa mtoto wake wa pili msichana, alishindwa kukaa. Alibeba virago na kuja nyumbani. Ndoa ikakatika hivyo,” akaeleza Bi Mose.

Alifanya juhudi za kujitafutia kibarua, ambapo alifaulu kupata kazi ya kufunza, japo katika hali ya kibarua katika Shule ya Msingi na Sekondari Msingi ya Mkunguni, iliyo Mokowe, Kaunti ya Lamu.

“Alifanya kazi huko kwa miaka miwili mfululizo kabla ya kutuma maombi ya kazi rasmi kwa serikali. Alifaulu kuajiriwa kwa mpango wa kudumu mnamo Januari 2025,” akasema Bi Mose.

Anasema bintiye alipokuja nyumbani kwa ajili ya likizo ya Aprili, alimdokezea kuhusu uhusiano wake na afisa wa GSU na mipango waliyokuwa nayo ya kumleta nyumbani ili ajulikane rasmi.

Bi Mose anasema alimuonya bintiye kuwa mwangalifu na kumkagua afisa huyo kwanza kujua endapo alikuwa mkweli alitaka kumuoa au la.
Anasema alipokea taarifa za kifo cha binti na mjukuu wake kwa mshtuko.

“Kwa nini GSU aniulie watu wangu kinyama hivyo? Sisi hatumtambui. Hakuwa mume wa Sheila ila rafiki tu. Hata mipango ya kumtambulisha nyumbani Desemba ilifaa kutegemea vipi wangepelekana kimahusiano kwanza. Ninaumia,” akasema Bi Mose.

Aliiomba serikali kuingilia kati na kutafuta haki ya bintiye na mjukuu wake akimtaja Sheila kuwa tegemeo la pekee kwa familia yake.

Kwingineko, polisi wamefichua jina la afisa wa GSU aliyetekeleza mauaji ya Jumapili mjini Mokowe.

Afisa huyo, Moses Makira Ayoga, 31, alitambuliwa kuwa afisa mwenye bidii na mcha Mungu ambaye hakutarajiwa kwamba angetekeleza mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Bw Kipsang Changach anasema mbali na kuhubiria wenzake ndani ya kambi ya GSU Mokowe, Makira pia alikuwa dereva wa lori la kumimina maji kambini aliyefanya kazi yake kwa bidii.

Jamii ya Mokowe pia ilimtambua afisa huyo kuwa mtu mwema na kushangaa kuhusu kitendo chake.