Mayonde adai kushindwa kuingiza pesa kimuziki ndio sababu ya ukimya wake
NA SINDA MATIKO
HIVI unamkumbuka Mayonde? Yule mrembo aliyetuangishia fataki nzito ‘Nairobi’ yapata miaka mitatu iliyopita.
Baada ya kuja kwa nguvu za soda na kufanya vizuri kwa muda kwenye chati za muziki hapa nyumbani, Mayonde aliingia gizani.
Sasa mrembo huyo ambaye anajipanga kurudi tena kwenye gemu, anakiri kuchoshwa na muziki baada ya kuona hakuwa akitengeneza faida yeyote.
Ndio, alipata umaarufu kweli kweli kupitia sanaa yake, ila kimfuko muziki huo haukuwa ukimuingizia senti zozote za maana.
Kwa kifupi, Mayonde alihisi kuendelea kufanya muziki, kulikuwa kunamletea hasara tu.
Lakini wikendi iliyopita, Mayonde alishangaza mashabiki waliohudhuria tamasha la Blankets & Wine baada ya kupiga shoo moja ya nguvu.
“Nina muda mrefu tangu nilipotumbuiza jukwaani, ilikuwa raha sana kurejea tena. Mwanzo kuna kipindi nilikuwa natumbuiza wimbo wangu wa Nairobi halafu hadhira ikawa nayo inaimba neno baada ya neno, jambo hilo lilinigusa sana. Ni tukio ambalo bado limenikaa kichwani,” anasema Mayonde.
Lakini amekuwa wapi?
“Nilipokuwa kimya, niliamua kurudi shule kusomea biashara ya muziki. Mimi ni miongoni mwa wale tuliokuwa kwenye mpango wa Perfom Music Incubator ulioasisiwa na mwaandaji wa Blankets & Wine, Muthoni The Drummer Queen.
“Kwenye mpango huo ambao nimekuwepo nao kwa miaka miwili sasa, pale ni skuli kabisa maana nimekuwa nikipokea mafunzo yanayohusiana na biashara ya muziki, namna ya kukuza brandi yangu, na kisha kuitumia kutengeneza pesa. Lakini hata zaidi kupata uelewa wa kina wa njia zingine za kutengeneza pesa kupitia muziki,” anafafanua.
Mayonde anakiri alikuwa ameshakwisha kata tamaa ya muziki kabla ya kujiunga na mpango huo.
“Nilikuwa nimechoka na usanii, kuwekeza kwenye sanaa lakini sitengenezi pesa kupitia sanaa yenyewe. Unawekeza fedha nyingi kwenye sanaa lakini fedha hizo hazirudi ndio sababu niliamua kurudi shule,” ameongeza.