MAZINGIRA NA SAYANSI: Kemikali za kuua wadudu hulemaza ubongo wa mtoto
Na LEONARD ONYANGO
UNASUMBULIWA na kunguni, mbu au mende nyumbani na unalazimika kunyunyizia dawa kila siku kabla ya kulala ili kupata usingizi mwanana?
Au wewe ni mkulima ambaye huenda hunyunyizia mazao dawa ya kuua wadudu ukiwa umeandamana na watoto wachanga? Huenda ‘unaroga’ watoto wako bila kujua.
Wataalamu wanaonya kuwa kuwaweka watoto katika mazingira yaliyo na kemikali za kuua wadudu kwa muda mrefu kunawafanya kuwa mbumbumbu darasani na hata kuathiri tabia zao.
Watafiti wa Chuo Kikuu cha California, Berkeley, Amerika pia walibaini kuwa kemikali hizo pia zinaweza kuathiri ubongo wa mtoto aliye tumboni ambaye hajazaliwa.
Ripoti ya utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Proceedings of the National Academy of Sciences, ulitumia teknolojia inayofahamika kama fNIRS kupima mtiririko wa damu katika bongo za vijana 95 wa kati ya umri wa miaka 15 na 17 waliozaliwa na kulelewa katika eneo la Salinas Valley, California ambapo wakulima hutumia kwa wingi kemikali kunyunyizia mazao yao shambani.
Watafiti hao waligundua kuwa kulikuwa na tofauti katika mtiririko wa damu katika bongo za vijana hao waliofanyiwa utafiti ikilinganishwa na wenzao kutoka maeneo mengine.
“Utafiti ni muhimu kwani umethibitisha tulichokuwa tukiamini kuhusu madhara ya kemikali za kunyunyizia wadudu kwa ubongo wa watoto wachanga, hasa wale ambao hawajazaliwa,” akasema Prof Sharon Sagiv, mmoja wa watafiti hao.
Chuo hicho kilianza kutafiti madhara ya kemikali za kuua wadudu kwa akili ya watoto miaka 20 iliyopita. Watafiti waligundua kuwa kemikali za kuua wadudu hudhuru bongo za watoto kwa kuwafanya kushindwa kung’amua mambo.
Walibaini kwamba watoto hao hawakuwa wanaelewa mambo yanayofundishwa darasani kwa haraka na walikuwa na ugumu wa kuelewa lugha na kupoteza kumbukumbu.
Teknolojia ya fNIRS hutumiwa kufuatilia mtiririko wa damu katika sehemu ya juu ya ubongo.
Waligundua kuwa watoto ambao wamekulia katika maeneo ambapo kemikali ya kuua wadudu inatumika kwa wingi, wana kiasi kidogo cha damu inayosambaa katika sehemu ya juu ya ubongo.
Sehemu hiyo ndiyo inaaminika kuhifadhi kumbukumbu na kuwawezesha watu kujifunza mambo mapya.
Hata hivyo, watafiti hao hawajui hasa kinachosababisha kemikali hizo kuathiri ubongo wa watoto wachanga.
Kemikali feki
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa madhara ya kemikali hizo nchini Kenya huenda yakawa mabaya zaidi haswa ikizingatiwa kuwa nyingi ya kemikali za kunyunyizia wadudu zinazotumiwa ni feki.
Kulingana na mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji Kemikali za Kilimo nchini Kenya (AAK) Patrick Amuyunzu, zaidi ya asilimia 20 ya kemikali za kunyunyizia mazao zinazouzwa humu nchini ni feki.
Anasema kuwa Kenya inapoteza zaidi ya Sh120 bilioni kila mwaka kutokana na uuzaji wa kemikali feki za kunyunyizia mashamba.
Ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na shirika lisilo la serikali la Route to Food Initiative ilionyesha kuwa kemikali zinazotumiwa na wakulima humu nchini ni hatari kwa afya.
Shirika hilo lilionya kuwa asilimia 75 ya kemikali zinazotumiwa kuua wadudu mashambani na nyumbani zimepigwa marufuku barani Ulaya kwa sababu zinasababisha maradhi ya kansa, magonjwa ya kiakili kati ya matatizo mengineyo.
Ripoti hiyo ilisema aina 24 ya kemikali zinazotumiwa na wakulima wa humu nchini zimeorodheshwa kama sumu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kuwa kemikali zinafaa kutumiwa kwa umakini mno.
Kulingana na WHO, kemikali za kuangamiza wadudu zinapotumiwa kiholela ndani ya nyumba, zinaweza kuingia ndani ya maji ya kunywa na vyakula vinginevyo hivyo kusababisha madhara zaidi ya kiafya.