• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
MAZINGIRA NA SAYANSI: Itabidi tususie ‘nyamchom’ kuokoa afya na mazingira

MAZINGIRA NA SAYANSI: Itabidi tususie ‘nyamchom’ kuokoa afya na mazingira

Na LEONARD ONYANGO

KILA Mkenya hula wastani wa kilo 15 za nyama ya ng’ombe, mbuzi na nguruwe, kila mwaka.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na shirika la Kenya Market Trust iliyotolewa mnamo Aprili, mwaka huu, inaonyesha kuwa kiwango cha nyama inayoliwa na kila Mkenya kimeongezeka kutoka kilo tisa kwa mwaka, miaka mitano iliyopita.

Utafiti pia ulifichua kuwa kila Mkenya wa mapato ya juu hula jumla ya kilo 18 huku mwenye mapato ya kadri akibugia kilo 16 za nyama kwa mwaka.

Wakazi wa jiji la Nairobi na Mombasa, kwa mujibu wa ripoti, ndio hula nyama nyingi ikilinganishwa na maeneo mengineyo ya nchi.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya hupendelea kwenda kula nyama katika vituo vya ‘nyama choma’.

Inakadiriwa kuwa ulaji wa nyama, haswa ya ng’ombe, utaongezeka kwa asilimia 75 kote duniani kufikia 2050 licha ya kuwa na athari kwa afya.

Utafiti uliochapishwa, mwezi uliopita, katika jarida la afya la The BMJ Today nchini Amerika, unaonyesha kuwa ulaji wa nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe unasababisha maradhi tele kama vile ugonjwa wa moyo, kisukari, aina fulani za kansa na kadhalika.

Lakini sasa Umoja wa Mataifa (UN) unaonya kuwa ikiwa wewe ni miongoni mwa Wakenya wanaopendelea kula nyama, basi unachangia katika kuongezeka kwa ukame na mafuriko nchini.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mabadiliko ya Hali ya Anga (IPCC) inasema kuwa ulaji wa nyama unachangia katika kurundikana kwa gesi chafu angani. Gesi chafu kama vile kaboni husababisha joto kuongezeka hapa duniani. Joto linapoongezeka, kunatokea ukame katika maeneo mbalimbali ya nchi au mvua kubwa kupita kiasi ambayo husababisha mafuriko.

Wanasayansi 107 waliohusika katika utafiti huo sasa wanataka watu kula chakula kinachotokana na mimea ili kuzuia athari zaidi zinazoletwa na mabadiliko ya hali ya anga.

“Hatutaki kuwaeleza watu ni chakula kipi wanafaa kula. Lakini itakuwa vyema kuachana na nyama kwa sababu za kiafya na kutunza mazingira,” akasema Otto Portner, mmoja wa watafiti hao.

Watafiti hao wanasema kuwa chakula kinachotokana na mimea ni kizuri kwa afya na iwapo watu wataachana na nyama, gesi chafu inayorundikana angani itapungua kwa asilimia 15.

Mbali na kusababisha joto duniani, watafiti pia walibaini kuwa gesi ya kaboni pia inaathiri baadhi ya mazao mashambani.

Wanasema gesi hiyo inapokuwa nyingi angani husababisha mazao kama vile ngano kupunguza kiwango cha vitamini.

Sawa na gesi chafu

Utafiti sawa na huo ulifanywa na Chuo cha Bardjimboni New York, Amerika ambapo wanasayansi walisema kuwa uzalishaji wa nyama ya ng’ombe unadhuru mazingira sawa na gesi inayotolewa na magari.

Kulingana na wanasayansi, kukuza nyasi inayoliwa na ng’ombe huhitaji kiasi kikubwa cha mbolea ambayo huchangia katika uharibifu wa mazingira.

Ng’ombe, mbuzi, kondoo na mifugo wengineo hutoa gesi aina ya ‘methane’ katika kinyesi.

Gesi ya ‘methane’ huchangia katika kuongezeka kwa joto duniani.

Mifugo hao pia huhitaji eneo kubwa la malisho na hilo husababisha uharibifu wa miti na mazingira.

Miti hufyonza asilimia 23 ya gesi aina ya kaboni kutoka angani sababu huitumia kutengeneza chakula chake.

“Tukiendelea kukata miti kiholela bila kupanda mingine, basi kuna hatari ya gesi hatari kuendelea kurundikana angani,” inasema ripoti ya IPCC.

Wataalamu wanasema kuwa huenda nchi mbalimbali zikashindwa kuchukua hatua kupunguza uchafuzi wa anga kutokana na ulaji wa nyama.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fafanuzi na nadharia za fasihi

KWA KIFUPI: Maradhi ya ngozi yanayosababisha mwasho, ukavu...

adminleo