• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
MAZINGIRA NA SAYANSI: Maji ya bahari hayaui virusi vya corona, wataalamu waonya

MAZINGIRA NA SAYANSI: Maji ya bahari hayaui virusi vya corona, wataalamu waonya

Na LEONARD ONYANGO

BAADHI ya wakazi maeneo ya Pwani kama vile Mombasa, Kilifi, Kwale na Lamu wamenukuliwa wakidai kuwa hawawezi kupatwa na maambukizi ya virusi vya corona kwa sababu wana maji ya chumvi na mazingira yao huwa na joto jingi.

Wakazi hao wanadai kuwa kusukutua mdomo kwa maji ya chumvi kutoka Bahari ya Hindi kunasaidia kuua virusi vya maradhi ya corona. Wengine wanadai kuwa virusi vya corona vinakufa mwathiriwa anapokuwa kwenye mazingira yenye joto jingi.

Lakini wataalamu wa afya wanasema kuwa maji ya chumvi na au mazingira yenye joto jingi hayawezi kukusaidia iwapo hautazingatia ushauri uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Kujikinga na virusi vya corona, shirika la WHO linashauri kuwa uepuke kugusa uso, mdomo au pua; unawe mikono mara kwa mara baada ya kusalimiana na watu, uepuke maeneo yenye msongamano wa watu na usikaribiane na mtu anayeonyesha dalili za ugonjwa wa mafua kama vile kukohoa, kuishiwa na pumzi na kuhisi joto jingi mwilini.

Mara baada ya kutokea mkurupuko wa homa ya corona jijini Wuhan nchini China, taarifa zilizodaiwa kutolewa na daktari wa maradhi ya mfumo wa kupumua nchini humo Zhong Nanshan zilidai kuwa maji yenye chumvi yanaweza kusaidia kuua virusi vya maradhi hayo hatari.

Dkt Zhong Nanshan ni mjumbe wa Tume ya Afya ya China ambaye alisaidia pakubwa katika kupambana na homa ya Mfumo wa Kupumua (SARS) iliyokurupuka nchini China mnamo 2002 na kusababisha vifo vya watu 774.

“Tia maji ya chumvi kinywani, inamisha kichwa hadi maji hayo yaguse kooni na kisha upumue kwa utaratibu. Tema maji hayo baada ya dakika moja. Kisha rudia hatua hiyo kati ya mara tatu na tano. Bakteria hutambaa kooni kwa muda mrefu kabla ya kuingia kwenye mfumo wa damu.

“Hivyo, kwa kusukutua na maji ya chumvi bakteria hao hufariki. Wakati wa mkurupuko wa SARS nilihimiza wanafunzi wangu kusukutua midomo yao kwa maji ya chumvi na hakuna hata mmoja aliyeambukizwa maradhi hayo,” ikadai taarifa hiyo.

Madai hayo yamekuwa yakisambazwa katika mtandao ya kijamii na yamewafanya baadhi ya watu kuamini kuwa maji ya chumvi ni tiba ya virusi vya corona.

Lakini Dkt Zhong alijitenga na madai huku akisema kuwa taarifa hiyo inapotosha na hakuna ithibati ya kisayansi kuthibitisha kuwa maji ya chumvi yana uwezo wa kuua virusi vya corona.

Shirika la WHO linasema kuwa hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa maji ya chumvi yana uwezo wa kuua bakteria au virusi.

“Kadhalika, hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa kusafisha mdomo au kinywa mara kwa mara kunaweza kusaidia kutibu homa ya kawaida,” linasema shirika la WHO.

Kulingana na WHO, kula kitunguu saumu pia hakusaidii katika kukabiliana na homa ya corona.

“Hakuna ushahidi kwamba kula kitunguu kumewahi kumlinda yeyote dhidi ya kupatwa na maradhi ya corona,” linasema shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Mbali na maji ya chumvi na kitunguu saumu, kumekuwa na itikadi kuwa virusi vya corona havisambai katika maeneo yaliyo na joto jingi kama vile maeneo ya Pwani, Kaskazini Mashariki na Magharibi mwa Kenya.

Habari hizo zilianza kuenea baada ya Dkt Stefan Baral wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins cha nchini Amerika mwezi uliopita kudai kuwa maambukizi ya virusi vya corona yatapungua kwa kiasi kikubwa wakati wa kiangazi nchini humo.

Kauli sawa na hiyo pia ilitolewa na Dkt John Nicholls, mtaalamu wa maambukizi ya viini katika Chuo Kikuu cha Hong Kong aliyenukuliwa akisema kuwa kuna mazingira aina tatu ambayo virusi vya corona havipendi: mwangaza wa jua, maeneo yenye joto jingi na unyevunyevu.

“Mwangaza wa jua unazuia virusi vya corona kukua na hufariki baada ya dakika 2 ikilinganishwa na gizani ambapo huwa hai kwa zaidi ya dakika 20,” akasema Dkt Nicholls kama alivyonukuliwa na shirika la habari la Ujerumani, Deutsche Welle.

Rais wa Amerika Donald Trump mwezi uliopita alidai kuwa homa ya corona itatoweka nchini humo kuanzia Aprili nchi hiyo itakapoanza msimu wa kiangazi.

“Ni kweli kwamba kunapokuwa na joto jingi virusi vya corona vinatoweka tu,” akadai Rais Trump alipokuwa akihutubia wafuasi wake katika eneo la New Hampshire, Februari 10, 2020.

Wataalamu wa afya wanakiri kuwa maeneo yenye joto jingi yanaweza kupunguza kusambaa kwa viini huku wakionya kuwa itakuwa ni kazi bure iwapo watu hawatazingatia kanuni za kuepuka virusi vya corona.

Utafiti uliofanywa nchini Ujerumani na kuchapishwa katika jarida la kitafiti la Journal of Hospital Infection ulibaini kuwa virusi vya corona vinaweza kusalia hai kwa siku kadhaa hata katika maeneo yaliyo na joto la zaidi ya sentigredi 25.

Mara nyingi maeneo ya Pwani, haswa Mombasa huwa na joto la kati ya sentigredi 20 na 35.

Kwa mfano, virusi vilivyosababisha maradhi ya SARS viliishi kwenye vitu vigumu katika mazingira ya zaidi ya sentigredi 25C kwa siku tano.

Wataalamu, hata hivyo, wanakiri kuwa maeneo yenye baridi yana visa vingi vya maambukizi ya homa ya corona.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Ndimu kutibu COVID-19 ni ‘Fake...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Mbona hedhi nzito katika umri...

adminleo