• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mazao yaliyokuzwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimo hai yana mazao bora

Mazao yaliyokuzwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimo hai yana mazao bora

Na SAMMY WAWERU

KAMPUNI ya kilimo cha bukini ya SunBerry Berry Enterprise imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupenyeza mazao yake sokoni.

Matunda ya bukini yanaaminika kukua porini. Yanaorodheshwa katika familia moja na nyanya. Sawa na wakulima wengine, kampuni hii yenye shamba lake Kiambu na Nakuru, hutumia mitandao kufanya matangazo.

Upanzi wa matunda haya ulifanywa kwa mara ya kwanza Uropa kabla ya kuenea mataifa mengine ulimwenguni. Ni kutokana na faida zake kiafya na kimatibabu, SunBerry Berry Enterprise iliyakumbatia na kuyalima Kenya kwa wingi.

Safari iling’oa nanga 2016, kwa mtaji wa Sh2 milioni ambapo ilikodi ekari nne eneo la Kwa Mbiu, Tigoni, Kaunti ya Kiambu. Kufikia sasa, inayapanda kwa zaidi ya ekari 20 Kiambu na kiasi sawa na hicho Nakuru.

Waasisi wa kampuni hii ni; afisa mkuu mtendaji Esther McCarthy, Steven Mwanzia afisa msimamizi wa mikakati na utendakazi, mshauri wa masuala ya biashara Gerry McCarthy na Kevin Billing mshauri wa kiufundi.

“Kiambu tunayakuza kwa zaidi ya ekari 20, na tunaendelea kuyavuna. Nakuru pia tuna ekari zingine 20,” adokeza Bw Mwanzia.

Kilimo hai

Ikizingatiwa kuwa wengi wanaamini matunda haya ni ya porini, Bi Esther anasema SunBerry Berry imefanikisha kilimo chake kwa sababu ya kuzingatia mfumo wa kilimo hai (Organic farming).

Wataalamu wa kilimo wanahoji mimea yoyote ile ikikuzwa kwa kuzingatia mfumo huu, haimpi mkulima mazao bora na yenye faida pekee ila inaafikia malengo ya wateja.

“Bukini zetu tunazilima kwa kuzingatia mfumo wa kilimo hai. Hatutumii dawa zozote kukabili wadudu, magonjwa wala makwekwe. Ndiyo maana tumeweza kupenyeza sokoni na mazao yetu kuwa mithili ya mahamri moto,” anaeleza Esther, akiongeza kuwa wateja huyasifu kwa kuwa na ladha tamu.

“Yanayokua vichakani au msituni, hayana yeyote wa kuyatunza na yana ladha tamu. Ni muhimu kutaja bukini haziathiriwi na wadudu ama magonjwa ya mimea,” anasema.

Bw Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya kilimo hasa matunda anahimiza wakulima kuzingatia njia asili kukuza mimea.

Mdau huyu anasema wateja wamepevuka na wanataka mazao yasiyopandwa kwa kemikali.

“Tukikubali kuegemea kilimo hai kwa kila mimea, malalamishi ya ugonjwa kama Saratani yatapungua,” anahimiza.

Kutegemea mvua

Ili kuhakikisha kilimo hai kimetekelezwa kikamilifu, Bi Esther anadokeza kuwa Sun Berry Berry hutegemea mvua na kwamba haitumii mfumo wa kunyunyizia maji mashamba. “Matunda ya bukini yanahitaji maji kidogo sana kuyakuza,” akaambia Taifa Leo Digitali wakati wa mahojiano. Alionya kuwa hayafanyi vyema kwa kutumia maji ya chumvi.

Mwanzia, afisa msimamizi wa mikakati na utendakazi anasema ekari moja ina uwezo wa kuzalisha karibu tani nne, sawa na kilo 4,000.

“Bei yetu ni nafuu, kipimo cha gramu 200 tunauza Sh100,” afichua.

Bukini hukomaa na kuanza kuvunwa miezi sita baada ya upanzi.

“Yanavunwa miezi minne mfululizo,” aeleza Kevin Billing, mshauri wa kiufundi.

Wengi wa wateja wa SunBerry Berry ni wa kijumla, ingawa Gerry McCarthy ambaye ni mshauri wa masuala ya biashara anasema wana wachache wa rejareja. Kampuni hii ya kilimo imebuni nafasi za kazi kwa zaidi ya vijana 30.

Mtaalamu wa afya

Matunda ya bukini ni kiini kizuri cha Vitamini A, B na C, na hata Protini. Wangui Mirara, mtaalamu wa masuala ya afya anasema pia yamesheheni madini ya Potassium, Manganese, na Phosphorus.

“Yana Fiber, ambayo ni muhimu katika kushusha athari za ugonjwa wa Kisukari, Moyo na Mafuta mwilini. Madini ya Potassium hudhibiti presha ya damu na kusaidia ukuaji wa ubongo hasa kwa watoto,” afafanua Bi Wangui.

Bukini pia husaidia kukabiliana na gesi tumboni, haswa inaposokota. Mtaalamu huyu anakubaliana kwa kauli moja na SunBerry Berry Enterprise haja ya kukuza matunda kwa mfumo wa kilimo hai. Anasema mengi ya magonjwa ibuka yanasababishwa na chakula chenye kemikali.

“Magonjwa tunayoshuhudia yatadhibitiwa ikiwa tutazingatia kilimo asili ili mazao tunayopata yawe salama,” asisitiza.

You can share this post!

Droo ya voliboli yaepusha timu za Kenya kukutana na...

Mbadi atofautiana na Orengo

adminleo