MAWAIDHA YA KIISLAMU: Chumo la haramu ni miongoni mwa madhambi yaliyozagaa katika jamii
Na HAWA ALI
SIFA zote njema anastahiki Mungu Azzawajalla, swala na salamu zimwendee Mtume Mtukufu Swallallahu A’alayhi Wasallam.
Amesema Allah Subhanahu wataala “Hakika mali zenu na watoto wenu ni fitna” (Taghaabun 15)
Mali ni fitna kwani ni kama upanga wenye ncha mbili, ambao ima itamnufaisha mtu au kumuangamiza.; ima aichume katika njia za halali imnufaishe duniani na akhera, au aichume kwa njia za haramu imnufaishe duniani na kumuangamiza akhera, Mtume rehma na amani ziwe juu yake ametuambia kua kila mtu ataulizwa mambo manne siku ya kiama na akataja moja ni mali vipi kaichuma na vipi kaitumia, hivyo mali itakua na maswali mawili tofauti na mambo mengine yenye swali moja kwa kila jambo.
Uislamu haukatazi mtu kuwa na mali nyingi maadamu kazichuma katika njia za halali na anazitumia zinavostahiki, kwani historia imewataja baadhi ya waja wema walokuwa matajiri na namna gani walivozitumia mali zao katika kumridhisha Mola wao, tukianzia maswahaba akina Sayyidina Uthmaan, Abdul-Rahmaan bin Auf na maswahaba wengineo na wema walokuja baada ya hapo radhiallahu anhum ajmain.
Amesema Mtume rehma na amani ziwe juu yake: “Ni mali bora ilioje ilokua nzuri inayomilikiwa na mtu mzuri” inaonesha kua mtu mwema anapomiliki mali basi ata mali yake hua nzuri kwani hutolewa na kutumiwa katika njia anazozipenda Allah subhaanah.
Lakini pia uislamu umekataza kuchuma mali kwa njia za haramu. Umekataza kuchuma mali kwa mambo aliyoyaharamisha Allah subhaanahu wataala: Tunaona tamaa za watu za kutaka kutajirika kwa haraka, wanatumia njia ambazo Allah ameharamisha, toka asili ya kile kitu seuze biashara yake. Na tutazame mifano michache:
1. Allah subhanahu wataala amekataza ULEVI, hivyo hata biashara yake haifai, tunaona katika hadithi ya Mtume Rehma na amani ziwe juu yake watu kumi wanaohusu ulevi wamelaaniwa. Toka muuzaji mpaka mkokoteni ulobeba pombe pia umelaaniwa. Ni vijana wangapi tunaoishi nao washalaaniwa? Vijana wangapi walojazana katika mahoteli yanayouzwa ulevi na wao kushiriki katika biashara hiyo?
2. Allah subhanahu wataala amekataza RIBA, lakini tunaona inavyochotwa katika benki na kwingineko mpaka kupambiwa majina ili ionekane kuwa ni halali. Tumeona kuwa kilichoharamisha sheria ni haramu na riba ni haramu katika kitabu na Sunnah, amesema Allah “Na Allah amehalalisha biashara na kuharamisha riba” Baqarah 275, na kuna hadithi nyingi zinazoonesha ukubwa wa dhambi ya riba ikiwemo riba kuwa miongoni mwa madhambi saba yenye kuangamiza na ile hadithi ya Mtume kuwa riba ina milango 70; wa chini yao ni mfano wa mtu kuzini na mamake.
3. Tumekatazwa kula RUSHWA. Tunaona swala la rushwa liko kila kona, sio wanasiasa wanaokemea rushwa, uislamu umetangulia kuikemea rushwa na kuonesha kua Mtoaji, mpokeaji na anaeshuhudia wote wamelaaniwa. Imekua haki yako huipati mpaka utoe rushwa yani laana za Allah zimejaa kila kona kiasi cha kutukosesha barka katika miji yetu.
4. Allah subhanahu wataala amekataza kula MALI YA YATIMA lakini wangapi wanafika hadi kupora haswaa mali za mayatima,wamesahau maneno ya Allah aliposema: “Hakika ya wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma hakika wanakula moto katika matumbo yao…” (Nisai 10 ) Tayari washatia moto katika matumbo yao toka duniani kabla ya kufika Akhera. (Allah atuhifadhi).
5. Allah subhanahu wataala amekataza MUZIKI, hivyo biashara yake pia ni haramu kama alivosema Mtume rehma na amani ziwe juu yake: kuwa biashara yake haina faida, wala thamani, lakini ni vijana wangapi wanashiriki kutoa, kuuza na kusambaza CD na mengineyo yanayohusu muziki?
6. Allah subhanahu wataala amekataza UZINIFU; hivyo kila kinachohusu na kupeleka uzinifu ni haramu, kwani tumekatazwa hata kuikaribia zinaa, lakini vijana wangapi wanafanya kazi kwenye sehemu zenye kuchochea zinaa au kushiriki katika uuzaji wa vitu vyenye kuchochea uzinifu, haya yote ni haramu na mwenye kusaidia kufanya jambo baya basi na yeye atapata malipo sawa na mfanyaji pasi na kupunguziwa yeyote chochote.
7. Allah subhanahu wataala amekataza SHIRKI, ni vijana wangapi wanatafuta utajiri kwa njia za kishirikina, na kufikia sasa wanauwaua wenzao kwa sababu ya mali? Yani ni haramu juu ya haramu. Tutaenda kumjibu nini Allah subhanahu wataala atakapotuuliza kuhusina na mali namna tulivoichuma na kuitumia? Mifano ya njia za haramu iko mingi ambayo imeenea katika jamii.
Tunaona migogoro ya ardhi na watu kupora ardhi si zao, na baadae kudai zao ili waziuze,na wanufaike nazo, ni makosa mtu kuzidisha shubiri moja tu ya ardhi isiyo yake seuze kupora ardhi au ma ekari kwa ekari.
Ndugu zangu wa Kiislamu, Mtume rehma na amani ziwe juu yake ametuonya pale aliposema katika hadithi ya Abdullah bin Mas-uud na kupokewa na Bukhari na Imam Ahmad rahimahumallah “ Hatochuma mja mali ya haramu kisha akaitoa (kwa kuitumia) Allah akambarikia, wala hatoitolea sadaka Allah akamkubalia, wala hatoiwacha nyuma yake (baada ya kufa) isipokuwa itakua ni akiba yake ya kumpeleka motoni. Subhnallah!
Mali ya haramu haina manufaa yoyote si katika kuitumia kulisha familia au kujilisha mtu mwenyewe, wala si katika kuitolea sadaka, na ukiiwacha pia ni mashaka. Allah atuhifadhi.