• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Je, mafuriko haya yanatufunza nini sisi waumini?

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Je, mafuriko haya yanatufunza nini sisi waumini?

NA ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogondogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii tukufu, bora na aula kuambizana, kukumbushana na kusemezana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote tuchukue uzito wa nafasi hii katika utangulizi huu kumshukuru, kumpwekesha na kumumiminia sifa kedekede kwake Muumba wetu, Allah (SWT).

Ni yeye pekee ndiye aliyeumba ardhi na mbingu na vyote vilivyomo. Hakuna Mola mwingine anayepaswa kuabudiwa na kuenziwa ela ni yeye mmoja pekee: Allah (SWT).

Ama katika usanjari uo huo, tunamtilia dua na kumfanyia maombi mwombezi wetu naye Mtume (SAW).

Leo hii ndugu yangu tunapitia kipindi kigumu mno. Kupitia kwa maana ya sisi nchini Kenya, Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa jumla. Tunapitia misukosuko, ndaro na mitihani chungu nzima! Sasa hivi tumeshuhudia mvua kubwa mno! Sisi waja tuliomba mvua. Lakini si gharika hili.

Ipo video moja imekuwa ikisambaa mitandaoni ambapo Shekhe mmoja anasema kuwa mvua kubwa kiasi hiki anaiona kama maapizo na laana!

Baadhi ya watu wanadai kuwa mara ya mwisho kumeshuhudiwa mvua kubwa kiasi hiki ni mwaka wa 1961! Zimenyesha mvua! Zikaja na El-nino! Zikapiga hata aina nyinginezo kali za pepo na vimbunga.

Lakini hii mvua iliyoshuhudiwa, na ingali inashuhudiwa nchini, ni kali mno, ni kubwa mno ni ya aina yake. Watu kadha wameaga dunia. Majengo yamebomolewa. Mifugo imesombwa. Shule zimegeuzwa mahame. Nyumba zimelowa maji na kufurika si haba! Picha ambazo zinashuhudiwa kila kona ni za kusikitisha mno! Video ambazo zipo kwenye runinga na mitandaoni ni za kuatua mioyo.

Kwa hakika waja wanapitia kipindi kigumu sana! Ajali zimeshuhudiwa kila kona. Watu na magari yao wanasombwa kila kona. Kijiji kizima kinasombwa hasa!

Mkasa wa eneo la Mai-Mahiu na maeneo mengineyo, ni mkasa wa kuogofya sana!

Eneo lililoathirika na mafuriko Mai Mahiu. PICHA | MAKTABA

Je, alivyosema Shekhe kuwa hii ni adhabu ni ukweli? Au ni mjadala wa siku nyingine? Siku zote sisi huomba mvua. Lakini tunasahau kuomba ni mvua za aina gani. Mvua ambazo zimesitisha kila shughuli. Biashara zimekwama. Nyingine kusitishwa.

Shule kuahirishwa kufunguliwa, japo sasa serikali ilisema zitafunguliwa wiki ijayo. Lakini yote hayo ni kwa majaaliwa yake Mwenyezi Mungu.

Ya Rabi utuonee imani na huruma. Sisi waja wako hatuna uwezo wala nguvu. Zilianza vema mvua za kheri.
Wakulima wengi wakapinda migongo na kulima kweli kweli! Kufumba na kufumbua, kudura zake Mwenyezi Mungu, kukatokea ya kutokea. Mvua kubwa. Mafuriko. Yakasombwa ya kusombwa ikiwemo mimea. Kwa hakika mazao sasa yamekuwa ni uozo.

Wakulima wanakadiria hasara ya mamilioni. Waliokuwa wamevuna hawawezi kusafirisha bidhaa zao hadi masokoni. Je, huu mtihani wa mafuriko unatufunza nini sisi waja-waumini? Inafaa tukae chini, kitako, na kutafakari kwa kina. Hali haitabiriki. Ndivyo yalivyo maisha. Hayatabiriki. Yote ni majaaliwa yake Mwenyezi Mungu, au siyo?

Ijumaa Mubarak!

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wakulima walia mgao wa mbolea nafuu ukipunguzwa

Wanamazingira wataka kupanda miti kuwe ni mazoea, si...

T L