Makala

MAZINGIRA: Kero ya kugeuzwa dampo vipande vya ardhi visivyo na majumba jijini

August 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MTAA wa Zimmerman ulioko pembezoni mwa Thika Superhighway na sehemu nyingine ikipakana na Kamiti Road, unakua kwa kasi.

Idadi kubwa ya majumba ni ya wapangaji kulipia kodi ama za vyumba na nyumba za kuishi au kufanyia biashara.

Ni mtaa uliositiri viwango tofauti vya watu, kuanzia wale wa mapato ya chini, ya kadri hadi ya juu.

Baadhi ya maeneo, wamiliki wa ploti wanaendelea kufurahia matunda ya kodi za nyumba, mengine yakiendelea kujengwa na ardhi zingine zimesalia mahame.

Hata hivyo, katika ardhi ambazo hazijafanyiwa maendeleo zinapaka tope sifa na taswira ya kuridhisha ya mtaa wa Zimmerman.

Malalamishi yameibuka kufuatia utupaji taka kiholela katika ardhi ambazo hazijajengwa. Aidha, zimegeuzwa kuwa dampo la taka za kila aina.

Katika mojawapo ya ploti, taka za kila aina zinatoa na kurusha uvundo kwa wapita njia.

“Tumekuwa tukishuhudia hali hii kwa muda wa miaka kadhaa. Ardhi zingine, zilizokuwa zimegeuzwa jaa la taka zilijengwa, ziliwapa vibarua wakati mguu kuzisafisha kwa kuzoa taka,” Simon Muchiri, mkazi, ameambia ‘Taifa Leo’.

Taka zilizotupwa kwenye nyingi ya ardhi tulizozuru zina mifuko ya karatasi za plastiki, zilizopigwa marufuku na Halmashauri ya Kitaifa ya Mazingira (Nema) mnamo 2017.

Isitoshe, zina chupa za plastiki, glesi zilizopasuka na kutia katika hatari wanaozoa taka. Jambo lingine la kushangaza ni sodo za wanawake na pia watoto zilizotumika.

Ni hali inayowatia wakazi kiwewe, wakihofia kuugua maradhi yanayosababishwa na uchafu. “Dampo hili ni fichio la mbu (mdudu anayesababisha na kuambukiza ugonjwa wa Malaria), na wadudu wengine hatari,” akalalamika mkazi wakati wa mahojiano.

Kulingana na Humprey Kibara, anayesimamia ploti kadhaa eneo la Zimmerman, ni jukumu la wamiliki wa nyumba za kupangisha kuhakikisha mikakati kabambe kuzoa taka na kuzipeleka zifakofaa, imewekwa.

“Ni uchafuzi wa mazingira unaotekelezwa na wapangaji wenyewe, ikiwa majengo husika hayana mikakati kuzoa taka,” Bw Kibara akasema, akieleza kwamba kila mwezi kila mpangaji wa ploti anazosimamia hutoa ada ya Sh200 kufanikisha uzoaji wa taka.

Huku taifa likiendelea na vita dhidi ya Homa ya corona, wasiwasi kuhusu utupaji kiholela wa maski zilizotumika kwenye majaa na pia kandokando mwa barabara na njia, umeibuka. Utupaji huo wa maski zilizotumika ni hatari, na unahofiwa huenda ukachangia msambao wa Covid-19.