MAWAIDHA YA KIISLAMU: Katika maisha ya leo yatubidi tuwe na subira kama alivyofanya Mtume
Na HAWA ALI
WANADAMU ni wenye tabia tofauti.
Wapo ambao kwa maelezo na muongozo mdogo wanaelewa ukweli wa mambo.
Wengine ni wenye kuleta ubishi lakini wanapopata hoja nzito hukubali ukweli.
Lakini wapo ambao wanapata maelezo ya kina kabisa na bado wanashikilia misimamo na tabia zao hata kama sio sahihi katika misingi ya Kiislamu. Hili ndio kundi ambalo daima hugongana na waja wema.
Katika ulimwengu wa leo ambao umejaa shughuli aina wa aina.
Hata mtoto mchanga anapozaliwa huwa na harakati zake, vivyo hivyo kwa mwendawazimu.
Ni dunia ambayo imejengeka kwa khulqa za “chako chako na changu changu”, au kwa kimombo tuseme “mind your own business.”
Hapo ndipo kunapotokezea kivumbi kwa yule anayekosolewa. Bila ya shaka mja mwema hatapendelea kumuona ndugu yake akiwa anatumbukia kwenye maasi kichwa na miguu.
Atafanya kila hali alimuradi apate kumuwaadhi aachane nayo. Ndipo misukosuko kadhaa wa kadhaa itamkuta mja mwema mwenye kuwapatia nasaha za kweli na zilizo sahihi ndugu zake waliovuka mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).
Tukumbuke kwamba Muislamu wa kweli ni yule anayeshikamana na mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akafanya mambo kwa ajili ya Muumba wake na sio kuridhisha wanaadamu. Hivyo, tabu yoyote atakayoipata kutokana na walimwengu basi ni lazima aelewe kwamba ina malipo makubwa mbele ya Mola Mlezi.
Wala hakuna mafanikio mema hapa duniani kuliko subira. Subira ambayo Muislamu anatakiwa kuyastahamilia hayo maudhi anayoyapata kutoka kwa wanaadamu wanaomsumbua kila kukicha. Na sababu kubwa ni kwamba yeye ameshikamana na kamba ya Uislamu.
Turudie yale maneno ambayo Bwana Luqmaan alimwambia mwanawe ashikamane na subira kutokana na yanayomsibu:
{{Ewe mwanangu! Shika Swalah, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayokupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa}} [Luqmaan: 17]
Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema kwamba tushikamane na kusubiri na kwa hakika Yeye Muumba yupo bega kwa bega pamoja na wenye kusubiri:
{{Enyi mlioamini! Takeni msaada kwa subira na Swalah. Hakika Allah Yu pamoja na wanaosubiri.}}[Al-Baqarah: 153]
Wapo baadhi ya walimwengu wanaopendelea wenzao wawe ni wenye kutenda maasi kama au kuliko wanavyofanza wao.
Wasipoendana na maasiyao hufanya kila jitihada kumpiga vita. Hapa ndipo vijana na wazee wanapotumbukia kwenye kutafuta wazinzi au vilabu vya pombe ili tu kuridhisha walimwengu.
Maudhi na kusumbuliwa sana na walimwengu kunahitajika uvumilivu wa hali ya juu kabisa. Kwani hali hiyo pia ilimkuta vile vile mbora wa walimwengu (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Naye alipata maudhi makubwa ya kutukanwa, kupigwa na kutengwa, na ndipo kila mara Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Alikuwa akimkumbusha kuwa si pekee mwenye kupata misukosuko ya walimwengu, bali Mitume wenzake pia wamepitia maudhi na Akimsimulia visa kadhaa vya Mitume katika Qur-aan ili ashikamane na subira.
Jambo kubwa linalohitajika kwa Muislamu ni kusubiri juu ya vitimbi anavyofanyiwa kutoka kwa walimwengu. Subira hii iendane sambamba na kutenda ‘amali njema na kuisaidia jamii yake kuachana na maovu. Kinyume cha subira mbele ya walimwengu ni hamaki. Katika hili Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametilia mkazo Muislamu kujizuia kuhamaki. Kuna mtu alitaka kuusiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamwambia:
“usihamaki” Yule mtu akakariri tena (ombi lake) mara nyingi, na akamwambia “(jizuie) usihamaki.” [Imesimuliwa na Abu Hurayrah na kupokelewa na Al-Bukhaariy]
Hadiyth ya hapo juu inatuonesha dhaahir kwamba hamaki ni yenye kuibomoa subira. Ni wajibu wetu kushikamana na subira bila ya kuchoka.
Tunakuomba yaa Jalaal, Subira Zako Zipo juu kuliko ghadhabu Zako, tughufurie madhambi yetu na tujaalie kuwa miongoni mwa wenye kushikamana na subira.